Ijumaa, 16 Novemba 2018

MAJAJI WA MAHAKAMA KUU CHINA WAITEMBELEA MAHAKAMA YA TANZANIA KUJIFUNZA MFUMO WA UTOAJI HAKI NCHINI

Na Lydia Churi – Mahakama

Majaji watano kutoka Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Watu wa China wameitembelea Mahakama ya Tanzania ili kujifunza namna mfumo wa utoaji haki wa Tanzania unavyofanya kazi na pia kubadilishana uzoefu kuhusu masuala yakisheria na utoaji haki.

Majaji hao kutoka jimbo la Zhejiang la nchini China pia wameitembelea Mahakama ya Tanzania kwa lengo la kujifunza zaidi na kubadilishana uzoefu hasa kuhusu adhabu zinazotolewa na Mahakama kwa ajili ya kuirekebisha jamii.

Akizungumza na Majaji hao, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati amewaambia kuwa Mahakama ya Tanzania ni chombo huru kinachotekeleza majukumu yake kwa uhuru pasipo kuingiliwa na Mihimili mingine. 

Akizungumzia adhabu zinazotolewa na Mahakama katika kuirekebisha jamii hasa zile za kifungo cha nje, Msajili Mkuu alisema adhabu hizo hutolewa kwa mujibu wa sheria na kwa vigezo mbalimbali ikiwemo kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani na kufanya shughuli za uzalishaji ili kuisaidia jamii.

Alisema Mahakama ya Tanzania imekuwa ikishauri matumizi ya adhabu mbadala ikiwemo kazi za nje badala ya adhabu za kifungo gerezani. Kupitia adhabu hizi, wafungwa watatumika pia kufanya kazi za uzalishaji mali na kuisaidia jamii.

Kwa upande wao, Majaji hao kutoka nchini China wamesema wamefika nchini kujifunza mfumo wa utoaji haki unavyofanya kazi na hasa kuhusu adhabu zinazotolewa na Mahakama katika kuirekebisha jamii kwa kuwa mfumo huo pia hutumiwa na Mahakama zao.

Kwa mujibu wa Majaji hao, China inazo fursa nyingi za kuwaendeleza wanasheria kitaaluma na hivyo wametoa wito kwa Mahakama ya Tanzania kutumia fursa hizo katika kuwaendeleza watumishi wake kama ambavyo nchi nyingine zimekuwa zikifanya.
 Pichani ni Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati (aliyeketi mbele) akiwa katika mazungumzo  ya pamoja na Wahe. Majaji kutoka Mahakama Kuu Zhejiang iliyopo nchini China walipotembelea Ofisi ya Mhe. Msajili Mkuu, Novemba 16, 2018.
 Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati (kushoto) akimpatia zawaji mmoja wa Majaji kutoka Mahakama Kuu Zhejiang nchini China.
Waheshimiwa Majaji kutoka Mahakama Kuu Zhejiang nchini China wakiwa katika picha ya pamoja na Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati (katikati), wa tatu kulia ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Menejimenti ya Mashauri, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya na wa kwanza kulia ni Mtaalamu Mwelekezi wa Mawasiliano-Mahakama ya Tanzania, Dkt. Cosmas Mwaisobwa.


Waheshimiwa Majaji kutoka Mahakama Kuu Zhejiang nchini China wakiwa katika picha ya pamoja walipokuwa katika Ukumbi namba moja (1) wa Mahakama Kuu, Dar es Salaam.
(Picha na Mary Gwera-Mahakama)
 
 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni