Jumatano, 15 Julai 2020

JAJI MRANGO ATOA USHAURI KUUNDWA KAMATI NDOGO ZA MAADILI.



Na. James Kapele – Katavi
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Mhe. David Mrango ametoa ushauri wa kuundwa kwa kamati ndogo za maadili zitakazotumika kama jukwaa la kushauriana miongoni mwa watumishi hasa katika masuala yanayohusu ukiukwaji wa maadili ya Utumishi wa Umma.

Mhe, Jaji Mrango akizungumza na Watumishi wa Mahakama mkoani Katavi ametoa rai hiyo kwenye  kikao kilichofanya jana katika ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi.

Alisema lengo la kamati hizo, ni kushauriana pindi inapotokea mtumishi kwenda kinyume na maadili na taratibu za kiutumishi badala ya kusubiri kamati za maadili za Mahakimu zinazosimamiwa na wakuu wa Wilaya na Mikoa.

“Kila mtu anao wajibu wa kuwa mwaminifu katika majukumu yake ya kila siku kwa kuwa hakuna anayependa kumuona mtumishi akipata matatizo kazini, nawashauri muone uwezekano wa kuanzisha kamati ndogo ndogo za maadili zitakazowasaidia kushauriana miongoni mwenu hasa pale mnapoona mwenzenu anakwenda kinyume cha maadili na kanuni,” alisema Jaji Mrango.

Aidha amewasisitiza watumishi hao, kuhakikisha wanaitumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ipasavyo na kila mtumishi ahakikishe anakwenda sambamba na mabadiliko hayo.

Jaji huyo  aliwataka Mahakimu kujituma na kuhakikisha wanamaliza mashauri waliyopangiwa kuyasikiliza kwa kuwa kila Hakimu anapimwa kwa ubora wa maamuzi anayoyatoa na idadi ya uwingi wa mashauri anayayomaliza.

Akisisitizia ubora wa maamuzi hayo, kwa Mahakimu amewakumbusha  kujiandaa kikamilifu kusikiliza  mashauri ya uchaguzi utakofanyika mwaka huu.

Alisema mashauri hayo yanahitaji kila mmoja wetu kuwa na utayari  kupitia  sheria mbalimbali za uchaguzi.

Naye Mtendaji wa Mahakama ya Mkoa wa Katavi, Bw. Epaphras Tenganamba amemshukuru, Jaji Mrango kwa ushauri huo na kuahidi kuyafanyia kazi maagizo hayo.

Mhe. Jaji Mrango alifanya kikao hicho, baada ya  kuhitimisha  usikilizwaji wa mashauri ya mauaji mahakamani hapo,yaliyoanza Juni 22  hadi   Julai 13, mwaka huu na kusikiliza mashauri tisa.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Mhe. Janeth Musaroche akifungua kikao cha Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, katika ukumbi wa wazi wa Mahakama hiyo. (Aliyeketi katikati) ni Mhe, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Mhe.David Mrango.

Mtendaji wa Mahakama Bw. Epaphras Tenganamba aliyesimama kulia akitoa ufafanuzi kwenye kikao hicho.

Baadhi ya Watumishi wa Mahakama Mkoani Katavi waliohudhuria kikao hicho.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni