Jumatatu, 16 Novemba 2020

MAHAKIMU NA WATENDAJI WA MAHAKAMA KANDA YA KIGOMA WAPATIWA MAFUNZO YA UONGOZI

 Na Festo Sanga, Mahakama-Kigoma

Jumla ya Mahakimu na Maafisa 40 wa kada mbalimbali wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma wamepatiwa mafunzo ya Uongozi ili kuwajengea uwezo watumishi hao kuweza kuimarisha maadili na umalizaji wa mashauri haraka kwa viwango ambavyo Kanda imejiwekea.

Akifungua rasmi mafunzo hayo hivi karibuni yaliyofanyika Wilayani Kibondo-Kigoma, Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Jaji  Ilvin Mugeta alisema lengo ni kuhakikisha kwamba watumishi wa ngazi ya Maafisa wa Mahakama na wale wa utawala (judicial and non- judicial officers) wanapata mafunzo katika maeneo ya Uongozi, Maadili, ukaguzi, usimamizi wa mashauri na usimamizi wa mali za Umma.

 “Natambua baadhi yenu hususani  Mahakimu wa Mahakama za mwanzo lakini pia maafisa mbalimbali ni waajiriwa wa siku za karibuni, ndio maana tumeendaa mafunzo haya ili kuwajengea uwezo kiuongozi ili muweze kutekeleza majukumu yenu kwa weledi na ufanisi na kujenga imani kwa walio chini yenu’ alisema Jaji Mugeta.

Jaji Mugeta aliongeza kuwa mafunzo hayo yanatolewa kwa Watumishi hao yamelenga pia kuwawezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiutumishi na hatimaye watumishi wanapofika kwa viongozi hao wawe na imani ya  kupata suluhu ya matatizo yao.

“Hakuna kitu kibaya kama kuongoza watumishi wasio na furaha, hivyo ni wajibu wa kiongozi kurejesha furaha ya watumishi kwa kuwasikiliza na kuwaongoza vyema,” alisisitiza Jaji huyo Mfawidhi.

Hata hivyo, Jaji Mugeta alieleza kuwa  Mahakama kanda ya Kigoma inayo maeneo mahsusi  katika utekelezaji wa kila siku wa mipango na shughuli ambayo usimamizi wake ni kipaumbele cha kwanza, huku akiyataja maeneo hayo kuwa ni kuimarisha maadili na umalizaji wa mashauri haraka kwa viwango ambavyo Kanda imejiwekea.

Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Moses Mashaka alisema  katika utekelezaji wa mpango wa Mafunzo ya ndani kwa mwaka 2019/2020 na mpango wa mafunzo wa mwaka 2020/2021 jumla ya watumishi 83 wa kada mbalimbali walipewa mafunzo.

Bw. Mashaka alisema kwa mwaka wa fedha 2019/2020  Kanda hiyo ilitoa mafunzo juu  ya taratibu za kufungua mashauri, maadili ya utumishi wa Umma, usimamizi na ujazaji sahihi wa rejesta za mashauri, mpango mkakati wa Mahakama  na mfumo wa kuratibu mashauri(JSDS II), Miongozo mbalimbali kuhusu usimamizi wa watumishi, usimamizi wa mashauri, na usimamizi wa Magari.

“Mafunzo hayo yameleta mabadiliko yenye tija katika utendaji kazi kwa mtumishi mmoja mmoja na kanda kwa ujumla” alisema Bw. Mashaka.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Jaji Ilvin Mugeta akifungua mafunzo ya Uongozi kwa Mahakimu na Maafisa wa kada mbalimbali yaliyofanyika wilayani Kibondo hivi karibuni.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Moses Mashaka akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango wa mafunzo ya ndani kwa washiriki wa mafunzo.

Mhe. Jaji Mfawidhi akiwasilisha mada ya Uongozi kwa washiriki wa mafunzo.

Washiriki wa Mafunzo wakifuatilia mada ya Uongozi iliyotolewa.











 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni