Jumamosi, 21 Novemba 2020

RASILIMALI WATU YENYE AFYA MANUFAA KWA TAASISI NA TAIFA: KABUNDUGURU

 Na Mary Gwera, Mahakama

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw.  Mathias Kabunduguru amewataka Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kutunza afya zao, kuzingatia maadili ya kazi pamoja na kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa ustawi wa chombo hicho muhimu kwa Mahakama na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza wakati akifungua rasmi Mafunzo ya Elimu ya kujikinga na Ugonjwa wa UKIMWI na Magonjwa yasiyoambukizwa, Bw. Kabunduguru ambaye pia ni Katibu wa Tume hiyo alisema kuwa Watumishi wa umma ni hazina muhimu kwa Serikali hivyo ni vyema kutunza afya ili kuwa na nguvu kazi kwa maendeleo ya nchi.

“Mkiwa na nguvu na afya bora mtazalisha, mapato yataongezeka na hatimaye mapato hayo yatawezesha kupatikana kwa huduma za jamii,” alieleza Bw. Kabunduguru.

Aliwasisitiza Washiriki wa mafunzo hayo kujiepusha na maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI kwa kuwa ugonjwa huo bado upo hali kadhalika kujikinga na magonjwa yasiyoambukizwa kama Shinikizo la damu (BP), Kisukari na mengineyo kwa kufuata kanuni stahiki za afya.

“Tunapaswa kuendelea kuchukua tahadhari, UKIMWI bado upo, UKIMWI unatisha na vilevile magonjwa yasiyoambukizwa yasipotibiwa yanaathiri nguvu kazi,” alisisitiza.

Kwa upande mwingine, Mtendaji huyo aliwaasa Watumishi hao kuzingatia maadili ya kazi kwa kujiepusha na vitendo vya rushwa.

“Rushwa ni hatari kwa familia na kwa nchi, rushwa ina tabia ya kumpumbaza mtu, inamfanya mtu kuwa mtumwa, hakuna mla rushwa aliyebaki salama, hivyo ni muhimu kufanya kazi na kujipatia kipato cha halali,” alisema Bw. Kabunduguru.

Aliongeza kuwa Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo nyeti kinachotambulika kikatiba hivyo ni muhimu kuunga mkono sera za Mkuu wa nchi ikiwemo mapambano dhidi ya rushwa.

Mafunzo hayo ya siku mbili (2) yameanza leo Novemba 20 na kuhitimishwa Novemba 21 yanafanyika katika Ofisi za Tume hiyo zilizopo jijini Dar es Salaam. Mafunzo haya yamelenga kuwawezesha watumishi hao kupata elimu ya afya, Ujasiriamali, Maadili na Rushwa pamoja na elimu ya Maandalizi ya kustaafu.

Katika siku ya kwanza ya Mafunzo hayo, Washiriki walipata fursa ya kufanyiwa  vipimo vya UKIMWI, Kisukari, Shinikizo la Damu pamoja na Chanjo ya homa ya ini.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw.  Mathias Kabunduguru (katikati) akizungumza na Washiriki (hawapo pichani) wa Mafunzo ya Elimu ya kujikinga na Ugonjwa wa UKIMWI, Magonjwa yasiyoambukizwa, Ujasiriamali, Maadili na Rushwa na maandalizi ya kustaafu. Kulia ni Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bi. Enziel Mtei na kushoto ni Bw. Donasian Kessy, Mkuu wa TAKUKURU wilaya ya Temeke-Dar es Salaam.

Sehemu ya Washiriki ambao ni Watumishi wa Mahakama wakimsikiliza mgeni rasmi alipokuwa akitoa neno la ufunguzi wa Mafunzo hayo.
Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bi. Enziel Mtei akitoa neno kwa washiriki hao.
Picha ya pamoja (katikati) ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ambaye pia ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Mathias Kabunduguru, kushoto ni Naibu Katibu wa Tume hiyo, Bi. Enziel Mtei na waliosimama ni watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaoshiriki katika mafunzo hayo.

(Picha na Lydia Churi, Mahakama)
Hakuna maoni:

Chapisha Maoni