Alhamisi, 24 Desemba 2020

SHERIA NA MAAMUZI YATAFSIRIWE KWA KISWAHILI ILI KUWAJENGEA WANANCHI UELEWA -WAZIRI NCHEMBA

Na Innocent Kansha – Mahakama.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ameiomba Mahakama ya Tanzania kuona uwezekano wa kubadilisha Sheria zile zinazotumika na kurejewa mahakamani mara kwa mara zitafsiriwe kwa lugha ya Kiswahili ili kuwapa fursa wananchi kupata uelewa mpana wa mambo ya kisheria pindi wanapoitafuta haki.

Akizungumza na wajumbe wa kikao cha Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania wakati wa ziara yake ya kikazi alipomtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania ofisini kwake Jijini Dar es salaam jana Waziri Nchemba alisema hata maamuzi ya mashauri yanaweza kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili kwa muhutasari tu ili kuwawezesha wadau wengi zaidi kuelewa na kuondoa sintofahamu ya wananchi walio wengi.

“Hatumaanishi kufuta lugha ya kiingereza lakini pia tusiwanyime wananchi walio wengi kufurahia lugha yao wanayoitumia kama njia ya mawasiliano hasa kupitia Taasisi muhimu na adhimu ya Mahakama ikiwa ndiyo chombo cha mwisho chenye kutoa maamuzi kwa mujibu wa katiba yetu”, alisema Dkt. Nchemba.

Dkt. Nchemba alishauri yatengenezwe mapendekezo na kuwasilishwa kwenye Mamlaka husika kama Tume ya kurekebisha Sheria na kamati za kanuni na maboresho ya sheria za Mahakama ili kuona uwezekano wa zile sheria zote zinazotumika kama rejea zitafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili.

Aidha, Waziri Nchemba aliipongeza Mahakama kwa dira na dhima imara pia miongozo thabiti iliyoleta mafanikio makubwa ya Taasisi, hasa Mpango Mkakati na mafanikio yake makubwa yanayoonekana hivi sasa, “hatuna budi kuendelea kuunga mkono juhudi hizi ili kutatua changamoto zinazoikabili Mahakama ifanye kazi kwa ufanisi na kwa ukaribu mkubwa hasa kwa yale yote yaliyo ndani ya uwezo wetu kama serikali”, alisisitiza.

Akizungumza katika kikao hicho Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi aliikumbusha Wizara kuendelea na ukamilishaji wa mchakato ulioanza muda mrefu wa Sera ya Sheria “National Legal Policy” ili kuendana na sera ya Mahakama ya mafunzo inayotumika kwa sasa.

“Mahakama inaihitaji sana Wizara katika kutekeleza majukumu yake, ziara hii imetuachia kitu cha kujivunia kama Mahakama na kuendelea kutekeleza majukumu yetu kwa kujiamini kutokana na kujitoa kwako ulikoonesha  kwetu”, aliongeza Jaji Kiongozi.

Aidha, Jaji kiongozi ameithibitishia Wizara kwamba Mahakama haitarudi nyuma bali itaendelea kushirikiana na wadau wake kwa ukaribu zaidi, huku akitolea mfano wa wa kipindi cha ugonjwa wa COVID 19 ambapo Mahakama iliendelea kuchapa kazi kwa kushirikiana na wadau wake kwa ufanisi mkubwa kwa kutumia mfumo wa Mahakama mtandao “video Conference” na kwa kuzingatia kanuni za Wizara ya Afya.

Katika hatua nyingine, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru aliiomba Wizara kushirikiana kuhimiza Matumizi ya Kamati za Maadili ya Maofisa wa Mahakama ambayo muongozo wake umeshatolewa kwa Wakuu wa Wilaya na Mikoa, kwa kutafuta namna bora ya kuendesha Kamati hizo, badala ya kutumia majukwaa yao kuwafedhehesha Maafisa hao kwa kuwa wao ni wenye viti wa kamati hizo.

“Tunapenda watambue kuwa hilo ni jukumu lao kisheria na watoe ushirikiano ili kuondoa sintofahamu inapotokea hali ya malalamiko”, alisema.

Bw. Kabunduguru alitoa rai kwa Wizara kuona uwezekana wa kuongeza bajeti kwa Tume ya Utumishi wa Mahakama kwani Tume hiyo ni kiungo muhimu katika masuala ya kumshauri Rais namna bora ya kuendesha shughuli za Mahakama.

Naye, Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama, Mhe. Zahra Maruma akitoa Taarifa ya utekelezaji wa maboresho ya Mahakama alianisha mafanikio mbalimbali yaliyotokana na Mpango Mkakati wa Mahakama wa mwaka 2015/16 hadi 2019/20, ikiwemo kiwango cha wananchi kukubali huduma zitolewazo na Mahakama kupanda na kufikia asilimia 78 kwa mwaka 2019, hii inatokana na huduma za Mahakama kuboreka na ushirikishwaji wa wadau.

Maeneo mengine ya mafanikio ni pamoja na miradi mikubwa ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya majengo ya Mahakama iliyokamilika na inayoendelea nchi nzima katika ngazi zote kuanzia Mahakama Kuu, Hakimu Mkazi, Wilaya na za mwanzo.

Mhe. Maruma alisema uanzishaji na uboreshaji wa mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) iliyorahisisha utoaji wa haki ilienda sambamba na uanzishwaji wa matumizi ya Mahakama inayotembea kwa mikoa ya Dar es salaam na Mwanza.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri, Mhe. Desdery Kamugisha akitoa taarifa ya hali ya usikilizwaji wa mashauri, alisema Mahakama imefanya kazi kubwa ya kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano na Dira ya maendeleo ya Taifa ya 2025.

Mahakama imeendelea kupiga hatua katika kusikiliza na kumaliza mashauri kwa wakati, hii inathibitishwa na taarifa kwamba kuanzia Januari 2020 hadi Novemba 2020, Mahakama katika ngazi zote imefanikiwa kusikiliza mashauri 220,872 kati ya mashauri 219, 527 yaliyofunguliwa na yale yaliyobaki mwezi Desemba 2019 ambayo ni sawa na asilimia 101.

Mhe. Kamugisha alisema jumla ya mashauri ya Jinai 2,499 yanaendelea kutajwa katika Mahakama za Hakimu Mkazi. Kati ya mashauri hayo kuna mashauri 788 ya jinai kawaida, mashauri 818 ya mauaji, mashauri 865 ya rushwa na uhujumu uchumi na mashauri 28 ya makossa ya usalama barabarani.

Jumla ya mashauri ya Jinai 4,469 yanaendelea kutajwa katika Mahakama za Wilaya nchini. Kati ya mashauri hayo mashauri 1,232 ni ya jinai kawaida, mashauri 1,754 ya mauaji, mashauri 1,422 ya rushwa na uhujumu uchumi na mashauri 61 ya makossa ya usalama barabarani, aliongeza Mhe. Kamugisha.

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (katikati) akizungumza na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania (hawapo pichani) alipofanya ziara yake ya kikazi kumtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania, Kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Geofrey Mizengo Pinda (kushoto).

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (wa pili kulia) alipomtembelea ofisini, kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi na kushoto ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Geofrey Mizengo Pinda.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akisaini Kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili ofisini kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Jijini Dar es salaam kwa ziara ya kikazi, Desemba 23,2020 kulia ni Naibu Waziri wa Katibu na Sheria Geofrey Mizengo Pinda.



Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (kushoto) akimkabidhi Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (kushoto) Miongozo mbalimbali iliyoandaliwa na Mahakama kusaidia kurahisisha utoaji haki.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiwa kwenye picha ya pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (wa pili kushoto), Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru (wa pili kulia), Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Geofrey Mizengo Pinda (wa kwanza kushoto) na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma (wa kwanza kulia) pamoja na Viongozi waandamizi wa Wizara naMahakama ya Tanzania. 


 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni