Alhamisi, 26 Novemba 2020

TUMIENI MAMLAKA NA TARATIBU ZILIZOWEKWA KUHARAKISHA UFUNGAJI WA MASHAURI YA MIRATHI – MSAJILI MKUU

 Na Innocent kansha – Mahakama Muleba.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma amewataka Mahakimu kutumia vizuri mamlaka ya kisheria waliyopewa ili kutatua tatizo la ucheleweshaji wa ufungaji wa mashauri ya Mirathi mahakamani.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na Watumishi wa Mahakama za Wilaya za Biharamulo na Muleba katika ziara yake inayoendelea kwenye Kanda ya Bukoba, Mhe. Chuma alisema uzoefu unaonesha kuwa Mahakimu walio wengi wanapomaliza kusikiliza mashauri ya aina hii kwa hatua ya kuteua wasimamizi wa mirathi hawaweki amri za kuwakumbusha wadaawa kurudi mahakamani kufunga Mirathi yao.

“Someni sheria hiyo vizuri ili muweze kuitumia kwa ukamilifu wake tuweze kupunguza tatizo hili, kuna hadi adhabu zimewekwa kwenye sheria ya mirathi kama msimamizi wa mirathi atashindwa kukamilisha zoezi hilo kwa njia rasmi zilizowekwa na zinazokubalika”, alifafanua.

Mhe. Chuma aliwataka Mahakimu kutumia muda uliobaki hadi kufikia mwisho wa mwezi Disemba 2020 kumaliza mashauri ya mlundikano katika Mahakama zao. Aliongeza kuwa endapo kila Hakimu ataonesha bidii ya kazi na kasi ya usikilizaji wa mashauri yake, hili linawezekana.

Aidha, aliwataka watumishi wa Mahakama kutunza na kuzingatia maadili pindi wanapotimiza majukumu yao na kulinda viapo vyao kama vinavyojieleza. Alisema mahakama haitegemei kusikia mtumishi analalamikiwa kwa kushindwa kutunza maadili ya kazi zake pale anapowajibika.

‘’Malalamiko mahakamani yatamalizika endapo kila mtumishi atawajibika ipasavyo kwa nafasi yake, kila mtumishi atambue kuwa ana nafasi kubwa ya kufanya mageuzi makubwa ya kiutendaji na kuhakikisha Mahakama inakuwa kioo na mfano wa kuigwa kwa jamii tunayoihudumia, alisema.

Alisema, Mahakama inakemea kwa nguvu zote watumishi kujihusisha na vitendo vya rushwa kwani vinapoteza imani na kuchafua taswira nzuri ya Taasisi kwa wananchi. “Yeyote atakayebainika kujihusisha  na vitendo hivi hatutasita  kumchulia hatua kali za kinidhamu ikiwemo kumwondoa kazini.

Kwa upande wa matumizi ya Tehama ndani ya Mahakama, Msajili Mkuu amewataka watumishi kutenga muda wa kutembelea mara kwa mara mitandao ya kijamii ya Mahakama ili waweze kupata habari na taarifa mbalimbali za shughuli zinazofanywa na Mhimili huo ili waweze kujielimisha kwa mambo mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Msajili Mkuu ameahidi kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto zitokanazo na mashauri ya jinai ikiwemo ucheleweshwaji wa upelelezi, wananchi kuipa Mahakama ushirikiano katika utoaji wa ushahidi mahakamani ili mashauri yaweze kukamilika ndani ya muda uliopangwa.

Akizungumza na Mkuu wa wilaya ya Muleba Mhandisi Richard Henry Ruyango alipomtembelea ofisini kwake, Msajili Mkuu alimuomba Mkuu wa wilaya kusaidia kuwaelimisha wananchi ili kupunguza malalamiko yanayotoka na uelewa mdogo wa taratibu mbalimbali za kimahakama.

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo ameihakikishia Mahakama ya Tanzania kuendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali kuhakikisha Mahakama inafikia malengo yake iliyojipangia.

“Kupitia Ofisi yangu nimefarijika kuona Mahakama imepiga hatua kubwa katika mambo mengi kama kuimarisha huduma za utoaji haki nchini hasa uanzishwaji wa Vioski ya kusajili mashauri kwa njia ya mtandao, na Mahakama inayotembea. “kwa hili niupongeze Uongozi wa Mahakama”, aliongeza Mkuu wa Wilaya.

Msajili Mkuu yupo kwenye ziara ya kikazi katika Kanda ya Bukoba kukagua shughuli mbalimbali za kimahakama ili kujionea utendaji kazi wa watumishi katika Mahakama za kanda hiyo.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Biharamulo (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi kukagua shughuli za Mahakama Kanda ya Bukoba, kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba Mhe. Janeth Masesa na kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Biharamulo Mhe. Flora Ndale.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Muleba, kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba Mhe. Janeth Masesa na kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Biharamulo Mhe. Asha Mwidudira.




Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Biharamulo, kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba Mhe. Janeth Masesa na kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Biharamulo Mhe. Flora Ndale.


Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert  Chuma (kulia) akimkabidhi  Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhandisi Richard Henry Ruyango machapisho ya Mahakama wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo.

 

  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni