Jumamosi, 24 Oktoba 2020

SHIRIKIANENI KWA MASLAHI YA TAASISI ; JAJI MSTAAFU WAMBURA

  Na Innocent Kansha - Mahakama

Jaji Mfawidhi Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Sophia Wambura amewataka watumishi wa Mahakama ya Tanzania kufanya kazi kwa upendo, ushirikiano na uadilifu ili kuleta tija kwa Taasisi.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kumuaga baada ya kustaafu rasmi iliyofanyika katika Mahakama hiyo Oktoba 23 mwaka huu, Mhe. Jaji Mstaafu Wambura alisema kufanya kazi kama kama timu kutawezesha malengo yao na ya Taasisi kutimia.

“Ili mkono ukamilike ni lazima kila kidole kiwepo, ndipo mkono unaweza kufanya kazi kwa ukamilifu na ufanisi ndivyo basi tunatakiwa kama watumishi kufanya kazi kwa ushirikiano na kufikia mafanikio kwa maslahi mapana zaidi”, alisema Jaji .

Jaji Wambura aliongeza kwa kuzungumzia nafasi ya kiongozi katika kufanikisha hilo huku akisema kuwa. “Kiongozi bora ni mtu anayetumia muda wake kuonyesha dira ya kuwafikisha Watu kwenye hatima ya mafanikio ya mtu moja moja na hata Taasisi anayoiongoza kwa kusimamia uwazi, uwajibikaji na mahusiano mazuri pahala pa kazi.”

Aidha, Mhe. Jaji Mstaafu Wambura aliwaeleza watumishi hao kuwa katika kutimiza majukumu yao ni lazima waige kundi la ndege warukao angani bila kuongozwa na mtu bali hutumia karama walionayo na kufikia hatima yao kwa juhudi na ushirikiano wao. “Kila Mtumishi aliyepo hapa yupo kwa sababu na si bure hivyo anatakiwa kuonyesha karama ulizonazo kwa kushirikiana na wengine ili malengo yenu kama Watumishi na Taasisi yenu yatimie.”

Jaji Wambura aliwakumbusha watumishi kuzingatia maadili ya kazi ili kutoharibu taswira ya Taasisi na kupoteza imani ya Umma unaouhudumia, Viongozi wanapaswa kutoa maelekezo ya mara kwa mara kuwakumbusha watumishi masuala muhimu ya kinidhamu.

Kwa upande mwingine, Mhe. Jaji Wambura aliwataka Watumishi kutoridhika na nafasi zao kazini aliwaasa kutafuta njia mbalimbali za kuongeza na kujiendeleza kielimu ili kutafuta fursa zaidi na kupanua wigo wa ujuzi na umahiri ili kutimiza majuku yao kwa ufasaha na weledi mkubwa zaidi.

Awali akitoa neno la utangulizi kwa niaba ya watumishi, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Devisheni ya Kazi, Mhe. Imani Daud Aboud alisema kuwa wangependa kuendelea kuwa na Jaji Mstaafu Wambura kwa ari ya utendaji kazi wake ila kwa mujibu wa sheria hana budi kupumzika katika utumishi.

Mhe. Jaji Aboud aliongeza kuwa Jaji Mstaafu Wambura ni mtu aliyekuwa na upendo wa hali ya juu kazini, ushirikiano, kusimamia nidhamu za watumishi, alikuwa mtiifu na mwadilifu, aliongeza kuwa alikuwa mpenda haki asiye na makuu na lionyesha unyenyekevu siku zote na kiongozi hodari.

Naye, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Zainab Muruke alimuelezea Jaji Mstaafu Sophia Wambura kama mfanyakazi hodari mwenye msimamo imara wa kusimamia mambo anayoyaamini katika kazi, kuwatia hari watumishi hasa wa jinsia ya kike na kuwaasa watumishi kutobweteka kujiendeleza kitaaluma ili kuboresha ufanisi kazini

Jaji Mstaafu Sophia Wambura amestaafu baada ya kuhutumikia Muhimili wa Mahakama kwa takribani miaka 35 katika nyadhifa mbalimbali.

Jaji Mfawidhi Msataafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi Mhe. Sophia Wambura (aliyesimama) akitoa nasaha zake kwa watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya kazi wakati wa hafla ya kumuaga iliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama hiyo Jijini Dar es Salaam, katikati ni Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe Imani Daud Aboud na kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Zainab Muruke.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Imani  Aboud (aliyesimama) akitoa neno la utangulizi wakati wa Hafla ya kumuaga Jaji Mfawidhi Msataafu, Mhe. Sophia Wambura (wa pili kulia),  kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Zainab Muruke na wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi- Bi. Hellen Mkumbwa.

Jaji Mfawidhi Mstaafu, Mhe. Sophia Wambura (wa pili kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi (wa pili kushoto) ni Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania- Divisheni ya Kazi Mhe, Imani  Aboud, (wa kwanza kulia) ni Jaji wa Divisheni hiyo, Mhe. Zainab Muruke na (wa kwanza kushoto) ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania- Divisheni ya Kazi Mhe. Angaza Mwipopo.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Zainab Muruke (aliyesimama) akitoa neno la shukrani mbele ya Jaji Mfawidhi Msataafu, Mhe. Sophia Wambura wakati wa hafla ya kumuaga iliyofanyika katika Ukumbi wa Mahakamani hapo, kushoto  ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi Mhe. Angaza Mwipopo.

Mtumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi Bi. Jane Lwiza kwa niaba ya watumishi wenzake akitoa neno la shukrani wakati wa hafla ya kumuaga Jaji Mstaafu, Mhe. Sophia Wambura.

Baadhi ya watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi wakifanya Igizo fupi la kupanga mbinu za kukabiriana na adui kama ishara ya kuonyesha maana ya uongozi mahala pa kazi wakati wa hafla ya kumuaga Jaji Mfawidhi Msataafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi Mhe. Sophia


Jaji Mfawidhi Msataafu Mhe. Sophia Wambura akikata Keki iliyoandaliwa na watumishi wa Mahakama Divisheni ya Kazi ikiwa ni ishara ya kumpongeza baada ya kustaafu utumishi rasmi.

 


Maoni 1 :

  1. Hongera sana Mhe. Jaji Sophia Wambura Mama mwenye busara na maadili mema kwa wote. Katika uongozi wako nikikumbuka ukiwa Msajili Mahakama kuu ya Tanzania Mbeya. Ulionyesha upendo kwa watumishi bila ubaguzi. Na uliendelea hata ulipokuwa Mhe. Jaji kwa kujituma na kuwahamasisha watumishi ngazi zote,wahe. Mahakimu na Wahe. majaji na kuenzi maadili ya kazi na imani katika dini zote. Ninakupongeza kwa utumishi uliotukuka Mhe. Sophia Wambura. Mungu akulinde na akutunze daima. Akujalie afya njema na kuufikia uzee mwema na mkamilifu. Ninakupenda Mama. ❤

    JibuFuta