Jumatano, 21 Novemba 2018

KANDA YA TANGA WAJIPANGA KUHAKIKISHA TAKWIMU ZA MASHAURI ZINAANDALIWA KWA USAHIHI NA KUWASILISHWA KWA WAKATI


Afisa Utumishi wa Mahakama Kuu, Bwana Faridi Mnyamike (Aliyesimama) akitoa mafunzo ya namna ya uandaaji taarifa na nakala za hukumu.
Na Amina Ahmad, Mahakama Kuu-Tanga
Uongozi wa Mahakama Kanda ya Tanga uliendesha mafunzo elekezi kwa Mahakimu,Watendaji na watumishi wanaoshughulika na uandaaji, uchakataji na uwasilishaji wa takwimu za mashauri ikiwa ni utekelezaji wa nguzo ya pili (2) ya mpango mkakati wa Mahakama.
Miongoni mwa mada zilizotolewa ni pamoja na usafishaji wa mashauri kwenye mfumo wa JSDS II (Data cleanup), ufanikishaji wa utoaji na usambazaji wa nakala za hukumu kwa wadau na posta hadi mlangoni na ujazwaji wa fomu mbalimbali  za takwimu za kimashauri zinazoandaliwa kila mwezi, robo mwaka na mwisho wa mwaka.
Sambamba na mafunzo hayo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Mhe. Amiri Mruma alizindua barua pepe ya wadau wa takwimu za mashauri (statistics tangazone group mail) ambayo itasaidia/kurahisisha usimamizi na uthibiti wa mienendo ya uandaaji na utumaji wa takwimu kwa usahihi na kwa wakati.
Wadau waliohudhuria mafunzo hayo ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Mhe Amiri Rajabu Mruma ambaye pia alikuwa ni mgeni rasmi, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga, Mahakimu Wafawidhi wa Wilaya, Maafisa utumishi na utawala, Afisa Tehama, Wasaidizi wa kumbukumbu na Makatibu Muhtasi.

Katika kikao hicho, jumla ya maazimio kumi na tisa (19) yaliafikiwa yanayolenga kuleta utendaji shirikishi na matokeo chanya katika Nyanja za utendaji wa kila siku wa shughuli za kimahakama na uendeshaji.
 
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Mhe. Amiri Mruma (aliyesimama) akizungumza na wadau waliohudhuria mafunzo. Kushoto kwake ni Naibu Msajili Mhe. Francis Kabwe na kulia kwake ni Mtendaji wa Mahakama, Ndugu Ahmed Selemani Ng’eni.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga, Mhe. Desdery Kamugisha akitoa mafunzo ya namna bora ya uandaaji wa takwimu za mashauri.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni