Jumatatu, 17 Februari 2020

JAJI MKUU:UONGOZI MADHUBUTI NI MSINGI WA MABORESHO


Na Mary Gwera, Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemueleza Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Meaza Mengistu kuwa uongozi imara ni moja ya chachu ya maboresho yaliyofikiwa na Mahakama ya Tanzania katika utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya huduma za Mahakama nchini.

Mhe. Jaji Mkuu aliyasema hayo wakati akizungumza na Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Mengistu aliyemtembelea mapema Februari 17, 2020 ofisini kwake, Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam kwa lengo la kupata uzoefu wa Mahakama ya Tanzania juu ya suala zima la maboresho na muundo wa utendaji kazi wa Mahakama.

“Mchakato wa maboresho ya Mahakama umekuwa shirikishi kwa kuhusisha ngazi zote za Watumishi mpaka ngazi ya Mahakimu, Majaji pamoja na Wadau, suala la maboresho limekuwa likitamkwa na watumishi mbalimbali, hii ni kulingana na ukweli kuwa uongozi umekuwa shirikishi katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wake wa miaka mitano 2015/2016-2019/2020,” alieleza Mhe. Jaji Prof. Juma.

Aidha; Mhe. Jaji Mkuu aliongeza kuwa suala la maboresho ya Mahakama linaenda sambamba na utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Maendeleo.

Mhe. Jaji Mkuu alimueleza Mhe.Jaji Mengistu kuwa maboresho ya Mahakama yameenda sambamba na mabadiliko ya Sheria ya Uendeshaji wa huduma za Mahakama ya 2011 ‘Judiciary Administration Act No.4 of 2011’, hali kadhalika kubadili mitazamo ya kitamaduni miongoni mwa watumishi wa Mahakama.

Hata hivyo; Prof. Juma alitaja baadhi ya changamoto ambazo Mahakama inakabiliana nazo ikiwemo baadhi ya sheria kutokuwa rafiki kwa mwananchi wa kawaida, changamoto ya kiteknolojia na nyinginezo.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Mengistu alimpongeza Mhe. Jaji Mkuu kwa hatua ya maboresho iliyopigwa na Mahakama ya Tanzania.

Mhe. Jaji Mkuu huyo alisema kuwa baadhi ya changamoto za Mahakama zipo katika Mahakama zote na si tu kwa upande wa Tanzania hivyo ni kuendelea kuzifanyia kazi.
 Aidha; katika mazungumzo baina ya pande zote mbili, Tanzania na Ethiopia walidokeza juu ya matumizi ya Usuluhishi ‘mediation’ hivyo ni muhimu kuongeza nguvu katika kutilia mkazo suala hili.

Mara baada ya mazungumzo hayo, ujumbe kutoka Ethiopia ukiongozwa na Jaji Mkuu wa nchi hiyo, waliwasilishiwa mada ya safari ya maboresho ya Mahakama iliyowasilishwa na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Zahra Maruma.

Jaji Mkuu huyo yupo nchini kwa siku tatu lengo likiwa ni kujifunza na kubadilishana uzoefu wa  Maboresho mbalimbali yaliyofanywa na Mahakama ya Tanzania. Nchi hiyo ipo katika Mpango wa Maboresho wa Huduma za Mahakama wa miaka mitatu. 
 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyeketi mbele) akiwa katika mazungumzo ya pamoja na mgeni wake Jaji Mkuu wa Ethiopia Mhe. Meaza Ashenafi Mengistu (wa nne kulia), pamoja na Viongozi wa Mahakama ya Tanzania na( wa pili kulia) ni Mtaalam kutoka Bank ya Dunia, Waleed Malik.

Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Meaza Ashenafi Mengistu (kushoto) akisisitiza jambo.
Mhe. Jaji Mkuu akimkabidhi zawadi Mhe. Jaji   Mkuu wa Ethiopia.
 Mhe .Jaji Mengistu wa Ethiopia akimkabidhi zawadi Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania.
 Picha ya pamoja, katikati ni Jaji Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Meaza Ashenafi Mengistu, kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, kulia ni Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, waliosimama ni sehemu ya Majaji,Watendaji Waandamizi wa Mahakama, Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia pamoja na Ethiopia.
Ujumbe kutoka Ethiopia ukiwasilishiwa Mada ya Maboresho ya Mahakama ya Tanzania, mada hiyo imewasilishwa na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Zahra Maruma.
(Picha na Innocent Kansha, Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni