Na Mary Gwera, Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma mapema leo Desemba 15, 2020 amewaapisha Mahakimu Wakazi wawili wa Mahakama za Mwanzo na kufanya idadi ya jumla ya Mahakimu wapya 41 waliopishwa leo na Novemba 27 mwaka huu.
Akizungumza mara baada ya kuwaapisha Ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mhe Jaji Mkuu amewaasa Mahakimu hao kufanya kazi kwa haraka ili kuendana na kasi ya karne ya 21.
“Ninyi ni Mahakimu wa karne ya 21, hivyo ni muhimu kuendana na kasi ya karne hii kwa manufaa ya Mahakama na Taifa kwa ujumla,” alisema Mhe. Jaji Prof. Juma.
Aidha, Mhe. Jaji Mkuu aliwasisitiza Mahakimu hao kufanya kazi kwa kufuata viapo vyao kwa kutoa haki kwa wananchi bila upendeleo wa aina yoyote.
“Ninyi ndio sura ya Mahakama, hivyo ni vyema mkafanya kazi kwa kufuata maadili yaliyopo ili kutochafua taswira ya Mahakama,” alisisitiza Mhe. Jaji Mkuu.
Upatikanaji wa idadi hiyo ya Mahakimu utasaidia kuongeza nguvu kazi Mahakamani na hatimaye huduma ya utoaji haki kutolewa kwa wakati.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akimuapisha Bi. Zainab Mtoro kuwa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo.
Mhe. Jaji Mkuu akisaini hati ya kiapo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akimuapisha Bi. Agnes Mziba kuwa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo.
Mhe. Jaji Mkuu akitia saini katika hati ya kiapo.
Makabidhiano hati ya kiapo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akimkabidhi kompyuta mpakato Bi. Agnes Mziba mara baada ya kumuapisha.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akimkabidhi kitendea kazi kompyuta mpakato ‘laptop’ Bi. Zainab Mtoro.
Viongozi na baadhi ya Maafisa wa Mahakama waliohudhuria katika hafla fupi ya uapisho wa Mahakimu hao. Kulia ni Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, katikati ni Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Joaquinne De Mello na kushoto ni Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru.
Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akiongoza hafla hiyo ya uapisho.
Mhe. Jaji Mkuu akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu Wakazi wapya aliowaapisha, kushoto ni Mhe. Zainab Mtoro na kulia ni Mhe. Agnes Mziba.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni