Alhamisi, 15 Februari 2018

MAHAKAMA NA WADAU WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI KATIKA KUTATUA MIGOGORO YA KAZI


Na Lydia Churi
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali amewataka watumishi wa Mahakama pamoja na wadau wake wanaohusika na utatuzi wa migogoro ya kikazi kushirikiana na kuimarisha maadili ya kitaaluma ili kuondokana na malalamiko kuhusu rushwa.

Akifungua Mkutano wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi pamoja na wadau wake leo jijini Dar es salaam, Jaji Wambali alisema Watumishi wa Mahakama pamoja na wadau wanapaswa kufahamu kuwa wanalo jukumu kubwa la kutoa haki kwa wakati, kwa ubora na kwa weledi wa hali juu ili wawe ni sehemu ya furaha kwa wale wanaofika kupata huduma.

Aidha, Jaji kiongozi aliwataka watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi pamoja na wadau wake kushirikiana katika kutatua migogoro ya kikazi  ili kujenga Taswira nzuri kwa Mahakama.

Akizungumzia kasi ya utatuzi wa migogoro ya kazi na utoaji wa haki, Jaji Wambali alizitaja sababu zinazorudisha nyuma kasi hiyo kuwa ni umakini mdogo wa uandaaji wa nyaraka mbalimbali zinazowasilishwa Mahakamani kwani kwa kutokuwa makini kumesababisha migogoro mingi ya kazi kuchelewa kumalizika.

Alizitaja sababu nyingine kuwa ni pamoja na Waajiri na waajiriwa kutumia wawakilishi wenye uwezo mdogo, na kutuma wawakilishi wasiokuwa na mamlaka ya kufanya maamuzi.

Baadhi ya wadau wa Mahakama katika utatuzi wa migogoro ya kazi ni pamoja  na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Ofisi ya Kamishna wa Kazi,  Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Vyama vya Wafanyakazi vikiongozwa na Shirikisho lao-(TUCTA, Mawakili, na Shirika la Kazi Duniani (ILO).

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa Alex amewataka wadau pamoja na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati ili kuvutia wawekezaji, kuongeza tija mahala pa kazi na kukuza uchumi wa nchi.

“Kukua kwa uchumi wa viwanda  kutachochewa na nguvu kazi yenye ujuzi inayofanya kazi kwa utulivu pasipokuwa na migogoro ya kikazi, hivyo kuwepo kwa amani na utulivu kutasaidia kupunguza migogoro mahala pa kazi na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza kwa wingi, alisema Naibu Waziri huyo.  

Akizungumzia kasi ya usikilizwaji wa mashauri, Mhe. Naibu Waziri  alimuomba Mhe. Jaji Kiongozi kuongeza idadi ya Majaji katika Mahakama kuu Divisheni ya kazi ili mashauri yamalizike kwa haraka.

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania-TUCTA, Dkt. Yahaya Msigwa amesema jamii ina uelewa mdogo wa sheria mbalimbali zinazohusu masuala ya kazi pamoja na haki za msingi za wafanyakazi hivyo amewaomba wanasheria kusaidia kuwaelimisha wananchi ili wafahamu haki zao za msingi.

Alisema endepo wananchi watakuwa na uelewa wa kutosha juu ya sheria hizi itasaidia kupunguza migogoro ya kikazi isiyokuwa ya lazima.

“Katika zama hizi maandamano na migogoro ya kikazi haina tija kwa pande zote mbili yaani kwa watumishi na kwa serikali pia, hivyo ni muhimu wafanyakazi wakazifahamu vizuri sharia za kazi”, alisema Dkt. Msigwa.

Aidha, Dkt. Msigwa amewataka waajiri mbalimbali nchini kuhakikishga wanakaa vikao muhimu na wafanyakazi wao ili kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima makazini.
 Baadhi ya wajumbe wa kikao cha Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi na wadau wanaohusika na utatuzi wa Migogoro ya Kazi wakiwa kwenye Kikao hicho kilichofanyika leo jijini Dar es salaam.

 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Sekretarieti ya Maandalizi ya Kikao cha Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na Wadau wanaohusika na utatuzi wa Migogoro ya Kazi. Wa tatu Kulia ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa Alex na wa tatu kushoto ni Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi Mhe. Lilian Mashaka.
  Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa Mahakama Wa tatu Kulia ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa Alex na wa tatu kushoto ni Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi Mhe. Lilian Mashaka. 
 Wajumbe wa kikao cha wadau wakiwa kwenye kikao hicho leo jijini Dar es salaam.
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali akiwa na  Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye Ulemavu Mhe. Stella Ikupa Alex kwenye kikao hicho.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Ferdinand Wambali (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania mara baada ya kufungua kikao cha Wadau. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni