Jumamosi, 24 Novemba 2018

PROF. KABUDI AAHIDI KUKISAIDIA CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA LUSHOTO


Na Ibrahim Mdachi, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb) ameahidi kukisaidia Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa kuwa anatambua mchango wake katika utoaji mafunzo ya Sheria nchini.

Waziri wa Katiba na Sheria  ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za Mahafali ya 18 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Novemba 23 alisema kuwa Serikali inatambua mchango wa Chuo hiki katika kutoa mafunzo ya sheria kwa ngazi ya Stashahada na Astashahada na katika kutoa mafunzo endelevu katika fani mbalimbali za sheria.
 
“Ninaahidi kutimiza wajibu wangu kwa kutoa msaada pale mtakapohitaji na nitakapoona sina budi nitatoa msaada huo hata kama hamjaleta rasmi hitaji lenu kwangu.” Alisema Prof. Kabudi.

Akiendelea kuhutubia hadhara ya Wahitimu, Watumishi wa Chuo na Mahakama Wazazi na Walezi wa wahitimu, Prof. Kabudi aliongeza kuwa wahitimu wa chuo hiki wamekuwa mfano kwa jamii kwa uadilifu na maadili kutokana na malezi wanayopata chini ya usimamizi wa Mahakama ya Tanzania.

Alipongeza Uongozi wa Chuo kwa jitihada unazozifanya katika kukabiliana na changamoto mbalimbali na namna unavyoweza kuzikabili na kuweza kutekeleza jukumu lake la utoaji wa mafunzo sambamba na utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Sambamba na hayo aliwaasa na kuwasisitizia Wahitimu na juu ya kujiendeleza katika fani ya Sheria ambayo huhitaji kusoma kwani sheria na kanuni hubadilika kila mara na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Mhe. Prof Kabudi aliwataka Wahitimu hao kuendelea kusoma vitabu kwa wingi kwani itawasaidia katika utendaji kazi wao wa kila siku.

 Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Jaji, Prof. Paul Kihwelo alisema kuwa Chuo kimeendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa Watumishi wa Mahakama ili kuwajengea uwezo zaidi.

“Kwa kutambua umuhimu wake kwa Mahakama ya Tanzania pamoja na kuwajengea uwezo wa utafiti watumishi wake, Chuo kimeendesha mafunzo yaliyowajumuisha Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo na Wajumbe wa Mabaraza ya Kata mkoani Tabora ili kuwajengea uwezo wa namna wanavyopaswa kusikiliza mashauri katika ngazi zao,” alieleza Mkuu huo wa Chuo. 

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Jaji Dkt. Gerald Ndika alitaja miongoni mwa mafanikio ya Chuo kuwa ni kuboresha utendaji kazi wa Kurugenzi ya Mafunzo Endelevu ya Kimahakama. 

“Nichukue fursa hii tena kwa niaba ya Baraza la Uongozi wa Chuo kutoa shukrani za pekee kwa Mhe. Jaji Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kwa ushirikiano wanaotoa kwa Uongozi wa Chuo, kutoa kipaumbele kwa shughuli za Chuo hususani kutenga fedha za mafunzo kwa maafisa wa mahakama na wasaidizi wao na kuamua kuwa mafunzo yote ya watumishi wa mahakama yaratibiwe na Chuo,” alieleza Mwenyekiti.


Aliongeza kuwa katika utoaji wa elimu bora  chuoni hapo, Chuo kwa sasa kina jumla ya Wanataaluma (Wahadhiri) Ishirini na Tatu (23) ambao wameendelezwa na kuwezesha Chuo kupata mafanikio ya kitaaluma yaliyotajwa. Miongoni mwa Wanataaluma hao, watano (5) wana Shahada ya Uzamivu na kumi na nane (18) wana Shahada ya Uzamili. Kwa sasa kati ya hao 18 wenye Shahada za Uzamili wawili wanafanya Shahada ya Uzamivu na wapo katika hatua nzuri.

Katika Mahafali hayo, Mhe. Waziri alizindua Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Chuo hicho, Mfumo wa Kielektroniki wa Menejimenti ya Mafunzo ‘Training Management Information System (TMIS)’ na Klabu ya utunzaji mazingira ijulikanayo kama ‘IJA Green Club’.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb), ambaye pia alikuwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 18 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto akitoa hotuba.

Sehemu ya Wahitimu wa Stashahada ya Sheria, katika Mahafali hayo jumla ya Wahitimu 345 wamehitimu katika ngazi ya Stashahada na Astashahada.

Sehemu ya Wahitimu wa Astashahada ya Sheria.

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Jaji, Dkt. Paul Kihwelo akitoa neno katika Mahafali hayo.

  Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Jaji Dkt Gerald Ndika akitoa hotuba yake katika Sherehe za Mahafali ya 18 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Maandamano kabla ya kuanza rasmi kwa Sherehe za Mahafali zilizofanyika Novemba 23, 2018 katika Ukumbi wa Nyalali uliopo ndani ya eneo la Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Mhe. Waziri, mgeni rasmi (aliyeshika kipaza sauti) akiongoza sherehe za Mahafala ya ‘IJA’ Lushoto.

Waziri wa katiba na Sheria akipewa maelezo ya jinsi mfumo wa Kielektroniki wa Menejimenti ya Mafunzo ‘Training Management Information System (TMIS)’ unavyofanya kazi, Mhe. Waziri alizingua rasmi mfumo huo ambao utakuwa ukitoa taarifa ya Mafunzo mbalimbali na kuwezesha kujua ni Watumishi wangapi wa Mahakama waliopatiwa Mafunzo na ambao hawajapata mafunzo.

Meza kuu ikiongozwa na Mhe. Mgeni rasmi (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Wahitimu wa Stashahada ya Sheria.
Meza Kuu katika picha ya pamoja na sehemu ya Wahitimu wa Astashahada ya Sheria.

(Picha na Mary Gwera, Mahakama)


 
 
 




 

Maoni 2 :

  1. Maoni haya yameondolewa na mwandishi.

    JibuFuta
  2. Hongera sana maana mahafali yalipendeza sana ila pia tunaomba kama kuna uwezekana kuwa na mpango wa kuanzisha masomo kwa ngazi ya shahada wanafunzi wengi wa IJA tunatamani shahada ingekuepo ili tusome tenĂ  hapo

    JibuFuta