MWENYEKITI TUME YA KUREKEBISHA SHERIA ATEMBELEA UJENZI WA MAHAKAMA KUU TABORA
Na Amani Mtinangi – Mahakama, Tabora
Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania,
Jaji wa Mahakama ya Rufani Mstaafu, Mhe. January Msoffe jana tarehe 28
Septemba, 2022 alitembelea mradi wa ukarabati na upanuzi wa jengo la Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora.
Lengo la ziara ya Mhe. Msoffe, ambaye aliambatana na
viongozi wa Mahakama Kuu Tabora ilikuwa kujionea hatua za maendeleo za mradi huo
unaotekelezwa na Kampuni ya M/S CRJE (East Africa) LTD katika Manispaa ya
Tabora ambao kwa sasa upo katika hatua za mwisho.
Baada ya kutembelea na kupatiwa maelezo kuhusu
utekelezaji wa mradi huo, Mwenyekiti wa Tume hiyo alipongeza na kusifu kazi
kubwa na nzuri inayoendelea kufanywa na timu ya Mkandarasi akishirikiana na
Wakala wa Majengo Tanzania na Mahakama ya Tanzania.
Mhe. Msoffe alijionea mabadiliko makubwa yaliyofanyika
ukilinganisha na kipindi cha nyuma wakati akija kusikiliza mashauri ya Mahakama
ya Rufani. Aliongeza kuwa ubunifu mzuri umeliwezesha jengo hilo kukidhi
mahitaji ya watumishi na wadau wote wa Mahakama kama ilivyo kwenye majengo
mengi ya kisasa yanayojengwa na Mahakama.
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Tabora, Mhe. Amour Khamis alisema kuwa mradi huo utakapomalizika na kuanza
kutumika utawezesha watumishi, wadau na wateja kuwa na mazingira mazuri ya
kufanyia kazi na kupokea huduma tofauti na ilivyokuwa awali.
Alisema kabla ya ukarabati na upanuzi huo kulikuwa na
uhaba wa vyumba, ufinyu wa ofisi na kukosekana kwa mifumo thabiti ya usalama wa
jengo na watumiaji wake. Mhe. Amour aliushukuru uongozi wa Mahakama ya Tanzania
kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi huo.
Akitoa maelezo ya utangulizi kwa Mwenyekiti wa Tume hiyo
kwa niaba ya Mshauri Mwelekezi wa Mradi, ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania
(TBA), Mbunifu Majengo, Bw. Malimi Masala alisema mifumo yote inayohitajika
imezingatiwa ili kulifanya jengo hilo kuwa rafiki kwa watumiaji wote hata wenye
mahitaji maalum.
Kwa upande mwingine Mhandisi
Majengo kutoka TBA Goodluck Sanga alisema kuwa mradi huo uliopo katika hatua
za mwisho unatekelezwa kwa kuzingatia mahitaji yote muhimu ya kimahakama, afya
ya watumiaji na usalama wa jengo kama uwepo wa mifumo ya TEHAMA, umeme, mifumo
ya kuzimia moto, maji na pia mandhari nzuri kwa kuweka bustani za majani.
Kaimu Mtendaji wa Mahakama, Kanda ya Tabora, Bw. Ginaweda
Nashon alieleza kuwa Mahakama Kuu Tabora itakuwa tayari kulipokea jengo hilo
baada ya mifumo muhimu kukamilika na kufanya kazi ipasavyo. Alisema baadhi ya
samani za ofisi zipo njiani na utengenezaji wa mapazia unaweza kukamilika muda
wowote kuanzia sasa.
Akahimiza kukamilika kwa shughuli zote muhimu ili jengo
hilo lianze kutumika. Mradi huo ambao ulianza kutekelezwa tarehe 16 Julai, 2021
unatarajia kumalizika na kukabidhiwa hivi karibuni tayari kwa watumizi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni