Na Lydia Churi-Mahakama, Lushoto
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
amekitaka Chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto kuwatayarisha wahitimu wake kufanya
kazi kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa kuwa Mhimili huo
unajiimarisha katika Teknolojia ili kuondokana na matumizi ya karatasi.
Akizungumza wakati wa Mahafali ya Ishirini ya Chuo
hicho ambapo alikuwa ni Mgeni rasmi, Jaji Mkuu alisisitiza
umuhimu wa Chuo hicho kutoa
wahitimu watakaoweza kumudu
matumizi ya Tehama kutokana na mabadiliko
makubwa katika karne ya 21 yanayogusa nafasi ya Mahakama
katika utoaji wa haki, hasa
ulazima wa
matumizi hayo kama
nyenzo wezeshi katika utoaji wa haki.
“Nawasihi mboreshe matumizi ya Tehama katika kufundishia Astashahada na
Stashahada ili kuweza kupata faida katika Teknolojia hiyo inayokua kwa kasi sana”, alisema Jaji Mkuu.
Alisema wahitimu wa chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto hawana budi kwenda sambamba na Mapinduzi makubwa
yanayoendelea katika matumizi ya Tehama katika huduma za kimahakama ikiwemo ulazima wa kufahamu namna Kanuni za ufunguaji
wa mashauri kwa njia ya kielekitroniki zinavyotumika kila siku.
Prof. Juma alisema ingawa Uongozi wa Mahakama ya
Tanzania uliamua kuwa matumizi ya Tehama si hiyari tena bali ni lazima ili
Mhimili uweze kutoa huduma zake kwa ufanisi zaidi, lakini bado matumizi ni
madogo kulinganisha na uwekezaji mkubwa uliofanyika hadi sasa.
Alikitaka Chuo hicho kujiimarisha ili kitoe mafunzo kwa watumishi wa
Mahakama kwenye eneo la Utoaji haki Mtandao (migration to e-judiciary, e-justice). Alisema ni muhimu kwa Chuo hicho kutoa watumishi walioiva katika matumizi ya
Tehama ili kuendana na uwekezaji mkubwa uliofanyika kwenye eneo hilo la Teknolojia.
Akimnukuu Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa katika Utangulizi aliouandika kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025
(Tanzania Development Vision 2025), Prof. Juma alisema Hayati Mkapa alitoa picha ya ushindani
kwa wanaohitimu
katika hii Karne ya 21,
hivyo wahitimu hao wajiweke kwenye utayari wa kushindana katika
ushindani uliotajwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa
2025 na watarajie
kufanya kazi
na kuishi katika Karne ambayo imejipambanua kwa ushindani.
“Wenye Astashahada na Stashahada
watakaoshinda ni wale tu ambao wataonyesha uwezo mkubwa ki-teknolojia, uzalishaji wenye tija, uwezo wa kujisomea kila siku na
kujiongezea maarifa, na wenye ujuzi
wa hali ya juu wanaoweza kufanya
udhubutu kwenye maamuzi”,
alisisitiza Jaji Mkuu.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho,
Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Gerald Ndika amewataka wahitimu wa chuo
hicho kutambua kuwa elimu waliyoipata ni mwanzo wa safari ya kupata elimu ya
juu kutokana na kukua kwa utandawazi.
“Ni vizuri mkajua kwamba ni wajibu wenu kuendeleza kujifunza
mbinu mpya za kuyakabili mabadiliko yanayotokana na utandawazi” alisema Jaji
Ndika.
Wakati huo huo, Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia ni Jaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Paul Kihwelo aliwaasa wahitimu kuishi
katika misingi ya maadili waliyofundishwa chuoni hapo.
“Kuna mambo ya msingi ya kitabia ya kuyaishi na kuyapa
hadhi yake stahiki katika maisha yenu yote. Siku zote muishi maisha ya uadilifu”,
alisema.
Mahafali ya ishirini ya chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto yaliambatana na kilele cha sherehe za
kutimiza Miaka Ishirini tangu
kuanzishwa kwa chuo hicho Oktoba 22 mwaka 2000. Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Barnabas Albert Samatta
alizindua rasmi shughuli za masomo tarehe 6 Disemba 2000 na Rais
wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin
William Mkapa alizindua rasmi chuo hiki tarehe 3 Machi 2001.
Wahitimu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto wa
Astashahada wakiwa kwenye Maandamano tayari kwa kuanza kwa sherehe za Mahafali
yao. Haya ni Mahafali ya 20 ya chuo hicho tangu kuanzishwa kwake.
Wahitimu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto wa Stashahada wakiwa kwenye Maandamano tayari kwa kuanza kwa sherehe za Mahafali yao. Haya ni Mahafali ya 20 ya chuo hicho tangu kuanzishwa kwake.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) ambaye pia alikuwa ni Mgeni Rasmi kwenye Mahafali ya 20 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto akiwa kwenye Maandamano tayari kwa kuanza kwa sherehe za Mahafali hayo.
Wahitimu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto wa Stashahada wakiwa kwenye sherehe za Mahafali yao.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza wakati wa sherehe za Mahafali yao. Haya ni Mahafali ya 20 ya chuo hicho tangu kuanzishwa kwake.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akikabidhiwa Zawadi na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto Jaji Mhe. Dkt. Gerald Ndika wakati wa sherehe za Mahafali ya 20 ya chuo hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni