Jumatatu, 17 Mei 2021

TENDENI HAKI KWA KUEPUKA MBINU ZA KIUFUNDI – JAJI MKUU

Na Innocent Kansha – Mahakama.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewapongeza Majaji wateule wa Mahakama ya Rufani kwa kuteuliwa kwao na kuwaomba watakapo kuwa wakisiliza mashauri zingatieni kupunguza mbinu za kiufundi ili haki ionekane ikitendeka kwa wananchi.

Akizungumza katika tukio hilo mapema leo asubuhi Mei 17, 2021 Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam Jaji Mkuu Prof. Juma alisema mbinu za kiufundi zinachelewesha upatikanaji wa maamuzi ya kimahakama moja ya maeneo ya maboresho ni hilo, msisite kuwasilisha mapendekezo na maoni yenu kwenye Kamati ya Jaji Mkuu ya Maboresho ya Sheria na Kanuni hasa kwenye maeneo mnayoona yanahitaji kufanyiwa hivyo.

 “Mmeteuliwa kutoka miongoni mwa idadi kubwa ya Majaji waliopo Mahakama Kuu, ni matarajio yetu mtatenda kazi zenu kwa ufanisi, uwazi na kwa kuzingatia weledi wa hali ya juu mkitambua ninyi ni tegemeo la Mahakama ya Tanzania na mtatoa huduma katika nafasi zenu kwa muda mrefu zaidi”, alisema Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu alisema taswira ya utoaji haki nchini inawategemea ninyi mkiwa kama Majaji wa Mahakama ya Rufani. Mahakama inapitia Maboresho mengi mbalimbali yakiwemo ya Sheria na Kanuni. Aidha akifafanua alisema, mmeteuliwa kutenda haki katika ngazi ya juu kabisa na mtatazamwa sana na kila mtu hata hivyo mtapimwa kwa kupitia maamuzi mtakayo yatoa kila siku.

Aliongeza kuwa Taaluma ya Sheria inapitia mageuzi makubwa kutokana na utandawazi wananchi wengi wanauelewa mpana wa masuala ya kisheria hasa katika karne ya 21 yenye ushindani mkubwa na inatawaliwa na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Profesa Juma alitoa angalizo kwa Majaji Wateule wa Mahakama ya Rufani kwamba itawalazimu kuendelea kujielimisha kwa mambo mengi zaidi ili kuendana na kasi hiyo, Mahakama inategemea kujifunza mambo mengi mazuri kutoka kwao.

Naye Jaji Mteule wa Mahakama ya Rufani, Mhe Patricia Fikirini akitoa neno kwa niaba ya Majaji wenzake alimshukuru Jaji Mkuu kwa kuwaalika na akamuhakikishia Jaji Mkuu kwamba wapo tayari kupokea majukumu na kutenda kazi waliyoaminiwa.

“Tunaahidi atutakuangusha wewe Jaji Mkuu wala Mahakama ya Tanzania, sisi sote kwa pamoja tumefanya kazi kwa muda mrefu kwa ushirikiano wa karibu, tutakupa ushirikiano uliotukuka wakati wote wa utumishi wetu”, alisistiza Jaji huyo Mteule wa Mahakama ya Rufani.

 

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyeketi mbele ya picha ya Rais) akiwa kwenye kikao cha pamoja na Majaji Wateule wa Mahakama ya Rufani walipomtembelea Ofisini kwake leo Mei 17, 2021.

Baadhi ya Majaji Wateule wa Mahakama ya Rufani wakiwa Ofisini kwa Jaji Mkuu wa Tanzania walipomtembelea na kukutana nae kwa mazungumzo wa kwanza kushoto ni Jaji Mteule wa Mahakama ya Rufani Mhe.Lilian Leonard Mashaka, na wa pili kushoto ni Jaji Mteule wa Mahakama ya Rufani Mhe. Patricia Saleh Fikirini, wa pili kulia ni Jaji Mteule wa Mahakama ya Rufani Mhe Abraham Mwampashe na wa kwanza kulia ni Jaji Mteule wa Mahakama ya Rufani Mhe. Issa John Maige.

Baadhi ya Majaji Wateule wa Mahakama ya Rufani wakiwa Ofisini kwa Jaji Mkuu wa Tanzania walipomtembelea na kukutana nae kwa mazungumzo wa kwanza kulia ni Jaji Mteule wa Mahakama ya Rufani Mhe. Pentelni Mlisa Kente, katikati ni Jaji Mteule wa Mahakama ya Rufani Mhe. Lucia Gamuya Kairo na kushoto ni Jaji Mteule wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Paul Kihwelo.

Picha na Innocent Kansha - Mahakama

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni