Ijumaa, 25 Mei 2018

TENDENI HAKI KWA WATUMISHI WALIO CHINI YENU:JAJI MKUU

Na Lydia Churi, Dodoma

Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim hamis Juma amewataka Naibu Wasajili, Watendaji, Mahakimu  pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Mahakama kutenda haki kwa watumishi walio chini  yao kwani kimbilio la Mtumishi anapopata matatizo ni kwa kiongozi wake katika sehemu yake ya kazi.

Akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania leo mjini Dodoma, Jaji Mkuu amesema endapo viongozi hao watajifungia na kutojihusisha na matatizo ya watumishi walio chini yao ni wazi kuwa morali ya utendaji kazi itashuka, tija itakosekana na hivyo wananchi watapewa huduma zisizoridhisha hasa katika kipindi hiki ambapo Mahakama ya Tanzania inaendelea na maboresho ya kisayansi ya huduma zake.
“Kiongozi sehemu ya kazi ni yule anayehamasisha na kuelimisha kwa kuonyesha njia mpya, anasikiliza, anajifunza na anakubali kuwa mfanyakazi anaweza kumfungus macho,” alisema Jaji Mkuu.

Aidha, Jaji Mkuu pia amewataka Viongozi hao kuacha tabia ya ubwana bali watekeleze wajibu wao kwa kuwaongoza watumishi walio chini yao kwa ustaarabu na uadilifu. 
Alisema Mahakama ya Tanzania imeamua kufanya kazi kisayansi na kwa malengo na misingi inayokubalika kwa vitendo na kwa mujibu wa Sheria na itatekeleza hilo kwa kuhakikisha kuwa inakuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano (2016/17-2020/21) kupitia Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania (2015/16-2019/20) ambao unatekelezwa kwenye maeneo matatu muhimu.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni Utawala Bora, Uwajibikaji na Usimamizi wa Rasilima, Upatikanaji wa Haki kwa wakati pamoja na Uimarishaji wa imani ya wananchi kwa Mahakama na ushirikishwaji wa wadau kwenye shughuli za Mahakama.
Jaji Mkuu alisema ili kutekeleza Mpango huo wa Maendeleo wa Taifa, Watumishi wa Mahakama hawana budi kujiona kuwa wao ni sehemu ya mabadiliko na kwamba mabadiliko yaliyopo sasa ndani ya Mahakama yanatokana na wao kutoa huduma bora kwa wananchi.    

Alisema imeshirikisha Watumishi wake katika hatua mbalimbali za kujenga Mpango Mkakati na kutekeleza kwa vitendo. Kupitia baraza la katika utoaji wa huduma za mahakama kuepuka migogoro isiyo ya lazima sehemu za kazi.

Mabaraza ya Wafanyakazi sehemu za kazi yanaundwa kwa mujibu wa Sheria na Miongozo ambayo ni Agizo la Rais namba 1 la mwaka 1970, Sheria ya Utumishi wa Umma namba 8 ya mwaka 2002 pamoja na kanuni zake za mwaka 2003 na Sheria ya Majadiliano ya pamoja katika Utumishi wa Umma Namba 19 ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake za mwaka 2005.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni