Jumamosi, 21 Novemba 2020

MAHAKAMA YATAFSIRI KANUNI ZA UENDESHAJI WA KESI ZA UCHAGUZI KWA LUGHA YA KISWAHILI

 Na Innocent Kansha – Mahakama.

Mahakama ya Tanzania imetafsiri Kanuni za utaratibu wa kuendesha mashauri ya uchaguzi katika lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wadaawa wa mashauri hayo kuwa na uelewa wa kanuni hizo katika lugha rahisi pale watakapotaka kuzitumia katika kutafuta haki zao.

Aidha, kanuni hizo zimetafsiriwa kupitia Tangazo la Serikali No. 934 na 935 la tarehe 23 Oktoba mwaka 2020 kwa lengo la kuhakikisha haki inawafikia watu wote na kuondoa vikwazo vya ucheleweshwaji wa upatikanaji wa haki.

Akifungua Kikao cha Kamati ya Kitaifa cha kusukuma mashauri ya jinai kilichofanyika jana Jijini Dar es salaam, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma alisema, Kanuni hizo ni zile za mashauri ya Uchaguzi Mkuu na za uchaguzi wa Serikali za Mitaa zote za Mwaka 2020.

Kwa mujibu wa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhimili huo umefanya  marekebisho na kuandaa kanuni, miongozo ya taratibu mbalimbali kwa lengo la kuharakisha usikilizwaji wa Mashauri yanayohusu uchaguzi.

Alisema Mahakama ina mpango wa kuendelea kutafsiri kanuni nyingine katika lugha ya Kiswahili kadri itavyowezekana. Baadhi ya kanuni hizo ni zile za Mahakama ya Rufani kwa lengo la kurahisisha taratibu katika Mahakama ya Rufani na Kanuni za makosa ya Rushwa na uhujumu Uchumi (The Economic and Organized Crime Control (The Corruption and Economic Crimes Division) (Procedure Rules, 2016.GN No. 267/2016), ili kuweka   utaratibu mzuri wa kushughulikia watuhumiwa wa makosa aina hiyo.  

Mhe. Chuma alizitaja kanuni nyingine zitakazotafsiriwa kuwa ni pamoja na Kanuni za Madalali wa Mahakama na Wasambazaji Nyaraka na Kanuni za kuwasilisha nyaraka za Mahakama kupitia mfumo wa kielectroniki.

 Akizungumzia mashauri, Msajili Mkuu alisema hadi kufikia mwezi Oktoba 2020, jumla ya mashauri 14,715 yalifunguliwa kwa njia ya Mtandao.

“Pamoja na mafanikio hayo nitumie hadhira hii kuwaomba wadau wa haki jinai kuunga mkono juhudi hizi kwa kila mmoja kutekeleza wajibu wake ili kupunguza, kuziba na kutokomeza kabisa mianya ya rushwa kwa kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano “TEHAMA” inayoonyesha ufanisi mkubwa,” alisisitiza Msajili Mkuu.

Mhe.Chuma alisema Mahakama ya Tanzania inakusudia kuondokana na matumizi ya karatasi na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kielekitroniki maarufu kama “E. Filing Digitized and Access to Justice Information Centre”, na kwamba imekiteua kituo cha Mahakama ya Wilaya  Kigamboni kuanzisha usajili wa shauri, usikilizwaji wake mpaka shauri linapomalizika kwa kutumia mfumo wa TEHAMA.

Huduma hii ilizinduliwa tangu Novemba Mosi, 2020 na kuanza kutolewa katika Mahakama ya Wilaya Kigamboni na itapelekwa kwenye Mahakama nyingine kwa kuwa dhamira ya Mahakama ni kuondokana na mfumo wa kutumia karatasi na kuingia kwenye mfumo wa kutumia mifumo ya TEHAMA katika shughuli zote za uendeshaji wa mashauri na shuguli nyingine za Mahakama, aliongeza Msajili Mkuu.

Kwa upande wa mashauri ya mlundikano Mhe. Chuma alieleza kuwa, takwimu zinathibitisha kuwa pamoja na mashauri mengine, yapo Mashauri 39 ya dawa za kulevya katika Mahakama Kuu ambayo ni ya mlundikano.

Alisema taarifa ya mashauri ya kuanzia mwezi Januari hadi mwezi wa Oktoba, 2020 kwa upande wa Mahakama za mikoa kuna jumla ya mashauri mlundikano 3,015 kati ya hayo mashauri 1178 ni ya uhujumu uchumi na Mauaji ambayo Mahakama hizi hazina mamlaka ya kuyasikiliza, aliongeza Mhe Chuma.

Msajili Mkuu alieleza kuwa katika Mahakama za Wilaya kuna mashauri ya mlundikano 3,632 na kati ya mashauri hayo, 1751 ni ya uhujumu uchumi na Mauaji ambayo pia Mahakama hizi hazina mamlaka ya kuyasikiliza.

“Mashauri hayo yapo katika hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutokamilika kwa upelelezi, hivyo hatuna budi kushirikiana ili kuweka mikakati ya kuyaondosha”, alisisitiza Msajili Mkuu.

Alitoa wito kwa wadau wa Mahakama kila moja kuwajibika ili kuepuka lawama ambazo mara nyingi huelekezwa mahakamani. Aliongeza kuwa wadau wana wajibu wa kuimarisha mfumo wa utoaji haki na kutatua changamoto zilizopo ili kuongeza Imani kwa wananchi.

Naye Naibu Kamishna wa jeshi la Polisi Bw. Salehe Ambika akizungumza kwa niaba ya Mkurungenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai alisema Polisi Kitengo cha Usalama barabarani kinakwenda kwa kasi katika kuratibu shughuli zake kwa njia ya TEHAMA, kwani hivi sasa watuhumiwa wote wa makosa ya usalama barabarani wanashunghulikiwa kesi zao kwa njia hiyo kabla hata ya kufikishwa mahakamani.

Kwa upande wa makosa ya jinai yanayopokelewa vituoni, Kamishna huyo alisema  kwa sasa yanashughulikiwa kwa njia ya mfumo wa TEHAMA unaofahamika kama “Case Management System” maana yake ni kusaidia kufuatilia taarifa za jalada husika na kujua hatua zilizochukuliwa ili kutoa taarifa sahihi za kiutendaji na kiukaguzi, aliongeza Bw. Ambike.

Bw. Ambike ametoa rai kwa Taasisi zote zinazojishughulisha na maswala ya mnyororo wa haki jinai kuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa Umma juu ya masuala mbalimbali ya haki zao ili kuondoa taharuki ili wadau wasibaki kutoa lawama kwa kutojua vizuri utendaji wa Taasisi husika, hilo litasaidia kupunguza malalamiko ya kuonewa au kutotendewa haki hasa pale wanapokinzana na sheria za nchi.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma akizungumza  wakati wa uzinduzi mbele ya Wajumbe wa Kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Kusukuma Mashauri ya Jinai (hawapo pichani) kilichofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Mafunzo na Habari cha Mahakama kilichopo Kisutu Jijini Dar es salaam, kushoto ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmillah Sarwatt ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo.

Baadhi ya Wajumbe wa Kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Kusukuma Mashauri ya Jinai wakifuatilia kwa makini wakati Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Usimamizi wa Mahauri Mhe. Desdery Kamugisha alipokuwa akiwasilisha mada ya hali ya usikilzwaji wa mashauri mahakamani.

Baadhi Baadhi ya Wajumbe wa Kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Kusukuma Mashauri ya Jinai wakiwa kwenye kikao hicho wakipiga makofi kuonesha kufurahishwa na hotuba ya ufunguzi iliyotolewa na Mgeni Rasmi Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert  Chuma (aliyesimama mbele).

Baadhi Baadhi ya Wajumbe wa Kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Kusukuma Mashauri ya Jinai wakiwa kwenye kikao hicho.



 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni