Jumatano, 12 Mei 2021

JAJI MKUU ATAMBULISHWA NAIBU WAKUU WAPYA WA CHUO

Na Innocent Kansha – Mahakama.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amekutana na kuwapokea Naibu Wakuu wawili (2) wapya kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA) kwa lengo la kujitambulisha. Watumishi hao ni Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Huduma za Ushauri Bw. Goodluck Chuwa na Naibu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala Dkt. Fatihiya Massawe.

Akizungumza katika tukio hilo mapema leo Mei 12, 2021 Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam Jaji Mkuu Prof. Juma aliwapongeza kwa kuteuliwa kwao kuwa Watumishi wa Chuo na kuwataka watumie muda wao kujifunza shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na chuo ili kumudu majukumu yao ya kitaasisi, katika kuboresha na kuimarisha huduma za utoaji haki. Mahakama inasisitiza matumizi ya mifumo ya kiteknolojia ili kutoa haki kwa haraka na uwazi zaidi. 

“Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ni miongoni mwa shabaha ya Mahakama ya Tanzania katika kuboresha utendaji kazi na kuleta mapinduzi makubwa katika mfumo wa utoaji haki nchini ili tuondokane na matumizi ya karatasi na hii ndiyo dhana halisi ya Mapinduzi ya nne (4) ya Viwanda inavyojitanabaisha”, aliongeza Jaji Mkuu.

Aidha, Jaji Mkuu aliwakaribisha na kuwaahidi kutoa ushirikiano wa kitaasisi katika kutekeleza majukumu yao.

Awali katika utambulisho huo, Watumishi hao waliambatana na mwenyeji wao ambaye ni Mkuu wa Chuo hicho, na Jaji mteule wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Dkt. Paul Kihwelo kwa lengo la kujitambulisha kama watumishi wapya kwa ngazi za Unaibu Mkuu wa Chuo.

 

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (mwenye tai nyekundu) akiwa kwenye picha ya pamoja na Naibu Wakuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA) waliofika Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujitambulisha kama watumishi wapya wa Chuo hicho mapema leo Mei 12, 2021, wengine ni Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Jaji Mteule wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (mwenye suti nyeusi), kulia ni Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Huduma za Ushauri Bw. Goodluck Chuwa na kushoto ni Naibu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala Dkt. Fatihiya Massawe.


Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA) Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Dkt. Gerald Ndika akiwa kwenye mazungumzo na Naibu Wakuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA) walipofika Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam mara baada ya kutambulishwa kama watumishi wapya wa Chuo hicho.

Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Huduma za Ushauri Bw. Goodluck Chuwa (kulia) na Naibu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala Dkt. Fatihiya Massawe (kushoto) wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kujitambulisha kama watumishi wapya wa Chuo hicho mapema leo Mei 12, 2021, Ofisini kwa Jaji Mkuu. 

(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni