Jumatano, 2 Oktoba 2019

MAHAKAMA KUU KANDA YA DAR ES SALAAM KUSIKILIZA KESI 3,372


Na Aziza Muhali- (SJMC)

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, inaendelea kusikiliza kesi 3,372 zilizosajiliwa Mahakamani hapo kwa sasa, zikiwamo za madai, jinai na ardhi.

Hayo yamesemwa na Naibu Msajili Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Joachim Tiganga, wakati akitoa elimu kwa umma kuhusu utoaji wa huduma  zinazotolewa  na mahakama hiyo, uliofanyika leo, Oktoba 2, mwaka huu katika ukumbi wa Mahakama Kuu, uliopo jijini Dar es Salaam.

Mhe. Tiganga  alisema  lengo la kutoa elimu hiyo  kwa wananchi ni kueleza huduma zinazotolewa na mahakama hiyo pia kupokea maoni na mapendekezo kutoka kwa wateja wao.

Akifafanua kuhusu kesi hizo, alisema kesi zinazoripotiwa kwa wingi ni kesi za madai ya kawaida ambazo ni 2,169 zikifuatiwa na kesi za jinai 789, wakati kesi za ardhi ni 354.

“Hivyo kutokana na idadi hiyo ya kesi, jaji mmoja anasikiliza kesi zipatazo 450 kwa mwaka badala ya kesi 220 kutokana na kuwepo kwa idadi ndogo ya majaji” alisema.

Aliongeza kuwa Mahakama hiyo ina jumla ya majaji saba, wakati idadi kamili inayohitajika ni 15, hivyo ina upungufu wa majaji 8. 

Akizungumzia kuhusu ukataji rufaa, ambapo baadhi ya wananchi walitaka kufahamu juu ya utaratibu wake,ambao ni Farida Mwalwaka mkazi wa Toangoma na Ally Idd mkazi  wa Majimatitu, jijini Dar es Salaam, alisema kwamba mahakama  huwawezesha wateja wake kukata rufaa kwa kuwapatia nakala za kumbukumbu zote za kesi.

Aidha  Tiganga  aliwataka wananchi wenye malalamiko kuhusu uendeshwaji wa kesi mbalimbali  kufika katika dawati la malalamiko ambalo hufanyika siku ya Jumanne na Alhamisi kila wiki. 

Kwa upande wake Hakimu Mhe. Joyce Karata, amewataka wananchi kuwa makini wakati wa utaratibu wa ukataji wa rufaa ambapo amesema kuwa rufaa inatakiwa kukatwa ndani ya muda, ili kuondoa usumbufu wa upatikanaji wa nyaraka.


Naibu Msajili Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Joachim Tiganga akitoa elimu kwa umma kuhusu huduma zinazotolewa na mahakama hiyo kwa wananchi.Kushoto ni Hakimu Mhe. Joyce Karatu.
Baadhi ya wananchi wakisiliza elimu iliyokuwa ikitolewa na Naibu Msajili Mfawidhi huyo.

Baadhi ya wananchi wakisiliza elimu iliyokuwa ikitolewa na Naibu Msajili Mfawidhi huyo.

Mzee Ally Iddy (katikati) akiuliza jambo kuhusu taratibu za ukataji wa rufaa.
Bi. Farida Mwalwaka (aliyevaa ushungi) akiuliza jambo kuhusu masuala ya hukumu.


(Picha na Magreth Kinabo)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni