Alhamisi, 26 Novemba 2020

MADALALI NA WASAMBAZA NYARAKA WA MAHAKAMA WAPIGWA MSASA

Na Rosena Suka, IJA

Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama ya Tanzania kutoka maeneo mbalimbali ya nchini wanashiriki katika mafunzo ya wiki mbili yanayoendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama  Lushoto ili kuhakikisha kuwa Mahakama inakuwa na Madalali na Wasambaza Nyaraka wenye mbinu bora na nyenzo za kufanyia kazi.

 Akifungua Mafunzo hayo yanayoendelea katika ukumbi wa Chipeta uliopo katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa vitendo, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo amewataka Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kuwa na mijadala huru itakayosaidia kuboresha utendaji kazi wao ili kupunguza malalamiko yanayotokana na wananchi kutokupata huduma bora. 

Mafunzo haya  yamekusanya zaidi ya washiriki 40 kutoka katika sekta mbalimbali za umma na  binafsi. Akielezea lengo kuu la mafunzo  hayo, Mhe. Dkt. Kihwelo amesema endapo Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama watalalamikiwa kwa kutokuwatendea haki wananchi ni dhahiri kuwa Mahakama pia itakuwa imelalamikiwa kwa kuwa watu hao hufanya kazi na Mahakama.

“Kuanzishwa kwa mafunzo ya Madalali na Wasambaza nyaraka za Mahakama ni mojawapo ya sehemu ya maboresho makubwa yanayoendelea katika muhimili wa Mahakama,” alieleza Mkuu huyo wa Chuo.

 Mhe. Kihwelo aliongeza kuwa mafunzo haya yanafanyika ili kuondoa malalamiko mengi yaliyokuwepo kutoka kwa wananchi ambapo kwa kufanya hivi itawawezesha Madalali na Wasambaza Nyaraka kufanya kazi kwa kufuata kanuni zilizopo.

Naye, Mratibu wa mafunzo hayo, Bi. Hamisa Mwenegoha alisema mafunzo hayo ambayo yalianza Novemba 23, 2020 na kutarajiwa kuhitimishwa Desemba 04 mwaka huu yanafanyika kwa mara ya sita ili kuendelea kuwajengea uwezo na kukuza taswira nzuri ya Mahakama ya Tanzania.

Kwa upande mwingine, Bi. Mwenegoha alisema sheria inaweka masharti kwa Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kuhuisha leseni za kufanyia shughuli hizo ili kutimiza matakwa ya sheria inayoongoza shughuli zao. Pamoja na mambo mengine, sheria imeweka vigezo vya mtu mwenye kufanya shughuli hizo ambapo moja ya vigezo hivyo ni kupatiwa mafunzo ya umahiri kutoka chuo katika chuo hicho.

Mafunzo mengine ya aina hiyo yatatolewa katika vipindi tofauti tofauti kwa lengo la kumpa fursa mtu yeyote mwenye vigezo stahiki kupatiwa mafunzo maalum yatakayomwezesha kupata cheti cha umahiri katika udalali na usambazaji nyaraka za Mahakama Pamoja na kuifanya kazi hiyo kwa weledi na kwa kuzingatia kanuni na taratibu za kisheria zilizopo.

 Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Jaji.Dkt. Paul Kihwelo akifungua Mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama yanayofanyika katika ukumbi wa Chipeta uliopo katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa vitendo Dar es Salaam. Kushoto ni Mratibu wa mafunzo hayo, Bi. Hamisa Mwenegoha.

Sehemu ya washiriki wakifuatilia Mafunzo.

Baadhi ya Washiriki katika picha ya pamoja na Viongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni