·Kutoa dozi kutwa mara tatu kwa kila timu.
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Tanga
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports)
imewasili jijini Tanga leo tarehe 1 Octoba,2022 kushiriki mashindano ya Shirikisho
la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI).
Kuwasili kwa Timu hiyo inayoshiriki katika michezo
nane mwaka huu ya Kamba Wanaume na Wanawake, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli,
Bao, Karata, Tufe, Riadha Wanaume na Wanawake pamoja na Baiskeli kumezua gumzo
kwenye viunga mbalimbali jijini hapa na kufanya baadhi ya wapinzani kuanza
kuweweseka.
Hatua hiyo inaonekana kuwakatisha tamaa wapinzani wa Mahakama
Sports baada ya kusikia minong'ono ya
chini chini kuwa timu hiyo ya Mahakama mwaka huu haipo vizuri na haitashiriki
mashindano.
"Jamaa wameshafika, sijui itakuwaje mwaka huu.
Tusipojipanga vizuri tutabaki kuwa wasindikizaji tu katika mashindano haya.
Hawa jamaa ni hatari, hasa kwenye mchezo wa Kamba, aisee wapo vizuri sana.
Hatuwawezi hawa," alisikika mwanamichezo mmoja ambaye hakufahamika anatoka
taasisi gani.
Akizungumza muda mchache baada ya kufika Tanga, Katibu
wa Mahakama Sports Donald Tende amesema wanamichezo wote wamefika salama na
wapo tayari kwa mashindano.
"Wachezaji wote wapo vizuri na tupo tayari kwa
michezo ambayo ipo mbele yetu. Kama kawaida yetu, Mahakama inatoa haki, tutatoa
haki sawa kwa wakati na kwa wote bila upendeleo wowote, tunaomba wapinzani wetu
walijue hilo,” alisema.
Tende ameonya kuwa haki watakayotoa kwa kila mpinzani
itaenda sanjari na dozi ya ‘kutwa mara tatu’ kwa kila mpinzani atakayejitutumua
na kutunisha misuri. "Safari hii hatubakishi kitu kwenye mashindano haya,
tuna wachezaji wazuri sana mwaka huu kwenye kila mchezo tunaoshiriki,"
alisema.
Mwalimu wa Timu Spear Mbwembwe amesema mara baada ya
kuwasili wachezaji wote wataenda moja kwa moja kambini kujiwinda na mechi kesho
tarehe 2 Octroba, 2022 kwenye michezo yote. "Hatuna muda wa kupoteza,
Mahakama Sports haipoi. Tunataka dozi tutakazotoa ziwe takatifu, nadhani
wapinzani wetu wanalijua hili," alisema.
Kwa mujibu wa ratiba ya mashindano, Mahakama Sports
Kamba Wanaume imepangwa kwenye kundi A pamoja na Ikulu, Dodoma RAS na Haki na
itaanza kupeperusha bendera ya Mahakama ya Tanzania kwa kutunishiana misuri na
Haki kesho tarehe 2 Octoba, 2022 na baadaye itakutana na RAS Dodoma tarehe 4 Octoba,
2022 kabla ya kumaliza mzunguko wa makundi na Ikulu tarehe 6 Octoba, 2022.
Ratiba hiyo inaonyesha Kamba Wanawake imepangwa kundi
A na timu za Maji, RAS Kilimanjaro na Viwanda na katika mechi ya kwanza
itakutana na Maji kesho tarehe 2 Octoba, 2022 na baadaye kupepetana na RAS Kilimanjaro
tarehe 4 Octoba, 2022 na kumaliza kwenye kundi hilo na Viwanda tarehe 6 Octoba,
2022.
Mahakama Sports Mpira wa Miguu Wanaume imepangwa kundi
D na timu za Tume ya Utumishi wa Umma, Ukaguzi na Hazina na itatupa karata yake
ya kwanza kwa kumenyana na Ukaguzi kesho tarehe 2 Octoba, 2022 na baadaye kukutana
na Hazina tarehe 4 Octoba, 2022 kabla ya kumaliza mechi za makundi tarehe 6 Octoba,
2022 kwa kukutana na Utumishi.
Katika Mpira wa Netiboli, Mahakama Sports imepangwa
katika kundi H na timu za Ujenzi, Kilimo, Waziri Mkuu Kazi na RAS Mtwara na
itaanza kupambana na RAS Mtwara kesho tarehe 2 Octoba, 2022 na baadaye kukutana
na Ujenzi tarehe 4 Octoba, 2022. Tarehe 6 Octoba, 2022 Timu hiyo itakutana uso
kwa uso na Waziri Mkuu Kazi, kabla ya kumaliza mechi za makundi kwa kukutana na
Kilimo tarehe 7 Octoba, 2022.
Mashindano ya SHIMIWI ambayo yameanza leo tarehe 1
Octoba, 2022 yanatarajiwa kufunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassimu Majaliwa tarehe 5 Octoba, 2022. Kauli
mbiu ya mashindano ya SHIMIWI 2022 ni “Michezo hupunguza magonjwa yasiyo
ambukiza na kuongeza tija mahala pa kazi.”
Mashindano hayo ambayo yanashirikisha michezo mbalimbali
yatafanyika katika viwanja tofauti tofauti nane ambavyo ni Viwanja vya
Mkwakwani, Shule ya Sekondari Popatlal, Galanos Sekondari, Bandari, Shule ya
Tanga, Polisi Chumbageni na Viwanja vya Gymkhana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni