Ijumaa, 16 Februari 2018

SUALA LA ELIMU KWA MADALALI LIPEWE KIPAUMBELE ASEMA JAJI KIONGOZI

Na Magreth Kinabo

 Jaji Kiongozi  wa Mahakama Kuu  ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali, amefungua Kongamano  la wadau  mbalimbali  wa Mahakama  wanaoratibu  na kusimamia  utekelezaji wa amri  za Mahakama wakiwemo  madalali, ambapo amesema  suala  la elimu  kwa madalali  lipewe kipaumbele.
 Kauli hiyo ilitolewa leo na Jaji Kiongozi huyo wakati akifungua Kongamano la Mazungumzo  ya wadau  kujadili rasimu   ya mtaala  wa mafunzo kwa Madalali wa Mahakama na Wanaopeleka  hati za Mahakama yanayoendelea  katika Kituo cha Mafunzo Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Jaji  kiongozi  huyo , amewataka  wadau  wa Mahakama  kuweka kipaumbele suala  la elimu  kwa madalali ikiwa  ni njia mojawapo ya kuongeza ujuzi na kuhakikisha  wanafanyakazi kwa weledi na maadili  yanayotakiwa.
“Ni  suala lisiloweza kubishaniwa na yeyote mwenye ufahamu wa elimu  kuwa ni muhimu  kuendelea  kujifunza kwani huwezi  kujua  kila kitu,” alisisitiza  Wambali.
Aliongeza kwamba suala la kujifunza  siku zote  lazima lipewe kipaumbele na kilammoja katika fani hii muhimu  na nyingine.

Aidha  Wambali aliongeza kwamba  madalali  wa Mahakama  na wale wanaopaswa  kupeleka  hati  za kuitwa  kwenye mashauri wanaowajibu mkubwa  katika kuhakikisha kuwa amri  mbalimbali  zinazotolewa na Mahakama hususani  katika mashauri ya madai  zinatekelezwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizowekwa.

“ Kwa  hali  hiyo , kazi  ya utekelezaji wa amri  za mahakama inatakiwa  kuhudumiwa  au kuongozwa na watu wenye uaminifu, maadili ya hali ya juu, bali pia wenye ujuzi na upeo  na uzoefu  wa hali ya  Juu kuhusu sheria na kanuni zinazohusu  upelekaji taarifa, uendeshaji  mashauri na utekelezaji wa maamuzi.
Alisema   pamoja  na ukweli  kuwa mwaka 1997 zilitungwa kanuni kuhusu uteuzi, maslahi na usimamizi wa madalali wa Mahakama na wengi wa madalali  waliendelea  kuifanya  kazi yao , bado hakukuwahi kuwa  na mafunzo  yoyote rasmi ya kuwafanya wapate ujuzi  zaidi wa utekelezaji wa kazi zao ukiacha  yale ya dharura  yaliyofanyika mwaka 2003 kwa wale wa Dar es Salaam na Mtwara.

Hali hiyo  ilisababisha  malalamiko mengi   kutoka  kwa wadaawa na umma  kwa ujumla  kuhusu mapungufu yaliyojitokeza ikiwemo ukiukwaji  wa taratibu na ukosefu wa maadili katika utekelezaji wa majukumu   ya madalali.
Wambali  alifafanua kwamba kutokana na changamoto kadhaa Mahakama ilifanya marekebisho kuhusu namna  ya kuwapata madalali, kusimamia  nidhamu na maadili , maslahi na jinsi ya kutekeleza majukumu yao. Ni kwa sababu hiyo Sheria (Taarifa  ya Serikali  namba  363 ya 2017)ilitungwa na kuchapishwa  tarehe 22/9/2017 hivyo ,sheria hiyo imefuta ya sheria ya 1997.

“ Ni matumaini  yangu  kuwa sheria hii itakuwa muarobani  wa changamoto nyingi zilizokuwa zimejitokeza badala ya kuwa ni kikwazo cha mabadiliko.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama(IJA) Dkt. Paul  Kihwelo alisema  ili kuondokana na lawama za madalali ambazo kimsingi zilikuwa  zikirejeshwa kwa Mahakama , Mahakama iliamua kutunga kanuni  mpya za 2017 zinazosimamia shughuli  za  na wasambaza wito.
Pamoja  na mambo  mengine  kanuni hizo mpya  zimeongeza mambo mawili ; imetenganisha Dalali  wa Mahakama na Msambaza Wito na Amri za Mahakama.

Dkt. Paul alisema kila mtu  anayekidhi vigezo vya kuwa dalali,  au msambaza wito na amri  za mahakama apate Cheti  cha Uthibitisho  kutoka  Chuo  cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ama  chuo kingine  kinachotambuliwa  na Kamati  ya Nidhamu na Uteuzi wa Madalali na Wasambaza wito  na Amri  za Mahakama ambayo mwenyekiti wake  ni Mheshimiwa Jaji Kiongozi


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinad Wambali akitoa hotuba katika Kongamano hilo.

 Baadhi ya wadau  wa mkutano wa Kongamano la  kujadili rasimu ya  mtaala wa mafunzo kwa madalali wakiwa katika kongamano hilo  na siku mbili.

 Baadhi ya wadau  wa mkutano wa Kongamano la  kujadili rasimu ya  mtaala wa mafunzo kwa madalali wakiwa katika kongamano hilo  na siku mbili.




Baadhi ya wadau  wa mkutano wa Kongamano la  kujadili rasimu ya  mtaala wa mafunzo kwa madalali wakiwa katika kongamano hilo  na siku mbili.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinad Wambali(wa tatu  kutoka  kushoto) akiwa katika  picha  ya pamoja na  baadhi  ya viongozi  wa Mahakama  mara baada ya kufungua    Kongamano hilo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni