Ijumaa, 18 Desemba 2020

KUJITUMA USHIRIKIANO UADILIFU SIRI YA MAFANIKIO KAZINI – JAJI MSTAAFU MATUPA

 Na Innocent Kansha, Mahakama

Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania,Devisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumu, Mhe. Sirillius Matupa amesema kujituma, kujitoa, ushirikiano, uadilifu, kuchagua na kusimamia mambo unayoyaamini ndio siri ya mafanikio katika utumishi wa umma.

 Akizungumza katika tafrija fupi ya kumuaga iliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Sheria kwa vitendo (Law School) mapema wiki hii, Jaji Mstaafu Matupa amesema kwa kufuata mambo hayo yatamuwezesha mtumishi kutekeleza majukumu yake kwa ustadi na Amani.

“Sijutii kuwa Mtumishi wa Mahakama ya Tanzania kwa kipindi chote cha utumishi wangu naondoka kifua mbele nikiiacha Taasisi yangu ikiwa imara, hivyo nawaasa watumishi kujipanga vizuri kuyapokea maisha baada ya utumishi, ni ukweli usiopingika kuna maisha baada ya utumishi wa Umma ni mazuri na hamna budi kuondoa wasiwasi changamoto ni zile zile za maisha ya kila siku”, alisema Jaji Mstaafu Matupa.

Aidha, Jaji huyo Mstaafu aliwapongeza watumishi aliofanya nao kazi kwa upendo na ushirikiano wa hali na mali katika kipindi chote alichokuwa kazini kwa ushauri, maoni, mapendekezo na hata kukosolewa pale mambo yalipokuwa yanaonekana kutokwenda sawa.

“Nashukuru kwa ushirikiano niliopata kutoka kwenu katika harakati za kuboresha utendaji wa kazi za kuwahudumia wadau wa Mahakama,” alieleza Jaji Mstaafu Matupa.

Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Devisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Lilian Mashaka alisema Jaji Matupa atakumbukwa kwa uchapa kazi wake uliotukuka, upendo, ushauri, ushirikiano na kujiamini kwake katika kutekeleza majukumu yake.

“Naamini hatutampata Jaji Matupa mwingine wa kaliba yake, alikuwa mtu wa viwango katika kazi, mnyenyekevu, msikivu na aliependa kumueshimu kila mtu aliyefanya nae kazi”, aliongeza Jaji Mashaka.  

Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Devisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Sirillius Matupa akizungumza na watumishi na wageni waalikwa (hawapo pichani) katika tafrija fupi ya kumuaga iliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Sheria kwa vitendo (Law School) Desemba 15, 2020. Aliyeketi ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Taasisi ya Chuo cha Sheria kwa Vitendo Tanzania, Mhe. Masoud Bennhaji.

Baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania waliohudhuria kwenye tafrija fupi ya kumuaga Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Devisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Sirillius Matupa (wa tatu kulia), wengine ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Devisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Lilian Mashaka, wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu na Mkuu wa Taasisi ya Chuo cha Sheria kwa Vitendo Tanzania Mhe. Masoud Bennhaji. (wa kwanza kushoto) ni Mhe.Immaculata Banzi na wa pili kushoto ni Mhe. Elinanza Luvanda.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Devisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi Mhe. Lilian Mashaka (kushoto), akimkabidhi keki Mhe. Jaji Mstaafu  Matupa (kulia) ikiwa ni ishara ya kumuaga, wengine wanaoshuhudia tukio hilo ni Majaji wa Divisheni hiyo, wa kwanza kushoto ni Mhe.Immaculata Banzi na Mhe. Elinanza Luvanda.

Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Devisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumu Mhe. Sirillius Matupa akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Divisheni hiyo wakati wa tafrija ya kumuaga, aliyekaa kushoto ni Mke wa Mhe. Jaji Mstaafu Matupa.

Baadhi ya Viongozi wa Mahakama ya Tanzania waliohudhuria tafrija ya kumuaga Jaji Mstaafu, kulia ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt, kushoto ni Mtendaji wa Devisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Bw. Willy Machumu na katika ni Mtendaji wa Mahakama Kuu- Divisheni ya Ardhi Bi.Mary Shirima.

Baadhi ya watumishi wa Divisheni hiyo wakisikiliza nasaha zilizokuwa zikitolewa na Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Devisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumu Mhe. Sirillius Matupa wakati wa tafrija hiyo.

 

 

 

 


 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni