Jumapili, 25 Oktoba 2020

MAHAKIMU MOSHI WAPIGWA MSASA UENDESHAJI MASHAURI YA UCHAGUZI

Na Paul Mushi, Mahakama Kuu- Moshi

Mahakama Kuu Kanda ya Moshi imefanya Mafunzo maalum kwa jumla ya Mahakimu 21 wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Wilaya sita juu ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi.

Lengo la Mafunzo hayo ni kuwawezesha Mahakimu wote wa wilaya  kanda ya Moshi juu ya kanuni, sheria na Maadili ya kushughulikia Mashauri ya Uchaguzi katika Kipindi hichi ambapo Tanzania inafanya uchaguzi Mkuu 2020.

Akifungua Mafunzo hayo hivi karibuni, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi-Mhe. Jaji  Beatrice Mutungi amewasihi washiriki kusikiliza mashauri kwa uwazi, uhuru ili kuonyesha uhuru wa muhimili wa Mahakama hali itakayoongeza imani ya wananchi kwa Mahakama.

“Ninawasihi kufanya maamuzi kwa kuzingatia kanuni na sheria za nchi na kuepuka vishawishi vya rushwa pamoja na kusimamia maadili ya uhakimu ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati,” alisema Mhe. Jaji Mutungi.

Naye Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Mhe. Bernazitha Maziku aliwataka washiriki hao kusikiliza kwa makini mada zitakazofundishwa ili ziwasaidie kuepuka migogoro itakayoweza kusababishwa  kwa kukiukwa kwa taratibu za uendeshaji mashauri ya uchaguzi.

Mpaka sasa Mahakama kwa kushirikiana na Chuo tayari imeshafanya mafunzo ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Maafisa mbalimbali wa Mahakama ikiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Zanzibar, Naibu Wasajili, Mahakimu Wakazi Wafawidhi lengo likiwa ni kuwawezesha kuyashughulikia kwa ustadi zaidi na kwa wakati.

Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Beatrice Mutungi akitoa nasaha zake kwa washiriki (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi rasmi wa Mafunzo ya siku moja ya namna bora ya kuendesha mashauri ya uchaguzi yaliyofanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi.

Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Beatrice Mutungi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mafunzo, kushoto ni Naibu Msajili, Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Omary Kingwele na kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Mhe. Benazitha Maziku.

Picha ya pamoja  na washiriki.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni