Jumamosi, 16 Januari 2021

MAHAKAMA 'SACCOS' YATAKIWA KUJITANGAZA

 Na Mary Gwera, Mahakama

Wanachama wa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Mahakama (SACCOS) wametakiwa kuongeza wigo wa kuutangaza ushirika huo ili watumishi wengine wa Mhimili huo waweze kujiunga na ushirika huo kwa manufaa mbalimbali.

Akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa mwaka 2020 wa SACCOS-Mahakama mapema leo Januari 16, 2021, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu-Masjala Kuu, Mhe. Nyigulila Mwaseba  alisema kuwa Viongozi na Wanachama wa SACCOS waongeze kasi ya kutangaza faida za Chama hicho.

Mhe. Mwaseba ambaye alimwakilisha mgeni rasmi Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt alisema kuwa idadi ya Wanachama wa SACCOS haishabihiani na idadi iliyopo ya Watumishi wa Mahakama nchini na hivyo kuwashauri kutumia njia mbalimbali kuongeza idadi yao.

“Kwanza ninashukuru kwa kuialika Ofisi ya Msajili Mahakama Kuu kuwa mgeni, naomba nikiri kuwa nimejulishwa faida nyingi za SACCOS ikiwemo kuwasaidia watumishi wa Mahakama kupata mikopo ya riba nafuu, mikopo kupatikana ndani ya miezi mitatu ya kuchangia na kadhalika,” alisema.

Aliongeza kwa kupendekeza kuwa wanachama kutoka kada mbalimbali wawahamasishe ili kupata wanachama wengine.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa SACCOS-Mahakama anayemaliza muda wake, Bw. Edwin Protas alisema Chama hicho hicho kinakabiliwa na changamoto ya mtaji mdogo huku akitoa rai kwa watumishi wengine wa Mahakama kujiunga na Chama hicho.

Katika mkutano huo ulioshirikisha wanachama kutoka Mahakama mbalimbali nchini, kutakuwa na uchaguzi mkuu wa Viongozi wa Chama baada ya kumalizika kwa muda wa viongozi waliokuwepo.

Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Mahakama (SACCOS) kilianzishwa mnamo mwaka 1970, kwa sasa kina jumla ya Wanachama 335.

Naibu Msajili, Mahakama Kuu-Masjala Kuu, Mhe. Nyigulila Mwaseba akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka 2020 wa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Mahakama (SACCOS) uliofanyika katika Ukumbi wa Mahakama Kuu-Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa SACCOS-Mahakama, Bw. Edwin Protas akizungumza wakati wa mkutano huo.




Sehemu ya Wanachama wa SACCOS waliohudhuria Mkutano huo.

(Picha na Mary Gwera, Mahakama)


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni