Alhamisi, 5 Novemba 2020

MAJAJI MAHAKAMA YA RUFANI WAKAGUA MIRADI YA UJENZI JIJINI DODOMA.

 Na Stanslaus Makendi, Mahakama Kuu Dodoma

Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania wametembelea na kukagua miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama iliyoko jijini Dodoma.  

Majaji hao wakiambatana na Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman pamoja na Viongozi wengine wa Mahakama ya Tanzania walipata fursa ya kukagua miradi ya ujenzi inayoendelea kutekelezwa mkoani humo ikiwemo ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, jengo la Mahakama Jumuishi “Intergrated Justice Centre”, pamoja na majengo ya Mahakama za Wilaya za Chemba na Kondoa ambayo baadhi imekamilika na tayari huduma za Mahakama zinatolewa katika jengo hilo.

Jengo la Mahakama ya wilaya ya Kondoa lilikamilika na kuzinduliwa rasmi Februari 4 mwaka huu na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai na tayari linatumika kutoa huduma kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Viongozi hao, licha ya kukagua miradi ya ujenzi pia wametoa wito kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi mingine ya Mahakama nchini kuzingatia maelekezo ya kitaalamu, viwango vya ubora na kuhakikisha miradi hiyo inaendana na thamani ya fedha zilizoelekezwa katika miradi husika kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanachagiza maendeleo ya Taifa letu.

Sambamba na hilo, Viongozi hao wamepongeza Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa Mipango iliyowekwa inayolenga kuboresha miundombinu iliyopo na ujenzi wa majengo ya kisasa katika maeneo mbalimbali nchini ili kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi.

Jaji Mkuu Tanzania Mstaafu Mhe. Mohamed Chande Othman (Wa tisa kushoto) akiwa pamoja na Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania pamoja na Viongozi wengine wa Mahakama na Wakandarasi wakiwa katika picha ya pamoja baada ya Majaji hao kutembelea na kukagua Mradi wa Ujenzi wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kinachojengwa jijini Dodoma. Sambamba na Mradi huo, Majaji hao pia walikagua miradi ya ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama pamoja na Mahakama za wilaya za Chemba na Kondoa. Jengo la Mahakama ya wilaya ya Kondoa limekamilka na linatumika.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Dodoma Mhe. Mustapher Siyani (kushoto) akionesha jambo wakati Jaji Mkuu Tanzania Mstaafu Mhe. Mohamed Chande Othman, Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania pamoja na Viongozi wengine wa Mahakama wqlipokagua ujenzi wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kinachojengwa jijini Dodoma.
Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Majengo cha Mahakama ya Tanzania, Mhandisi Khamadu Kitunzi akielezea jambo kwa Waheshimiwa Majaji. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni