Alhamisi, 5 Novemba 2020

JAJI MKUU WA TANZANIA AMUAPISHA RAIS DKT JOHN MAGUFULI

Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemuapisha rasmi Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliyeshinda kiti cha Urais baada ya kutangazwa mshindi kufuatia kukamilika kwa uchaguzi mkuu wa Taifa uliofanyika Oktoba 28, 2020.

Sambasamba na hilo katika hafla hiyo ya Uapisho wa Mhe. Rais wa awamu ya tano (5) anayetumikia nafasi hiyo kwa muhula wa pili, Mhe. Jaji Mkuu alimuapisha pia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma mapema Novemba 05, mwaka huu.

Akizungumza na wananchi mara baada ya kuapishwa rasmi, Rais Magufuli aliwashukuru Watanzania kwa kumpatia kura nyingi za ushindi na kuwaahidi kushirikiana nao katika kuleta maendeleo ya Taifa.

“Uchaguzi umekwisha, sasa tuchape kazi, napenda kuwahakikishia kama ilivyokuwa kwenye miaka mitano iliyopita na kwa miaka mitano ijayo nitaendeleza na kutimiza yale yote niliyoahidi,” alisema Rais Dkt. Magufuli.

Mhe. Rais aliongeza kuwa ataendelea kuimarisha ulinzi wa rasilimali zilizopo nchini ili ziendelee kutoa ajira, kuongeza fursa za uwekezaji na kutatua kero mbalimbali.

Katika hatua nyingine Mhe. Rais amesema Serikali itaendelea na mapambano dhidi ya rushwa na ubadhilifu wa mali za umma, kukamilisha miradi mikubwa iliyoanza na kutekeleza mingine mipya.

Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Museveni aliyehudhuria katika hafla hiyo amempongeza Mhe. Rais kwa ushindi aliopata na kuwapongeza Watanzania kwa uchaguzi wa amani na wa kidemokrasia na kuwataka kuendeleza uzalendo aliouacha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Hafla hiyo muhimu kwa Taifa ilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akila kiapo mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Juma. Tukio hilo la uapisho limefanyika leo Novemba 05, 2020 katika Uwanja wa Jamhuri uliopo jijini Dodoma.
Rais Magufuli akitia saini hati ya kiapo mara baada ya kuapishwa rasmi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika muhula wa pili wa awamu ya tano. 
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Juma (kulia) akitia saini katika hati ya kiapo cha Mhe. Rais mara baada ya kumuapisha rasmi mapema Novemba 05 mwaka huu.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Juma akimkabidhi Mhe. Rais Magufuli Katiba ya Tanzania.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Juma akimuapisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan. 
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Juma akimkabidhi Makamu wa Rais Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiongozana na Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe. Job Ndugai, Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi John Kijazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Adelardus Kilangi, baadhi ya  Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu pamoja na Viongozi wa Dini wakielekea katika nafasi zao kabla ya kumuapisha rasmi Mhe. Rais Magufuli.
Baadhi ya Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Tanzania pamoja na baadhi ya Viongozi na wageni wengine waalikwa wakiwa katika hafla hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi mara baada ya kuapishwa rasmi.
Wageni mbalimbali waliohudhuria katika hafla ya uapisho wakimsikiliza Mhe. Rais (hayupo pichani)
Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni akitoa hotuba yake katika hafla hiyo.
Sehemu ya wananchi waliohudhuria katika hafla ya uapisho.
Baadhi ya makundi ya Jeshi la Ulinzi na Usalama wakipita mbele ya Mhe. Rais.
Mhe. Jaji Prof. Juma akiondoka eneo la tukio baada ya kuhitimishwa kwa ratiba ya hafla ya uapisho wa Mhe. Rais.
Baadhi ya Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu wakiondoka eneo la tukio . Wa pili kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi.
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Dodoma, Mhe. Mustapher Siyani (wa tatu kushoto) pamoja na baadhi ya Maafisa wengine wa Mahakama waliohudhuria katika hafla hiyo wakiondoka eneo la tukio.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru akifurahia jambo, Bw. Kabunduguru ni miongoni mwa wageni waalikwa waliohudhuria katika hafla hiyo muhimu kwa Taifa.
Baadhi ya Wasanii wa muziki wa kizazi kipya waliotumbuiza katika hafla ya uapisho.


 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni