Alhamisi, 22 Oktoba 2020

JAJI KIONGOZI AIOMBA TAKUKURU KUELIMISHA WANANCHI KUHUSU MALALAMIKO DHIDI YA MAHAKAMA

 Na Lydia Churi-Mahakama, Mwanza

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa-Takukuru kuwaelimisha wananchi na kuyachunguza malalamiko ya rushwa dhidi ya Mahakama kwani mengine hutokana na wananchi kutofahamu taratibu mbalimbali za Mahakama.

Akizungumza na Mkuu wa wilaya ya Magu Mkoani Mwanza Pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya Magu, Jaji Kiongozi amesema tuhuma za rushwa dhidi ya Mahakama zinaweza kusababishwa na wananchi kutofahamu taratibu za utendaji kazi wa Mhimili huo ikiwemo jinsi ya upatikanaji wa nakala za hukumu, mwenendo wa shauri na namna ya usikilizwaji wa mashauri katika ngazi mbalimbali za Mahakama.

“Mahakama haijishirikishi na vitendo vya rushwa wala haiwalindi wanaojihusisha na vitendo hivyo”, alisema Jaji Kiongozi na kuongeza kuwa vitendo vya rushwa hufanywa na mtumishi mwenyewe asiye na maadili.

Alisema Mahakama haitasita kuwachukulia hatua kali za kinidhamu watumishi wake wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na imekuwa ikifanya hivyo wakati wote.

Kuhusu upatikanaji wa nakala za hukumu, Jaji Kiongozi alisema Mahakama ilianzisha huduma ya usambazaji wa nyaraka zake mbalimbali iitwayo Posta Mlangoni baada ya kuingia mkataba na shirika la Posta Tanzania ambapo hivi sasa nakala za hukumu Pamoja na nyaraka nyingine husambazwa na kufikishwa moja kwa moja kwa wananchi.

Alisema licha ya kuwepo kwa huduma hiyo, bado kuna baadhi ya wananchi ambao hawajaikubali huduma hiyo na kutaka kufika wenyewe mahakamani kuchukua nakala za hukumu hivyo pamoja na Mahakama kuwaelimisha wananchi, ameiomba pia Takukuru kuwaelimisha wananchi wanaopeleka malalamiko ya aina hiyo dhidi ya Mahakama. 

 Wakati huo huo, Mkuu wa wilaya ya Misungwi Bw. Juma Samwel Sweda ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa maboresho ya huduma zake ikiwemo kujenga na kukarabati majengo yake na kuongeza kasi katika usikilizaji wa mashauri. “Hivi sasa majengo yanajengwa na mashauri yanapungua hususan kwenye mahakama ya wilaya ya Misungwi”, alisisitiza.

Mkuu huyo wa wilaya pia aliiomba Mahakama ya Tanzania kuangalia uwezekano wa kujenga jengo la kisasa la Mahakama ya wilaya ya Misungwi kwa kuwa jengo lililopo hivi sasa ni dogo ukilinganisha na mahitaji halisi.  

 Jaji Kiongozi anaendelea na ziara yake ya kikazi kwenye Mkoa wa Geita ambao ni sehemu ya Mahakama Kuu kanda ya Mwanza. Kiongozi huyo anatarajiwa kukagua shughuli za Mahakama katika wilaya za Chato na Bukombe.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akimsikiliza Mtumishi wa Mahakama ya wilaya ya Magu (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza na watumishi wa Mahakama hiyo alipoenda kukagua shughuli za Mahakama. Jaji Kiongozi yuko Mkoani Mwanza kwa ziara ya Ukaguzi. Kushoto ni Jaji Mfawidhi wa kanda hiyo Mhe. Sam Rumanyika na kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Kuu Mhe. Nyigulila Mwaseba akifuatiwa na Mtendaji wa Mahakama Kuu Bibi. Masalu Kisasila. 
Watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Magu wakimsikilza Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi alipozungumza nao. 




Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (wa nne kushoto), Mkuu wa wilaya ya Magu Bw. Salum Kali (wa nne kulia) na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Mwanza Mhe. Sam Rumanyika wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo na baadhi ya Viongozi wa Mahakama ya Tanzania wakati Jaji Kiongozi alipomtembelea Mkuu huyo wa wilaya ofisini kwake.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa wilaya ya Kwimba (wa pili kulia) pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya na Viongozi kutoka Mahakama ya Tanzania.Wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Mwanza Mhe. Sam Rumanyika. 

Watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Kwimbawakimsikilza Jaji Kiongozi alipozungumza nao.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni