Na Mary Gwera, Mahakama
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Mustapher Siyani amezindua rasmi Tovuti ya Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni
ya Kazi (labourcourt.judiciary.go.tz) huku akizitaka Mahakama nyingine anazozisimamia
kubuni njia mbalimbali zilizopo ndani ya uwezo wao ili kuweza kufikisha taarifa
za kimahakama kwa wananchi wengi kwa urahisi zaidi.
Akizungumza leo tarehe 30 Septemba, 2022 katika hafla
fupi ya kuzindua Tovuti ya Divisheni hiyo iliyopo Kinondoni jijini Dar es
Salaam, Mhe. Siyani amesema kwa kuwa sera ya Mahakama inaelekeza kuimarisha
matumizi ya TEHAMA kote nchini, hivyo ni muhimu kuendelea kuchukua hatua kadhaa
ili kutimiza azma ya Mahakama ya kuwa na matumizi kamili ya mtandao ‘e-Judiciary’
ifikapo mwaka 2025.
“Kila Mahakama kote nchini ni vyema sana ikatafuta na
kubuni namna tofautitofauti kulingana na uwezo wake kuona inawezaje kuwafikia
wananchi walio wengi, hilo ndio lengo letu kusogeza huduma kwa wananchi,
kwahiyo tovuti hii ni moja ya njia za kuwafikia wananchi, hivyo mwananchi
yeyote mwenye simu janja popote alipo anaweza kupata taarifa kuhusu Mahakama
hii” amesema Jaji Kiongozi.
Ameipongeza Divisheni ya Kazi kwa kuamua kutekeleza
kwa vitendo ajenda ya uboreshaji wa huduma za Mahakama na mageuzi yaliyoainishwa
katika Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021-2024/2025 unaolenga kuifanya
Mahakama ya Tanzania kuwa Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’. Akiongeza kuwa,
upatikanaji wa tovuti hiyo ni muhimu na una faida kubwa kwani itawawezesha
Wadau wa Divisheni hiyo kuifikia Mahakama kwa urahisi zaidi.
Aidha; Mhe. Siyani amewasisitiza Viongozi wa Divisheni
hiyo kuzingatia matumizi ya Kiswahili katika Tovuti ili wananchi wa aina zote
waweze kupata taarifa zilizomo.
“Jambo jingine ambalo ningependa kusema kupitia hafla
hii ni kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili kupitia tovuti. Kwa ngazi ya
Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi imekuwa kinara na kuenzi matumizi ya lugha hii
adhimu, hivyo, ni matarajio yangu na bila shaka nimefurahi kusikia kwamba,
hatua zinachukuliwa kuhakikisha kuwa, tovuti hii inamuwezesha mwananchi kupata
taarifa zote muhimu kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza,” amesisitiza Jaji
Kiongozi.
Ameongeza kwa kuwaomba Wadau wa Divisheni hiyo hususani
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) hapa nchini kuendelea
kushirikiana na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kutafsiri nyaraka mbalimbali za
kimahakama zilizo katika lugha ya Kiingereza ikiwezo uamuzi na mikataba
mbalimbali ya kimataifa kwenda kwenye lugha ya Kiswahili, lakini pia na kuanza
kuweka misamiati mingi inayotumika katika Mahakama hiyo.
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni
ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi amesema lengo la kuanzisha tovuti ya Divisheni
hiyo ni kuwarahisishia wadau wa Mahakama hiyo kupata kwa urahisi na kwa haraka
taarifa mbalimbali ikiwemo rejea za Sheria na Kanuni za Kazi na Ajira, uamuzi
wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani yanayohusisha mashauri ya kazi.
“Tovuti hii itakuwa inaonesha taarifa mbalimbali za Mahakama
hii mfano ‘causelist’ ya kila wiki kwa kila Jaji na Msajili, taarifa za vikao
maalum vya mashauri (Special Court Sessions), taarifa za kutokuwepo kwa Majaji
na Wasajili ili kuokoa muda wa wadau ili wasifike mahakamani. Tovuti hii pia
imeunganishwa na Tovuti ya Mahakama ya Tanzania ambapo imo mifumo mbalimbali
ikiwemo Mfumo wa kuhifadhi hukumu za Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani, Sheria
na Kanuni mbalimbali ‘TanzLII’,” amesema Mhe. Maghimbi.
Ameongeza kuwa, Tovuti hiyo imeunganishwa na tovuti za
wadau muhimu ambao ni Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Chama cha
Waajiri (ATE), Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na Shirika la Kazi Duniani
(ILO).
Amesema uanzishwaji wa tovuti hiyo iliyotengenezwa na baadhi
ya Watumishi/Wataalam wa ndani wa Divisheni hiyo unaenda sambamba na utekelezaji
wa nguzo namba moja ya Mpango Mkakati wa Mahakama wenye lengo la kuboresha na
kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji haki na kuboresha miundombinu ya kitehama
katika ngazi zote za Mahakama.
Kwa upande mwingine, Jaji huyo alimtaarifu Jaji Kiongozi
kuhusu hatua kubwa waliyopiga kwenye umalizaji wa mashauri huku akibainisha
kuwa, mpaka kufikia leo ni mashauri matatu (3) pekee ya mwaka 2021 yaliyobaki
ambayo yote yako katika hatua ya hukumu na mpango uliopo ni mashauri hayo yawe
yamemalizika ifikapo tarehe 06 Oktoba, 2022, na hivyo kubaki na mashauri ya
mwaka 2022 tu.
Akitoa neno la utangulizi, Mwenyekiti wa Kamati maalum
ya Utengenezaji wa Tovuti ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ambaye pia ni Jaji
wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Biswalo Mganga amesema kuwa, tovuti
hiyo imekidhi viwango vya kiusalama na mamlaka husika (eGA) wameridhia ianze
kufanya kazi.
“Mahakama ya Kazi tuliona ni vizuri wananchi wafikiwe
kwa urahisi zaidi pamoja na kuwakusanya wadau kwa pamoja kwahiyo njia mojawapo
tuliyokubaliana kwa pamoja ni kuanzia tovuti ambayo imejumuisha pia tovuti za
wadau wetu ili tuweze kuwasiliana kwa urahisi na kuwawezesha wananchi kupata taarifa
mbalimbali kwa urahisi zaidi. Na niwahikishie kuwa Tovuti hii iko salama na tumezingatia
vigezo vyote vya uanzishwaje wake,” amesema. Mhe. Mganga.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akibonyeza kitufe kwenye kompyuta mpakato kuashiria ufunguzi wa tovuti ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi leo tarehe 30 Septemba, 2022.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akizungumza kabla ya ufunguzi rasmi wa tovuti ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi akisisitiza jambo alipokuwa anaongea kwenye ufunguzi wa tovuti ya Mahakama hiyo.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni