Alhamisi, 14 Desemba 2017

TAARIFA KWA UMMA

 JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA          

MAHAKAMA

TAARIFA KWA UMMA
Kumekuwa na taarifa inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kupitia bango la kitambaa lililoandikwa ujumbe kwenda kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ujumbe huo ukimtuhumu Mhe. Frederica Mgaya (Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu) kudhulumu haki ya kurithi kwenye Shauri la Mirathi Namba. 81 la mwaka 2006. Ujumbe huo unamwomba. Mhe Rais kumwajibisha Jaji Mgaya.

Mahakama ya Tanzania inapenda kuufahamisha Umma kuwa taarifa hiyo si ya kweli, na tunapenda kutoa ufafanuzi wa kuhusu suala linalolalamikiwa kama ifuatavyo:
                        Kwamba, Mhe. Jaji Mgaya hajawahi kusikiliza shauri la mirathi Na. 81/2006 na wala Mahakama ya Ardhi ambayo Jaji huyo alikuwa akifanya kazi haina mamlaka ya kusikiliza mashauri ya mirathi;

                        Kwamba, Mhe. Jaji Mgaya amewahi kusikiliza shauri la Ardhi Na. 329/ 2015, hata hivyo wanaotoa ujumbe huo hawakuwa sehemu ya shauri hilo.
                        Kwamba baada ya uamuzi wa shauri Na. 329/2015 kutolewa, mlalamikaji aliandika malalamiko yanayoonyesha kuwa aliona amenyimwa haki kwani alitamani awe sehemu ya shauri hilo. Hatua za kisheria zilichukuliwa na Mahakama na kulifunguliwa shauri la Mapitio (Revision) namba 6 la mwaka 2017 katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania.

                        Siyo kweli kwamba Jaji ameiba jalada la Mahakama kwani jalada hilo limeitishwa Mahakama ya Rufani kwa ajili ya mapitio baada kupokea malalamiko toka kwa mlalamikaji.

                        Shauri la Mapitio (Revision) bado linaendelea katika Mahakama ya Rufani na anayelalamika katika bango alifika Mahakamani mwezi Julai, 2017 shauri  lilipopangwa kusikilizwa.

                        Aidha, kutokana na suala hilo kuwa bado liko Mahakamani na linasubiri uamuzi wa Mahakama, Mahakama ya Tanzania kwa sasa inazuiliwa  kutoa maelezo ya kina juu ya masuala mengine yaliyolalamikiwa.
Mahakama ya Tanzania inauhakikishia Umma kwamba itaendelea kutoa huduma kwa misingi ya Katiba na sheria za nchi bila upendeleo huba wala chuki.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI
MAHAKAMA YA TANZANIA.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni