·Waichapa RAS Simiyu tano ikiingia nusu fainali
·Wakubali mziki wao hauchezeki
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Tanga
Timu ya Mahakama Sports
Mpira wa Miguu Wanaume leo tarehe 12 Octoba, 2022 imeingia katika hatua ya nusu
fainali kwa kishindo kikubwa baada ya kuigaragaza RAS Simiyu kwenye mashindano
ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika
jijini hapa.
Mahakama Sports iliichapa
Timu ya RAS Simiyu mabao 5:1 katika mechi ya robo fainali baada ya kutandaza
kabumbu safi na la kuvutia. Mchezo huo umevuta hisia za washiriki wengi wa SHIMIWI
kufuatia mizengwe iliyokuwa imesababishwa na Timu ya Uchukuzi hapo awali.
Mchezo huo ambao
umechezwa kuanzia majira ya saa tatu asubuhi ulianza kwa kasi huku timu zote mbili
zikishambuliana kwa zamu. RAS Simiyu walikuwa wa kwanza kulisalimia lango la
Mahakama katika dakika za mwanzo mwanzo, lakini bao hilo lilikataliwa kutokana
na mfungaji kuwa katika nafasi ya kuotea.
Baada ya kuingia kwa bao
hilo, Mahakama Sports wakachachamaa na kulisakama lango la wapinzani wao mara
kwa mara. Winga machachari wa Mahakama Sports Shamte Seif alifungua kalamu ya
magori kwa timu yake katika dakika ya 10 ya mchezo baada ya kuukwamisha mpira
katika nyavu kufuatia pasi ya upendo kutoka kwa Mshambuliaji hatari Martin
Mapinduzi.
Dakika nne baadaye, Mshambuliaji
huyo aliweka mpira kwenye kamba baada ya kupokea pasi mpenyezo kutoka kwa Kiungo
wa Juu Gabriel Tabana na kuiandikia timu yake bao la pili.
Pamoja na magori hayo,
Mahakama Sports iliendelea kutandaza kandanda safi na kushambulia lango la RAS
Simiyu kama nyuki na kufanikiwa kupata bao la tatu katika dakika ya 31 ya
mchezo kupitia Frank Obadia aliyepokea pasi nyororo kutoka kwa mshambuliaji
Martin Mapinduzi.
Hadi timu zote mbili zinaenda
katika mapunziko, ubao wa matokeo ulikuwa unasomeka 3:0. Kipindi cha pili
kilipoanza, RAS Simiyu walilishambulia lango la Mahakama kwa dakika za mwanzo
na kufanikiwa kupachika bao baada ya mabeki kutoka timu pinzani kujichanganya.
Kuingia kwa bao hilo
kuliwaamsha wachezaji wa Mahakama na kuanza kumiriki mpira na kucheza pasi fupi
fupi zilizowachanganya wapinzani wao. Katika dakika ya 54, Frank Obadia
aliingia tena kwenye nyavu baada ya kupachika bao safi kufuatia pasi ya upendo
kutoka kwa Kiungo Gabriel Tabana.
Mahakama Sports
ilizidisha mashambulizi kila wakati na kuwafanya wapinzani wao kukata pumzi na
kupoteana, hatua iliyowapa mwanya mwingine wachezaji wa Mahakama kutumia udhaifu
wa RAS Simiyu kupachika bao la tano na la mwisho kwa mchezo huo kutoka kwa
mshambuliaji Martin Mapinduzi.
Katika vipindi vyote viwili,
timu zote zilifanya mabadiliko ya wacgezaji, ambayo yaliinufaisha Mahakama
Sports ambo waliweza kupata mabao mawili katika kipindi cha pili.
Hadi mwamuzi anapuliza
kipenga cha kumaliza mpambano huo, matokeo ya mchezo huo yalikuwa yanaonyesha
5:1 kwa Mahakama na RAS Simiyu, mtawaliwa. Kufuatia ushindi huo, Mahakama
Sports itamenyana na Timu ya Ulinzi katika hatua ya nusu fainali.
Akizungumza baada ya
mchezo huo, Katibu wa Mahakama Sports Robert Tende amewapongeza wachezaji wote
kwa kujituma na kuipigania timu kwa ujumla ili ipate matokeo mazuri. Amewaomba
wachezaji hao kuendelea kujipanga kwa mechi inayofuata kwani hatua waliyofikia
siyo mchekea.
Kwa upande wake, Mwalimu
wa Timu hiyo Spear Mbwembwe aliwataka wachezaji kukaza uzi zaidi, kwani safari
bado haijaisha. Amewatumia salamu wapinzani wao wanaokuja kuwa kazi inaendelea.
“Ndugu yangu, suala lilotuleta
Tanga ni kuchukua kombe, kwa hiyo bado hatujamaliza. Nadhani vijana wangu
wameanza kunielewa sasa. Kuna mtu atapigwa nyingi hapa, mtashangaa. Tunamsubiri
huyo anayekuja naye apate zake, hatuna kitu kingine sisi,” alisema.
Wachezaji wa Mpira wa
Miguu walioiwakilisha Mahakama katika mchezo huo walikuwa Fahamu Kibona; Iman
Patson; Gisbert Chentro; Akida Mzee; Emmanuel Mwamole; Selemani Magawa; Frank
Obadia; Gabriel Tabana; Martin Mpanduzi; Mwinjuma Bwanga, Shamte Seif, Hassan Aufi; Nassoro Mwampamba; Kelvin
Rutalemwa; Shabiru Hood; David Mnubi; Beatus Simwanza na Timoth Mwakisambwe.
Viongozi ambao
wameambatana na Timu ni Mwenyekiti Wilson Dede, Makamu Mwenyekiti Fidelis
Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Katibu Mkuu Msaidizi Theodosia Mwangoka, Mweka
Hazina Rajab Ally, Timu Meneja Antony Mfaume, Afisa Michezo Nkrumah Katagile na
Mjumbe Mwakilishi wa SHIMIWI Taifa Shaibu Kanyochole.
Mashindano ya SHIMIWI
ambayo yalianza tarehe 1 Octoba, 2022 na kufunguliwa rasmi tarehe 5 Octoba,
2022 yanafanyika katika viwanja tofauti tofauti ikiwemo Viwanja vya Mkwakwani,
Shule ya Sekondari Popatlal, Galanos Sekondari, Bandari, Shule ya Tanga, Polisi
Chumbageni na Viwanja vya Gymkhana kwa kuhusisha michezo kadhaa.
Mwalimu wa Timu ya Mahakama Sports Spear Mbwembwe kiongea na wachezaji wakati wa mapumziko.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni