Jumamosi, 28 Novemba 2020

TUBORESHE MASLAHI YA WATUMISHI KUONGEZA NGUVU KAZI; MSAJILI MKUU

Na Innocent Kansha, Mahakama Kuu- Bukoba

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amewaagiza Watendaji wa Mahakama kuwapa motisha watumishi wa Mhimili huo hasa wale wanaohudumu nafasi zaidi ya moja ili kuongeza tija kazini.

Akizungumza Novemba 27, 2020 katika mkutano na watumishi wa Mahakama Kanda ya Bukoba uliofanyika katika Ukumbi wa Mahakama Kuu ya Kanda hiyo, Mhe. Chuma alisema tatizo la upungufu wa watumishi lipo kwa nchi nzima na linashughulikiwa kwa kadiri vibali vya ajira vinapotolewa.

 “Unakuta kwenye kituo kuna Mtumishi kaajiriwa kada yake ni Mlinzi lakini anafanya kazi ya mtunza kumbukumbu, anashughulikia mfumo wa kusajili na kuhuisha mashauri (JSDS II) na wakati huo huo yeye anatumika kama dereva kwenye kituo chake cha kazi, sasa mtumishi kama huyu anatakiwa apewe motisha ya kazi”, alisema Msajili Mkuu.

Mhe. Chuma alisema, shughuli za Mahakama haziwezi kusimama kutokana na upungufu wa watumishi hivyo hakuna budi kutumia vyema rasilimali watu iliyopo pamoja na kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi, kuwajali watumishi wenye uwezo wa kufanya jukumu zaidi ya moja kwa kuwapa motisha ili kazi za Taasisi zisonge mbele.

Kwa upande mwingine, Msajili Mkuu amewaagiza Maafisa Utumishi na Tawala kutenga muda wa kutoa elimu kwa Watumishi kuhusu masuala yanayowatatiza ili kuondoa sintofahamu na kupata taarifa sahihi, mfano: mambo yanayohusu michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, mapunjo na nyongeza za mishahara, upandishwaji wa vyeo (madaraja) ikiwemo miongozo na miundo ya kiutumishi kuwongezea uelewa zaidi watumishi.

Kwa upande wa mashauri, Msajili Mkuu amewakumbusha Mahakimu kuzingatia waraka alioutoa wa kumaliza mashauri mlundikano ifikapo Desemba 2020 kwa yale mashauri walio na mamlaka nayo.

Mhe. Chuma aliwasisitiza pia watumishi hao kuzingatia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kutumia mifumo ya TEHAMA iliyopo Mahakama kama Mfumo wa kuratibu na kusajili Mashauri (JSDS2), matumizi ya vioski vya kusajilia kesi kwa njia ya mtandao “E – Filing” na mingineyo.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martine Chuma Akizungumza na watumishi (hawapo pichani) wa Mahakama Kuu, Mkoa, Wilaya na Mahakama ya Mwanzo Bukoba Mjini, kwenye mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za Mahakama. Kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba, Mhe. Janeth Massesa na kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bukoba, Mhe. John Mpitanjia Mnamba.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi- Bukoba, Mhe. Janeth Massesa akitoa neno wakati wa kufungua kikao cha Watumishi na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martine Chuma (aliyeshika jalada) akikagua majalada na rejista za kusajili mashauri alipofika kufanya ukaguzi Mahakama ya Mwanzo Bukoba Mjini, kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba, Mhe. Janeth Massesa (wa pili kulia) ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bukoba, Mhe. John Mpitanjia Mnamba na (wa pili kushoto) ni Katibu wa Msajili Mkuu, Mhe. Jovin Bishanga.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martine Chuma (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Mahakama ya Kuu, Mkoa na Wilaya Bukoba Mjini, (kulia) ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba, Mhe. Janeth Massesa na (kushoto) ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bukoba, Mhe. John Mpitanjia Mnamba.

(Picha na Innocent Kansha, Mahakama)

 

 


 


 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni