Jumatatu, 2 Desemba 2019

JSDS II KUWA CHANZO RASMI CHA TAARIFA ZA MASHAURI MAHAKAMANI


Na Mary Gwera, Mahakama-Arusha

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema kuwa kuanzia Januari 01, 2020 taarifa zote za mashauri zitaanza kuchukuliwa rasmi kupitia Mfumo wa kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (JSDS II).

Akifungua rasmi Mafunzo elekezi kwa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na baadhi ya Majaji wa Mahakama hiyo, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa zoezi la utumaji wa takwimu kila mwezi kwenye madodoso, litakoma tarehe 31 Desemba 2019.

“Kuanzia sasa hadi Desemba 31, mwaka huu maandalizi muhimu yanayohusiana na maelekezo haya yafanyike ikiwemo kuhakiki usahihi wa taarifa za mashauri zilizoingizwa katika mfumo wa JSDS II na kuhakikisha kuwa mashauri yote yanaingizwa kwenye Mfumo kama nilivyoelekeza kupitia nyaraka mbalimbali,” alisema Mhe. Jaji Mkuu.

Jumla ya Washiriki 30 wakiwemo Majaji Wafawidhi pamoja na baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu wanashiriki katika Mafunzo elekezi yanayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mkoani Arusha.

“Matumizi ya TEHAMA ni suala ambalo halikwepeki, hivyo ni muhimu kwa kila mmoja wetu kukumbatia teknolojia hususani katika zama hizi za mapinduzi ya teknolojia,” alisisitiza Mhe. Jaji Mkuu.

Aliwataka Viongozi hao wa Mahakama kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa zoezi hili linafanikiwa kwa kuhimiza Watumishi walio chini yao kuwajibika ipasavyo katika zoezi hili muhimu lenye manufaa kwa wananchi.

Mhe. Jaji Prof. Juma aliongeza kuwa mfumo huu utasaidia katika upatikanaji wa taarifa sahihi za mashauri ikiwemo mashauri yaliyofunguliwa katika Mahakama husika, yaliyosikilizwa na kumalizika na vilevile itasaidia kupunguza changamoto mbalimbali ikiwemo upotevu wa majalada ya kesi na kadhalika.

“Vilevile mfumo huu utawawezesha pia wananchi kufuatilia mienendo ya kesi zao kwa njia ya TEHAMA hivyo natoa wito kwa wananchi kutembelea mitandao ya Mahakama ikiwemo tovuti ya www.judiciary.go.tz ili kupata taarifa mbalimbali ikiwemo za mashauri,” aliongeza Mhe. Jaji Mkuu.

Mafunzo hayo ya siku tano (5) yamelenga katika kuboresha utendaji kazi wa Viongozi hao ambao ndio wawakilishi wa Mhe. Jaji Mkuu katika maeneo yao ya kazi vilevile watapata fursa ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano (5) (2015/2016-2019/2020) ikiwemo pia kuja na vipaumbele vya mpango mkakati ujao. 


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifungua rasmi Mafunzo elekezi ya siku tano (5) kwa Wahe. Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu yanayofanyika katika Ukumbi wa ‘EAC’ jijini Arusha.
 Wahe. Majaji wakifuatilia hotuba ya ufunguzi kutoka kwa Mhe. Jaji Mkuu.

Jaji Kiongozi-Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akizungumza na Wahe. Majaji katika Mafunzo hayo.

  Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Bw. Mathias Kabunduguru akitoa neno kwa Wahe. Majaji.

 Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna akitoa neno.
 Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto (IJA), Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo akizungumza jambo na Wahe. Majaji.
 Meza Kuu ikiwa katika picha ya pamoja na Wahe. Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu pamoja na baadhi ya Majaji wa Mahakama wanaoshiriki katika Mafunzo jijini Arusha. Katikati ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, wa pili kushoto ni Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna, wa kwanza kulia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto (IJA), Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo na wa kwanza kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Bw. Mathias Kabunduguru.


Meza Kuu na baadhi ya Watendaji na Maafisa wa Mahakama walioshiriki katika mafunzo hayo.
 Meza kuu katika picha ya pamoja na mmoja wa Wawezeshaji wa Mafunzo kutoka chuo cha ‘ESAMI’ Prof. Dkt. Michael Munkumba.


 (Picha na Mary Gwera, Mahakama)








Hakuna maoni:

Chapisha Maoni