Ijumaa, 29 Novemba 2019

JAJI MKUU - ATAKA ELIMU YA SHERIA KUWA SILAHA


Na Magreth Kinabo - Mahakama, Lushoto
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka wahitimu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) kutumia silaha ya elimu ya sheria kuitumikia jamii kikamilifu.

Aidha, Jaji Mkuu amesema kwamba wahitimu hao wanapaswa kuinoa elimu hiyo kila wakati ili silaha hiyo iwe na nguvu ya kuibadilisha dunia.

Prof. Juma alisema hayo katika sherehe za mahafali ya 19 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa wahitimu wa Stashada na Astashahada ya Sheria, yaliyofanyika leo Novemba 29, mwaka huu chuoni hapo, wilayani Lushoto mkoani Tanga. 

 ‘Katika fani ya sheria, moja ya njia ya kuinoa silaha hiyo ni kujisomea kila wakati kwa sababu sheria na kanuni huwa zinabadilika mara kwa mara. Sio vyeti vyenu vitakavyofanya kazi ya kutoa huduma. Kwa kuhitimu hivi leo haina maana kwamba mtakuwa mmemaliza kujifunza masuala yote ya kisheria.

‘Bali mnapaswa kuendelea kuwa wanafunzi kila wakati ili kujua sheria mpya na kanuni zake pindi zinapobadilika. Mhitimu mzuri ni yule anayeacha milango wazi ya kujifunza kutoka kwa wengine’.alisema Jaji Mkuu.

 Jaji Mkuu aliwaasa wahitimu hao, popote pale watakapokuwa kujifunza jambo jipya kila siku ili wasipitwe na wakati ili kutoiaibisha fani yao, hivyo  wajiendeleze hadi kufikia viwango vya juu kabisa katika fani hiyo muhimu.

 ‘Jengeni tabia ya kujisomea wenyewe vitabu ili kuendelea kujielimisha. Kamwe usimtegemee mtu mwingine asome kisha akuelekeze. Katika kujisomea, hakikisheni mnasoma pia mambo yasiyo ya kisheria kwa mfano hivi karibuni, Mhe. Benjamin William Mkapa (Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu) alizindua kitabu chake “My Life” My Purpose, A TANZANIA PRESIDENT REMBERS”,’ alisisitiza.

Alisema  kitabu hicho  kitawaongezea ufahamu wa historia ya nchi yetu kupitia miaka 81 ya maisha ya Rais huyo wa Awamu ya Tatu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa chuo hicho, lililomaliza muda wake, Mhe.Jaji Dkt. Gerald Ndika, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, alisema mahafali haya ya 19, yamefanya jumla ya wahitimu 6,037 katika ngazi ya Stashahada na Astashada ya Sheria tangu kilipoanzishwa mwaka 2001.

Naye Mkuu wa chuo hicho, Mhe Jaji  Dkt.Paul Kihwelo alizitaja  takwimu za wahitimu hao kwa mwaka huu, kwa upande wa Stashahada ya Sheria kati ya wahitimu  169 wanaume ni 93 (55.03%) na wanawake 76 (44.97%) na kwa upande wa Astashahada ya Sheria, kati ya wahitimu 234 wanaume ni 102 (43.59%) na wanawake ni 132 (56.41%).

Mahafali hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali, pia baadhi wahitimu walizawadiwa vyetieti, vitabu pamoja na fedha taslimu kutoka chuo hicho na  Mahakama yaTanzania.

Pia wahitimu bora wawili kutoka kutoka ngazi hizo, waliopata wastani wa daraja   ‘A’ katika somo la mwenendo wa mashauri ya  madai na jinai  walipewa zawadi kutoka kwa  Jaji Mkuu.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma(aliyevaa kofia nyekundu)   akiwa katika maandamano ya mahafali ya 19 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).Wengine ni  baadhi ya wahadhiri wa chuo hicho na viongozi wengine. Maandamano  hayo yamefanyika leo, Novemba 29, mwaka huu.



Wanafunzi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wa ngazi ya Astashahada ya Sheria wakiwa katika  mahafali  hayo.



Wanafunzi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto  (IJA) wa ngazi Stashahada ya Sheria wakiwa katika mahafali hayo.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma (kulia) akizindua nembo ya kuadhimisha  miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto  (IJA), ambayo ni ishara ya kuanza kwa shughuli mbalimbali za kusherehekea miaka hiyo.  Kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho lililomaliza muda wake.Mhe. Dkt. Gerald Ndika, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma (katikati) katika picha ya pamoja na wahitimu bora kitaaluma wa ngazi ya Stahada na Astashatada ya Sheria wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto  (IJA).

 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim  Hamis Juma amkipatia zawadi mhitimu bora wa ngazi Astashahada ya Sheria, Saida Rajabu aliyepata wastani wa daraja   ‘A’ katika somo la mwenendo wa mashauri ya  madai na jinai hizo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru (kulia wa tatu) akizungumza jambo na Balozi Mteule, Mhe. Hussein  Kattanga (kulia wa nne).


 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma akitoa hotuba

 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma, (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, waliomaliza muda wao.

 Jaji Mkuu  wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma, (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi wahitimu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto  (IJA) wa ngazi Stashahada ya Sheria.

Jaji Mkuu  wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma, (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi wahitimu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto  (IJA) wa ngazi Astashahada  ya Sheria.


(Picha na Magreth Kinabo na Ibrahim Mdachi-Lushoto).




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni