Alhamisi, 16 Mei 2019

JAJI MKUU ASHAURI CHAMA CHA WANASHERIA KUSHIRIKIANA NA MAHAKAMA


Na Waandishi-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amekishauri chama cha wanasheria cha Tanganyika Law Society (TLS) kushirikiana na Mahakama katika kutekeleza majukumu yake.

Akizungumza na Rais wa TLS pamoja na ujumbe wake walipomtembelea leo ofisini kwake jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu amesema Mahakama pamoja na chama hicho wanayo maeneo mengi ya kushirikiana pasipo kuingiliana katika majukumu yao.

Aidha, Jaji Mkuu pia amekishauri chama hicho kuwa na mpango kazi wa muda mrefu ili kuongeza ufanisi ndani ya chama hicho kwa kuwa kwa mujibu wa Sheria, viongozi wa chama hicho hukaa madarakani kwa kipindi cha mwaka moja kabla ya uchaguzi kufanyika tena.

Akizungumzia mapambano dhidi ya rushwa katika utoaji wa haki, Jaji Mkuu amewataka Mawakili nao kupambana na rushwa kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa kufuata maadili.

 “Zifanyieni kazi changamoto za rushwa na shirikianeni na Mahakama ya Tanzania kwa kuwa Mahakama ni mfumo wa kukosoana, alisema Jaji Mkuu.

Kwa upande wake, Rais wa TLS Mhe. Dkt. Rugemeleza Nshala ameiomba Mahakama ya Tanzania kushughulikia changamoto mbalimbali wanazokutana nazo Mawakili wanapotekeleza majukumu yao ya kisheria Mahakamani ikiwemo kuchelewa kuanza kwa kesi mahakamani.

Rais huyo pia aliishukuru Mahakama kwa ushirikiano inaoutoa kwa chama chake na kuahidi kufanya kazi zake kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania.

Naye Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezar Feleshi amewapongeza viongozi wapya wa TLS waliochaguliwa hivi karibuni na kuwashauri kufanya kazi kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania.

“Mifumo yetu iko wazi nasi tuko tayari kufanya kazi nanyi kwa kuwa wote tunayo nia moja ya kumtumikia mwananchi”, alisema Jaji Kiongozi. 

Wakati huo huo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bwn. Hussein Kattanga amewashauri viongozi wa TLS kushirikiana na Mahakama katika kutatua changamoto mbalimbali za upatikanaji wa haki na kuwataka kuwasilisha hoja na malalamiko kwa kuwa Mahakama kwa sasa inapokea hoja, maoni na malalamiko ili kuboresha huduma zake.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizunzumza na viongozi wa Chama cha Wanasheria  Tanganyika (TLS) walipomtembelea mapema Mei 16, 2019 ofisini kwake  Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kulia  kwake ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi,  anaefuata ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga, kushoto kwake ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika  (TLS)  Dkt. Rugemeleza Nshala, anaefuata ni Makamu wa Rais wa Chama hicho Bw. Mpale Mpoki , pamoja na wajumbe wengine walioshiriki katika mazungumzo hayo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. ibrahim Hamis Juma akisisitiza jambo wakati akizungumza na ujumbe kutoka Chama cha Wnasheria Tanganyika, ukiongozwa na Rais wa chama hicho, Dkt. Rugemeleza Nshala.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akizungumza na ujumbe huo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga akichangia jambo katika mazungumzo hayo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (TLS)  Dkt. Rugemeleza Nshala (kushoto kwa Jaji Mkuu) pamoja na wajumbe wengine. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni