Jumanne, 1 Desemba 2020

MAHAKIMU WATAKIWA KUELIMISHA JAMII MADHARA YATOKANAYO NA RUSHWA

 Na Tawan Salum-Mahakama, Lushoto

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewataka Mahakimu kujiepusha na vitendo vya rushwa na badala yake wawe mstari wa mbele katika kuielimisha jamii madhara yanayotokana na vitendo hivyo.

Jaji Kiongozi ameyasema hayo wakati akifungua rasmi Mafunzo kwa Mahakimu wapya walioapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma Novemba 27 mwaka huu, yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa lengo la kuwajengea uwezo Mahakimu hao.

 “Rushwa ni adui wa haki, ikataeni na kuiogopa kama ukoma na mkawe mabalozi wazuri wa kutoa elimu juu ya madhara ya rushwa kwenye jamii zetu kwa kuwa nina imani ndiyo mmeapishwa hivi karibuni mnajua kuwa rushwa ni mbaya”, alisema Jaji Kiongozi.

Alisema Mahakama ya Tanzania iko katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na ukosefu wa maadili kwa watumishi wake kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ambavyo amekuwa akiifananisha na ugonjwa wa Saratani na kupambana nayo kwa nguvu zote.

Aliwataka Mahakimu hao kuichukia rushwa kabla haijajipenyeza na kupata makao ili kulinda heshima yao, ya Mahakama na hata Taifa kwa ujumla. “Ninaamini hata ninyi hampendi kukosa haki zenu au ndugu na jamaa zenu kutokana na vitendo vya rushwa”, alisema Jaji Kiongozi.

Alisema hategemei Mahakimu kufanya Makosa hasa katika maeneo ambayo Sheria iko wazi kwa kuwa Hakimu anatakiwa kujitayarisha kwa kuwa na uelewa wa Sheria na taratibu zote za shauri lililo mbele yake kabla ya kuingia mahakamani, hivyo Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo ili waweze kuwa na utayari huo.

Akizungumzia mafunzo hayo, Dkt. Feleshi aliwaambia Mahakimu hao kuwa kupatiwa mafunzo kama hayo ni fursa muhimu na historia kwa kuwa ni mwanzo mwema kwa Maadhimisho ya miaka 100 ya Mahakama Kuu ya Tanzania yatakayozinduliwa hivi karibuni na Jaji Mkuu. Aliongeza kuwa uzinduzi huo utatanguliwa na Maadhimisho ya Miaka ishirini (20) ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Katika hatua nyingine Jaji Kiongozi ameipongeza Tume ya Utumishi wa Mahakama na Jaji Mkuu kwa kuweka mfumo madhubuti wa kuhakikishia Tume inaajiri Mahakimu mahiri na kwa ushindani wa haki. Alisema Mahakimu 39 waliapishwa Ijumaa ya Novemba 27, 2020.

Naye Msajili wa Mahakama ya Rufani Mhe. Kevin Mhina alimshukuru Jaji Kiongozi kwa kutoa muda wake na kukubali kufungua mafunzo hayo kwa Mahakimu waliapishwa hivi katibuni. Aliwataka Mahakimu hao kuzingatia maadili katika utekelezaji wa majukumu yao na kuzingatia mambo yote mengine muhimu waliyoaswa na Jaji Kiongozi.  

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akifungua Mafunzo kwa Mahakimu 39 waliopishwa hivi karibuni. Mafunzo hayo yamefanyika katika chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwa lengo la kuwajengea uwezo. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na wa pili kulia ni Msajili wa Mahakama ya Rufani Mhe. Kevin Mhina. Kushoto ni Msajili wa Mahakama Kuu Mhe. Sharmilla Sarwatt na wa kulia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Edward Nkembo. 

Baadhi ya Mahakimu wakifuatilia jambo wakati wa Mafunzo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mahakimu mara baada ya kufungua mafunzo yao jana mjini Lushoto.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto mara baada ya kufungua kwa Mafunzo kwa Mahakimu 39 waliopishwa hivi karibuni. 
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mahakimu mara baada ya kufungua rasmi mafunzo yao.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni