Jumanne, 22 Mei 2018

WATUMISHI JIANDAENI KWA MATUMIZI YA TEHAMA: JAJI MKUU

Na Lydia Churi-Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amefungua kikao kazi cha Majaji cha kutathmini na kuupitisha Mfumo Mpya wa kuhifadhi takwimu na taarifa za mashauri wa Mahakama ya Tanzania (JSDS) mjini Dodoma na kuwataka Majaji, Mahakimu na Watendaji wengine wa Mahakama kubadili fikra na kujiandaa kwa matumizi ya Tehama.


Akifungua kikao hicho kilichowakutanisha baachi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na Majaji Wafawidhi wa kanda na Divisheni za Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji Mkuu  amesema Mahakama haiwezi kukwepa Matumizi ya Tehema kwenye kazi zake wakati tayari Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilishatunga sheria kukubali mabadiliko haya ikiwemo Sheria ya Miamala ya kielekitroniki ya mwaka 2015 pamoja na Sheria ya Makosa ya kimtandao ya mwaka 2015.

Amesema hivi sasa tayari Mahakama ya Tanzania imeshaingia kwenye matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenye huduma zake za utoaji wa Haki kwa kuwa imeshatayarisha ‘ICT Road Map’ ikiwa ni sehemu muhimu ya Mpango Mkakati wake wa miaka mitano.

Amesema kuwa awamu ya kwanza katika kuingia kwenye Tehama ni kuanza kutumika kwa mfumo wa kuhifadhi takwimu na taarifa za mashauri kupitia Tovuti ya Mahakama.
Jaji Mkuu amesema ni mfumo unaotoa taarifa na takwimu za mashauri ambao hutumika kama nyenzo inayoweza kupima utendaji kazi katika ngazi yoyote ya Mahakama na huwezesha kujua hatua ya kila shauri ilipofikia baada ya kusajiliwa Mahakamani.

Aidha, Jaji Prof. Juma amesema Mahakama imejenga ushirikiano wa karibu na Serikali ili kufikia hatma ya kuungaisha Mahakama zote kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Akielezea hatua iliyofikiwa na Mahakama katika matumizi ya Tehama, Jaji Mkuu amesema Mhimili huo umepiga hatua kadhaa katika matumizi hayo ikwemo upatikanaji wa watumishi wenye utaalamu na ujuzi wa masuala ya Tehama, kuunganishwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, ongezeko la ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mifumo ya Benki ya kujiunga kwenye mfumo wa Serikali, kutumika kwa mfumo wa utambuzi wa mahitaji ya Mahakama (Court Mapping) na ukusanyaji wa takwimu za mashauri kwa mfumo wa JSDS.

Amesema Mahakama inasimamia na kutekeleza ahadi kwa watanzania iliyotoa wakati wa siku ya Sheria nchini mwaka huu ya kuhakikisha imejiwekea malengo ya kuongeza uwazi na ufanisi katika masuala ya utawala na uendeshaji wa mashauri, na Tehama ndiyo jibu sahihi la Mahakama ya karne ya 21 inayolenga Uwazi na Ufanisi.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifungus kikao kazi cha Majaji cha kutathmini na kuupitisha mfumo mpaya wa kuhifadhi takwimu na taarifa za mashauri wa Mahakama ya Tanzania jana mjini Dodoma.
  Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani pamoja na Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania mara baada ya kufungua kikao kazi cha kutathmini na kuupitisha mfumo mpaya wa kuhifadhi takwimu na taarifa za mashauri wa Mahakama ya Tanzania jana mjini Dodoma.

 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani mara baada ya kufungua kikao kazi cha kutathmini na kuupitisha mfumo mpaya wa kuhifadhi takwimu na taarifa za mashauri wa Mahakama ya Tanzania jana mjini Dodoma.
 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania mara baada ya kufungua kikao kazi cha kutathmini na kuupitisha mfumo mpaya wa kuhifadhi takwimu na taarifa za mashauri wa Mahakama ya Tanzania jana mjini Dodoma.
 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji, Naibu Wasajili na Wakuu wa Idara na Vitengo vya Mahakama ya Tanznaia mara baada ya kufungua kikao kazi cha kutathmini na kuupitisha mfumo mpaya wa kuhifadhi takwimu na taarifa za mashauri wa Mahakama ya Tanzania jana mjini Dodoma.
  Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Wataalamu wa Tehama wa Mahakama pamoja na wataalamu wengine mara baada ya kufungua kikao kazi cha kutathmini na kuupitisha mfumo mpaya wa kuhifadhi takwimu na taarifa za mashauri wa Mahakama ya Tanzania jana mjini Dodoma.







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni