Na Lydia Churi-Mahakama, Shinyanga
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kesho anatarajiwa kuzindua rasmi jengo la
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga katika hafla itakayofanyika kwenye
viwanja vya Mahakama Kuu kuanzia saa 2:00 Asubuhi.
Uzinduzi huo unatarajiwa
kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga, baadhi ya Waheshimiwa Majaji na viongozi wengine wa Mahakama ya
Tanzania, viongozi wa dini, pamoja na wananchi wa mkoa huo.
Mhe. Prof. Juma amewasili
mkoani Shinyanga kwa ajili ya uzinduzi huo ambapo pia alipata nafasi ya
kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi Zainab Telack na kufanya naye
mazungumzo alipomtembelea ofisini kwake.
Jaji Mkuu pia alimkabidhi
Mkuu huyo wa Mkoa kitabu cha Mwongozo wa taratibu za ufunguaji wa mashauri
katika Mahakama ya Rufani.
Akizungumza kwa upande
wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga amesema Serikali mkoani humo imefurahishwa na
hatua ya Mahakama ya kusogeza huduma za Mahakama Kuu karibu zaidi na wananchi
na kwamba itawasaidia wananchi kupata haki kwa wakati.
Jaji Mkuu pia yuko mkoani
humo kwa ajili ya kuanza vikao vya Mahakama ya Rufani vinavyotarajiwa kuanza Jumatatu,
Agosti 10 mwaka huu katika kanda ya Shinyanga.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis akizungumza wakati alipomtembele Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack leo mjini Shinyanga.
Viongozi wa Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga walipoambatana na Jaji Mkuu. Wa pili kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru akifuatiwa na Msajili Mkuu Mhe. Wilbert Chuma kushoto kwake. Wa pili kulia ni Msajili wa Mahakama ya Rufani Mhe. Kevin Mhina na wa kwanza kulia ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmila Sarwatt.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni