Jumatano, 30 Desemba 2020

MAHAKAMA YAONGEZA KASI MATUMIZI YA TEHAMA KURAHISISHA UPATIKANAJI WA HAKI

Na Stanslaus Makendi, Mahakama Kuu - Dodoma

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma Mheshimiwa Latifa Mansoor amewataka Mahakimu wa Kanda hiyo kujiimarisha katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha usikilizwaji wa mashauri mahakamani na upatikanaji wa haki kwa wakati.

Akizungumza wakati wa hafla ya ya ugawaji wa Kompyuta Mpakato (Laptop) zilizotolewa na Mahakama ya Tanzania kwa Mahakimu wote nchini, Jaji Mansoor aliwataka Mahakimu hao kuvitunza vizuri vitendea kazi hivyo na kuhakikisha vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa pekee.

Mahakama ya Tanzania kupitia utekelezaji wa Mpango Mkakati wake pamoja na mradi wa Maboresho ya huduma za Mahakama imewapatia Mahakimu wote nchini Laptops kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi wao kama hatua ya utekelezaji wa Mpango mkubwa wa kutoa huduma za kimahakama kwa njia ya mtandao (e-judiciary) na hatimaye haki mtandao (e-justice).

“Vifaa hivi ni vitendea kazi vya ofisi, hivyo tunatarajia vitaleta tija katika kazi zetu na hatimaye kuimarisha imani ya wananchi juu ya utendaji wa Mahakama, alisema Kaimu Jaji Mfawidhi huyo”

Mahakama za Mkoa wa Dodoma zimepatiwa jumla ya kompyuta sitini (60), mashine kubwa ya kudurufu nyaraka moja (1) na ‘Scanner’ tisa (9) ambazo zimegawiwa kwa Mahakama zote ndani ya Mkoa huo kuanzia Mahakama Kuu na Mahakama zote za chini

Mahakama ya Tanzania imetoa vifaa hivyo kwa Mahakama zote nchini kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na ufikiwaji wa lengo la utoaji wa haki kwa wakati kwa wananchi. Vifaa hivyo vinatarajiwa kuongeza kasi ya utoaji na upatikanaji wa nyaraka za maamuzi yanayotolewa na Mahakama katika ngazi mbalimbali za Mahakama nchini ikiwemo nakala za hukumu, mienendo ya mashauri na amri mbalimbali za kimahakama.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma Mheshimiwa Latifa Mansoor akimkabidhi moja wa Mahakimu kitendea kazi (Laptop)

 Mahakimu wa kanda ya Dodoma wakizungumza na Kaimu Jaji Mfawidhi wa kanda hiyo Mhe. Latifa Mansoor. 

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma Mhe. Latifa Mansoor akiwa katika picha pamoja na Waheshimiwa Mahakimu wa Kanda hiyo mara baada ya kuwakabidhi vitendea kazi. (Laptops)
Hakuna maoni:

Chapisha Maoni