Ijumaa, 15 Februari 2019

JAJI MKUU AFUNGUA MAFUNZO ELEKEZI KWA MAJAJI WAPYA

Na Lydia Churi-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Prof. Ibrahim Hamis Juma leo amefungua mafunzo elekezi kwa Majaji kumi na watano (15) wa Mahakama Kuu ya Tanzania na kuwataka Majaji hao kuwajibika na kuzingatia Maadili na Uongozi bora.

Akifungua Mafunzo elekezi ya Majaji wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania leo katika kituo cha Mafunzo kilichopo Kisutu jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu pia amewataka Majaji hao kuzingatia matumizi ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano (Tehama)  ili kurahisisha upatinaji wa haki.
Akizungumzia suala la uongozi, Jaji Mkuu amewakumbusha Majaji wapya  kutambua kuwa sasa wanao wajibu wa kiuongozi pamoja na ule wa kazi zao za kila siku za kimahakama.

“Kama Viongozi, mnapaswa sasa kufahamu mengi zaidi yanayoihusu Tanzania kwa ujumla pamoja na yale yanayoihusu Mahakama ya Tanzania”, alisema.
Kuhusu uwajibikaji, Jaji Mkuu amewataka Majaji wapya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ili kuimarisha na kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama. Alisema hakuna Mahakama itakayosimama endapo wananchi watakosa imani na heshima dhidi yake.

Akizungumzia Matumizi ya Tehama, Jaji Mkuu amesema matumizi ya Tehama ndani ya Mahakama siyo ndoto tena kwa kuwa hivi sasa kazi nyingi zinafanywa kwa kutumia Tehama ikiwemo kusajili Mashauri, kuhifadhi taarifa mbalimbali pamoja na kusikiliza mashauri. Aliwataka Majaji hao kuhakikisha hawabaki nyuma katika matumizi hayo.
Kuhusu Maboresho ndani ya Mahakama ya Tanzania, Prof. Juma amesema Majaji wapya wanayo bahati ya kuingia ndani ya Mahakama wakati Mhimili huo ukitekeleza Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2015/2016-2019/2020) pamoja na Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama unaodhamiria kusogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi na kuwapatia haki kwa wakati.

Aidha, Jaji Mkuu pia amewashauri Majaji wapya kuendelea kujiongezea ujuzi katika kazi zao. Alisema Majaji bado wanahitaji elimu endelevu ya sheria ili waweze kutatua changamoto za karne ya 21 pamoja na mabadiliko ya kasi ya ulimwengu wa sasa.
Naye Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi alisistiza umuhimu wa Majaji wapya kupatiwa Mafunzo elekezi kwa kuwa mafunzo hayo ni endelevu na muhimu katika utekelezaji wa kazi yao.

Alisema kazi ya Jaji ni ya kipekee hivyo inamtaka mtu kufuata maadili na kutenda haki wakati wote. 
Akizungumzia Mafunzo hayo, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Jaji Dkt. Paul Kihwelo amesema katika mafunzo hayo, Majaji watapata fursa ya kujadili changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo wakati wa kutekeleza wajibu wao, kuzingatia maadili katika kutekeleza majukumu yao,  pamoja na kukumbushana mifumo ya utendaji kazi katika Mahakama ya Tanzania.

Amesema Majaji hao pia watajadili namna mihimili mitatu ya dola inavyofanya kazi bila kuingiliana, usuluhishi kwa njia ya muafaka na uandishi wa hukumu na utoaji wa adhabu.
Ni utamaduni wa Mahakama ya Tanzania, kupitia chuo chake cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kuwapatia mafunzo elekezi nay a awali watendaji wake ili kuwaandaa kuwatumikia wananchi kwa weledi na uadilifu.

Januari 27, mwaka huu, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli aliwateua Majaji 15 wa Mahakama kuu ya Tanzania.

 Majaji 15 Wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo pichani) akizungumza nao leo alipokuwa akifungua mafunzo elekezi ya Majaji hao Kisutu jijini Dar es Salaam.

 Watumishi wa Mahakama ya Tanzania wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza nao leo alipokuwa akifungua mafunzo elekezi ya Majaji wapya.

  Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa pamoja na Majaji wenzake. Wa pili kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi, wa kwanza kulia ni Jaji Mstaafu Mhe. Eusebia Munuo. Wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam Mhe. Beatrice Mutungi na anayefuata ni Jaii wa Mahakama ya Rufani Mhe. Gerald Ndika.

 Majaji wa Mahakama kuu ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja na

Meza kuu.

 Majaji wa Mahakama kuu ya Tanzania (wapya) wakiwa katika picha ya pamoja na

Meza kuu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni