Na
Lydia Churi
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewakumbusha na kuwasihi viongozi wote wa Serikali
wenye mamlaka za kikatiba na kisheria kubaki ndani ya maeneo yao ya kikatiba na
kujiepusha kuingilia maeneo yaliyo ndani ya Haki, Hadhi na Mamlaka ya Kikatiba ya
Mahakama.
Akizungumza leo jijini
Dar es salaam Jaji Mkuu amesema kuwa Mahakama haitasita kumchukulia hatua mtu yeyote
atakayeingilia Mamlaka ya Kikatiba ya Mhimili huo. Pia amewakumbusha Majaji na Mahakimu
kuhakikisha wanalind a hadhi na uhuru wa Mahakama kwa kuwachukulia hatua wale
wanaovunja amri halali za Mahakama.
“Niwakumbushe kwamba anayelinda
hadhi na uhuru wa Mahakama ni Hakimu, Jaji na Mahakama husika, kama umetoa amri
unaona kuna mtu anaivunja, mwite na kumuuliza kwa nini asichukuliwe hatua”,
alisisitiza Jaji Mkuu.
Akitolea mfano wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof. Juma alisema Mhimili huo unapoingili wa
Mamlaka yake ya kikatiba, muhusika huitwa mbele ya kamati, kuhojiwa na kuchukuliwa
hatua, hivyo aliwataka Mahakimu na Majaji nao kuchukua hatua kwa yeyote atakayeingilia
Mhimili wa Mahakama.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam. Wa pili kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali na wa pili kulia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hussein Kattanga. Wa kwanza kushoto ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Katarina Revokati na wa kwanza kulia ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ilvin Mugeta.
“Nawakumbusha wananchi na
viongozi mbalimbali nje ya Mahakama kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania,
mamlaka ya Utoaji haki ni ya Mahakama tu”, alisema.
Alisema Sheria ndiyo inayoipa
nguvu Mahakama na kutaka kila Mhimili kubakia kwenye eneo lake na Mamlaka yake ili
kusiwepo na migongano.Aliongeza kuwa kuanzia sasa Majaji na Mahakimu watakuwa wakali
kwa yeyote atakayeingilia uhuru wa Mahakama.
“Mahakama haiingilii Mamlaka
aliyopewa mwinginekama vile Mamlaka ya Polisi, Mwendesha Mashitaka, Takukuru ama
Taasisi nyingine yeyote, Hakimu au Jaji hawezi kuingilia, hivyo tunawataka waliopewa
Mamlaka yao wabaki huko waliko, na tukifanya hivyo hatutakuwa na migongano yoyote,” alisema Jaji Mkuu.
Naye Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali alisema kasi ya usikilizwaji wa mashauri
katika Mahakama za ngazi zote nchini ni ya kubwa. Alisema Mahakama imefanikiwa kupunguza
idadi ya hukumu ambazo bado hazijatolewa.
Alisema mwaka 2017
wakati wa kuanza kwa mwaka wa Mahakama, kulikuwa na jumla ya hukumu 880 ambazo hazijatolewa
lakini hivi sasa kuna hukumu 440 ambazo bado hazijatolewa lakini muda wa kutoa hukumu
hizo bado haujamalizika. Baada ya shauri kumaliza kusikilizwa hukumu inapaswa kutolewa ndani ya siku 90.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali akizungumza na Waandashi wa Habari leo jijini Dar es salaam. Kushoto Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Katarina Revokati.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni