Ijumaa, 10 Julai 2020

JAJI MKUU AWATAKA MAWAKILI WAPYA KUTENDA HAKI

·        Idadi yao yafikia 9,962 nchini

Na Lydia Churi-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo amewakubali na kuwapokea Mawakili wapya 601 na kufanya idadi ya Mawakili wote nchini kufikia 9,962 ambapo pia amewataka kutenda haki wanapotekeleza majukumu yao.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuwakubali na kuwapokea Mawakili hao, Jaji Mkuu amesema Mawakili hawana budi kutenda haki kwa kuwa kabla jambo halijafika mahakamani, hushughulikiwa na mamlaka nyingi ambazo pia, zinatakiwa zitende haki, na zikishindwa ndiyo Mahakama inakuwa na nafasi ya mwisho.

“Katika kazi zenu za kila siku mnagusa haki za wananchi, hivyo basi fanyeni kazi zenu za uwakili kwa haki bila kusubiri mwananchi apeleke shauri mahakamani", alisema Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu amewataka Mawakili wapya kuheshimu maadili, Katiba na Sheria za nchi na kutumikia taaluma waliyoipata kuibadili na kuiboresha Tanzania.

Aidha, amewataka Mawakili hao kutojishirikisha na vitendo vya rushwa ili kutenda haki. Alisema kanuni za Maadili za Mawakili [Advocates (Professional Conduct and Etiquette) Regulations, 2018] zilitungwa mwaka 2018 ili kuwakumbusha Mawakili umuhimu wa kuheshimu maadili yao.

Jaji Mkuu amewataka Mawakili wapya kujiandaa kufanya kazi katika karne ya 21 yenye ushindani mkubwa katika soko la ajira kwani karne hii imetajwa kuwa ni karne iliyoipa kazi ya uwakili msukosuko mkubwa ambao taaluma ya sheria haijawahi kukumbana nao katika karne za 19 na 20.

“Mabadiliko makubwa na ya haraka ya kiuchumi, teknolojia, siasa, kijamii na hata kiutamaduni yamefanyika kwa kasi kubwa zaidi ya uwezo wa Sheria, Wanasheria, na uwezo wa Mawakili kuhimili mabadiliko hayo, ili kuelewa haya ni lazima Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025”, alisema Jaji Mkuu.

Alisema ni wazai kuwa karne ya 21 itamilikiwa na wale wenye teknolojia ya hali ya juu, wenye njia bora za kuzalisha mali na kutoa huduma bora na kwa tija, hivyo wakili atakayeshindwa kutoa huduma bora, au kuchelewesha usikilizwaji wa mashauri, hatamudu ushindani wa karne hii.

Akizungumzia ajira ya Mawakili wa Tanzania, Jaji Mkuu alisema ajira ya Wanasheria nchini ina picha ya ajabu kwani mawakili wamejazana katika miji mikubwa na kukosa ajira, wakati maeneo mengine ya Tanzania yana upungufu mkubwa wa Mawakili.

Alishauri Chama cha Wanasheria wa Tanganyika kufanya utafiti ili kuweza kutathmini Mawakili wanaokubaliwa kila mwaka, wanakwenda kufanya kazi gani, wanafanya kazi za aina gani na wapi. Alisema utafiti huo pia ujikite katika kufahamu kama kuna umuhimu wa kuwa na mitaala mipya ambayo itawawezesha Mawakili kukabiliana na changamoto za karne ya 21.

Jaji Mkuu amewashauri Mawakili wapya kufuatilia mipango ya kitaifa ili waweze  kuibua fursa za kazi nje ya kazi za uwakili. Alisema fursa hizo zinaweza kuibuliwa kutoka kwenye miradi mikubwa ya serikali- SGR, Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, Umeme Vijijini, Gesi, Bwawa la kufua Umeme la Nyerere, na Madini.

Kuhusu Tehama, Jaji Mkuu alisema matumizi hayo hayakwepeki mahakamani huku akitolea mfano wa janga la COVID-19 lililolazimu Mahakama ya Tanzania kutumia TEHAMA kuhakikisha kuwa shughuli za utoaji haki zinaendelea. Hadi kufikia Julai 8 mwaka huu, jumla ya mashauri 3874 yalipokelewa kupitia mitandao ya Mahakama.

Alisema mafanikio makubwa pia yameonekana katika usikilizwaji wa mashauri kwa njia ya video conference. Alisema katika kipindi cha tahadhari ya ugonjwa wa COVID-19 magereza yote yalikuwa katika zuio (Lockdown) lakini mashauri ya jinai na rufani za jinai zilizowahusu wafungwa na mahabusu, zimeendelewa kusikilizwa kwa njia ya Tehama (video conferencing) ambapo hadi kufikia Julai 8, 2020, jumla ya mashauri 8,815 yalisikilizwa katika ngazi ya mahakama mbalimbali kwa njia ya TEHAMA.

Jaji Mkuu alisema mafanikio haya yamewezekana baada ya Mahakama ya Tanzania kununua vifaa vya TEHAMA na kuvisambaza kwenye Magereza 16 mbalimbali nchini ambayo ni Ukonga, Segerea, Mwanza, Tabora, Mtwara, Mbeya, Tanga, Musoma, Arusha, Moshi, Dodoma, Sumbawanga, Shinyanga, Iringa, Bukoba na Songea.
Vifaa hivyo ni pamoja na SMART TV (30), Kamera (30), Kompyuta mpakato (30) na viunganishi vya sauti na picha za video (HDMI) (30). Jumla ya Gharama ya Vifaa hivyo ni Tshs. 230,018,661.40/-

Wakati huo huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Prof. Adelardus Kilangi amewataka Mawakili wapya kutokuwa na haraka ya kupata mafanikio kwani hali hiyo huweza kuwasababisha kujishirikisha na vitendo vya uhalifu, rushwa na ukosefu wa maadili katika kazi yao.

Mwanasheria Mkuu huyo pia amewashauri Mawakili wapya kutotarajia kufanya kazi kwa lengo la kujipatia fedha kila mara bali wakati mwingine wajitoe katika kuwasaidia wananchi wasiokuwa na uwezo ili wapate haki zao.

Naye Rais wa Chama cha wanasheria Tanganyika (TLS) Mhe. Dr. Rugemeleza Nshala amewataka Mawakili wapya kuwa na utamaduni wa kujiendeleza kielimu na kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa kufuata maadili.

Jumla ya Wanasheria 601wamekubaliwa na kupokelewa kuwa Mawakili na Jaji Mkuu wa Tanzania na kufanya idadi ya Mawakili wote nchini kufikia 9,962.
 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo amewakubali na kuwapokea Mawakili wapya 601 na kufanya idadi ya Mawakili wote nchini kufikia 9,962. Pichani Jaji Mkuu akizungumza na Mawakili wapya kupitia Mkutano na Waandishi wa Habari (Press Conference). Amewataka kutenda haki wanapotekeleza majukumu yao.

 Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru (kulia) akiwa kwenye hafla ya kuapishwa Mawakili wapya Mahakama Kuu jijini Dar es salaam. kushoto ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmila Sarwatt.

Viongozi mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye hafla ya kuapishwa Mawakili wapya Mahakama Kuu jijini Dar es salaam. Anayesoma kitabu ni Msajili wa Mahakama ya Rufani Mhe. Kevin Mhina kushoto ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmila Sarwatt.
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmila Sarwatt akizungumza kwenye hafla hiyo.
Viongozi mbalimbali walioalikwa na Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye hafla ya kuapishwa Mawakili wapya. Wa kwanza kulia ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Prof. Adelardus Kilangi akifuatiwa na Rais wa Chama cha wanasheria Tanganyika Mhe. Regemeleza Nshala.

 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (waliokaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani  na Majaji Wafawidhi wa Mahakama kuu (waliosimama) katika hafla ya kuwakubali na kuwapokea Mawakili wapya 601 na kufanya idadi ya Mawakili wote nchini kufikia 9,962. Wa pili kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi na wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Dar es salaam Mhe. Lameck Mlacha.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni