Na Lydia Churi-Mahakama
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt.
Eliezer Feleshi amesema mashauri ya madai ni lazima yatazamwe kwa mapana na
yakamilike kwa haraka ili wananchi watumie rasilimali na muda mwingi katika
uzalishaji mali na kutoa huduma badala ya kupoteza muda mwingi kutafuta utatuzi
wa mashauri hayo.
Akifungua kikao cha kitaifa cha kusukuma mashauri ya
madai jijini Dar es salaam, Jaji Kiongozi alisema kuchelewa kumalizika kwa
mashauri hayo kunaweza kukwamisha au kuchelewesha azma ya nchi ya kukuza uchumi
na kufifisha mapambano dhidi ya umaskini.
Alisema ingawa Mahakama ndicho chombo cha mwisho
katika utoaji haki, lakini haiwezi kutekeleza
jukumu hilo pasipo mchango wa wadau wake
ambao baadhi yake ni Polisi, Magereza, Takukuru, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, Mawakili na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa
Serikali.
Jaji Kiongozi alisema pamoja na maboresho makubwa
yaliyofanyika ndani ya Mahakama endapo wadau hawatashirikishwa hayatafika mbali
hivyo aliwataka wajumbe wa kamati ya kitaifa ya kusukuma mashauri kuwa daraja
la kukutanisha wadau wote kutatua changamoto na kuimarisha umoja.
Akizungumzia ucheleweshwaji wa mashauri ya madai, Jaji
Kiongozi alisema ucheleweshwji huo hausababishwi na mapungufu ya sheria bali ni
mapungufu ya wasimamizi katika utoaji haki na wadau pamoja na maahiriho marefu na
mapingamizi yasiyokuwa na sababu za msingi.
Kuhusu Tehama alisema matumizi bora ya Teknolojia hiyo
ndani ya Mahakama ni nyenzo muhimu katika kuwezesha utoaji haki kwa wakati na
kusogeza huduma karibu ziadi na wananchi.
“Mahakama inapoendelea kutumia Tehama katika kutoa
huduma za ufunguaji, usikilizwaji na menejimenti ya mashauri, wadau katika
sekta ya utoaji haki lazima tawe pamoja na kwa kasi moja”, alisisitiza.
Jaji Kiongozi alisema mwelekeo wa Mahakama kwa sasa
katika matumizi ya Tehama ni kuwa Mahakama isiyotumia karatasi (Paperless Cout)
na tayari imeanza na Mahakama ya wilaya ya Kigamboni kama eneo la majaribio
(Pilot Court) na hivi karibuni Mahakama za wilaya zote zenye majengo mapya na ya
kisasa zitafikiwa.
Mirathi
Katika hatua nyingine, Jaji Kiongozi amesema mashauri
ya mirathi huchukua muda mrefu kumalizika kutokana na ndugu na jamaa wa
marehemu kushindwa kuelewana katika viako vya familia na ukoo na kuleta tofauti
na uadui wao mahakamani kupitia mashauri hayo.
“Sheria na taratibu zinazoongoza mashauri ya mirathi hazina
tatizo, tatizo linakuja pale ndugu na jamaa wa marehemu wanaposhindwa kuelewana
kwenye vikao vyao vya familia na ukoo”, alisema Jaji Feleshi.
Alisema eneo la mirathi limegubikwa na uadui kwa ndugu
na jamaa na kusababisha kutokubaliana na maamuzi ya Mahakama zilizosilkiliza shauri
hivyo kuwafanya wahusika kushindana kwa kufungua mashauri ya rufaa au maombi
mbalimbali kwenye Mahakama za juu.
Alisema hali hii huchangia ucheleweshwaji kwa kuwa
taratibu za mahakama hugeuzwa kuwa silaha za kukomoana na kuchelewesha
kukamilika kwa mashauri ya mirathi.
Aliongeza kuwa kuchelewa kwa mashauri haya huchelewesha
na hata kuwanyima warithi manufaa yao hivyo amewataka wajumbe wa kamati ya
kitaifa ya kusukuma mashauri kutafuta namna bora ya kumaliza tatizo hilo.
Baadhi ya Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Viongozi wengine wa Mahakama pamoja na wadau wakiwa kwenye kikao cha kamati ya kitaifa ya kusukuma mashauri kilichofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam.
Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Viongozi wengine wa Mahakama pamoja na wadau wakiwa kwenye kikao cha kamati ya kitaifa ya kusukuma mashauri kilichofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam.
Baadhi ya Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Viongozi wengine wa Mahakama pamoja na wadau wakiwa kwenye kikao cha kamati ya kitaifa ya kusukuma mashauri kilichofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni