Na Faustine Kapama – Mahakama.
Msajili
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amewasihi wajumbe wa menejimenti
ya Mahakama kuboresha utendaji na kuacha kufanya kazi kwa desturi na mazoea ya
awali ili wadau wa ndani na wananchi kwa ujumla wapate huduma zilizo bora.
Mhe. Chuma
alitoa wito huo jana tarehe 28 Septemba, 2022 alipokuwa anafunga mafunzo ya
siku tatu kuhusu uongozi
bora kwa wajumbe hao kutoka kurugenzi, vitengo na idara mbalimbali yaliyokuwa
yanayofanyika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia
Temeke jijini Dar es Salaam.
“Rai
yangu kwenu ni kwamba, ushiriki wenu na tija ya mafunzo haya udhihirishwe
katika ubora wa huduma mtakazokuwa mnatoa kwa umma na kwa watumishi wenzenu. Kwa
kuzingatia mada zilizotolewa ni matumaini yangu kuwa tutaishi na kushirikiana
vyema na watumishi walio chini yetu pamoja na viongozi kwa ujumla,” alisema.
Msajili
Mkuu huyo aliwaomba wajumbe hao wa menejimenti kila siku kukumbuka na kujiuliza
kwa namna gani wanawasaidia wale waliopo chini au juu yao katika utendaji wao
wa kazi ili kufikia malengo ya taasisi, kwa maana ya Mhimili wa Mahakama.
Kadhalika,
Mhe. Chuma aliwasihi kutoa ushauri, maoni na mapendekezo kwa uongozi wa
Mahakama yenye mlengo wa kutatua changamoto mbalimbali katika uendeshaji wa
shughuli za Mahakama. “Kazi yako kubwa kama kiongozi ni kuondoa vikwazo na
kutatua changamoto na siyo kuwa sehemu ya tatizo. Tafuta majibu ya tatizo,” aliwaambia
wajumbe hao.
Amesema
kufanyika kwa mafunzo hayo kumekuwa chachu ya kuboresha uendeshaji wa shughuli
za Mahakama katika Kurugenzi, Idara, Vitego na sehemu mbalimbali wanazofanyia
kazi. Mhe. Chuma alisema kuwa ni matarajio ya uongozi wa Mahakama kuwa mafunzo
hayo yamewaongezea ufanisi wa kazi ya msingi ya kutoa haki kwa wakati na kwa
watu wote.
“Ni imani
yangu kuwa mafunzo haya mahususi yamewaongezea ujuzi na weledi katika huduma ya
utoaji haki kwa wakati kama inavyoelezwa na Dira ya Mpango Mkakati wetu. Aidha,
ni imani yangu kuwa mafunzo haya yamewawezesha kuwa na uelewa wa pamoja katika
maeneo (mbalimbali),” alisema.
Msajili
Mkuu huyo aliwakumbusha washiriki wa mafunzo maneno yaliyowahi kusemwa na Mkuu
wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na Jaji wa Mahakama ya Rufani,
Mhe. Dkt. Paul Kihwelo aliyoyasema tarehe 30 Aprili, 2021 wakati wa ufunguzi wa
sehemu ya mafunzo chuoni hapo.
Alimnukuu
Mhe. Dkt. Kihwelo akisema, “Haitoshi tu kuhudhuria mafunzo na kupata cheti. Inafaa
zaidi ukipata mafunzo ukayatumie kwa ubora uliokusudiwa kwako wewe na kwa
maafisa wengine wa Mahakama na kuleta mabadiliko chanya pamoja na kwamba
mabadiliko wakati mwingine yana maumivu yake…...”
Awali,
akitoa taarifa kwa ufupi kuhusu mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo wa Mahakama
ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu alimweleza Msajili Mkuu kuwa
katika kipidi hicho cha siku tatu, wajumbe wa menejimenti wapatao 34 walipitishwa
katika maeneo mbalimbali, ikiwemo utamaduni wa Mahakama ya Tanzania na fikra za
kimkakati.
Bi.
Ngungulu alitaja maeneo mengine yaliyoguswa wakati wa mafunzo hayo yaliyoanza tarehe
26 Septemba, 2022 ni namna ya kuhimili mihemuko, huduma ya wateja katika
muktadha wa Mahakama, itifaki na utii, muundo wa Serikali na utawala wake,
uongozi na maadili yake, usimamizi wa ofisi, uandishi wa taarifa, uwianisho wa
taaluma na utu na udhibiti wa msongo wa mawazo na masuala ya kisaikolojia.
“Kwa
mada hizi (washiriki wa mafunzo haya) walizojifunza, ni imani yetu sisi Sekretarieti
na Kurugenzi ya Utawala na Rasilimali Watu kuwa tumejifunza, hatutoki kama vile
tulivyokuja, tunatoka na kitu. Pengine kila mmoja wetu atajitahidi kukitumia
kile alichojifunza hapa katika kuboresha utendaji wa kazi,” alisema.
Mmoja wa washiriki, Bi. Glady Qambaita akitoa neno la shukurani kwa uongozi wa Mahakama kwa kuwezesha uwepo wa mafunzo hayo.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo (juu na chini) wakifuatilia hotuba iliyokuwa inatolewa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (hayupo katika picha).
Sehemu nyingine ya washiriki wa mafunzo hayo (juu na chini) wakifuatilia jambo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni