·Baada ya kuwafumua Mambo ya Ndani, Waziri Mkuu Sera
·Wapinzani wapoteana, kila mmoja aondoka na njia yake
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Tanga
Timu ya Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanawake na Wanaume leo tarehe 12 Octoba, 2022
zimetinga katika hatua ya fainali baada ya kuzichakaza vibaya timu za Mambo ya
Ndani na Waziri Mkuu Sera katika mchezo wa nusu fainali kwenye mashindano ya
Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika
jijini hapa.
Mahakama Sports Wanawake
ilifikia hatua ya nusu fainali baada ya kuwanyoa RAS Iringa, huku Kamba Wanaume
wakifika katika hatua hiyo baada ya kushinda rufaa yake dhidi ya Timu ya
Uchukuzi ambayo ilichezesha mamluki kwenye robo fainali.
Ilikuwa mchezo wa Kamba
Wanawake ulioanza kuchezeshwa majira ya saa moja asubuhi katika Viwanja vya
Shule ya Sekondari Usagala ambapo Mahakama Sports waliwakaba koo Waziri Mkuu
Sera kila mbinu waliyotumia. Mchezo huo mzuri wa nusu fainali ulianza kwa
Waziri Mkuu Sera kuwavizia Mahakama Sports ili waweze kuwatoa kwenye mchezo.
Hata hivyo, Mahakama
Sports ambao walionekana kuwa na stamina na nguvu za kutosha walisimama imara
na kufanikiwa kuwagalagaza wapinzani wao katika mzunguko wa kwanza.
Mzunguko wa pili
ulipoanza Mahakama Sports hawakuwa na mjadala na mtu ambapo Waziri Mkuu Sera alikamuliwa
mara moja na kuachwa hawana cha kufanya zaidi ya kujisalimisha na kuwaacha
Mahakama Sports wakiondoka na ushindi.
Baada ya mchezo huo, Kamba
Wanaume ilifuata ambapo Mambo ya Ndani walianza kwa kasi kwa kuwavuta Mahakama
lakini kabla ya kupata ushindi kibao kikawageukia ambapo Mahakama Sports
iliwapigisha kwata kwa mvuto mmoja na kujikuta wanalamba nyasi katika mzunguko
wa kwanza.
Katika mzunguko wa pili,
Mahakama Sports haikutoa nafasi yoyote kwa wapinzani wao kujitutumua na
haikuchukua muda wakaumaliza mchezo huo bila kumhurumia mtu yoyote ambapo
walitoa kichapo cha maana kwa Mambo ya Ndani na kuwafanya wapinzani hao
kupoteana na baadaye kuondoka katika uwanja kila mmoja na njia yake.
Kwa matokeo hayo, Timu ya
Mahakama Sports imetinga fainali ambapo Kamba Wanaume itakutana na Ikulu, ambao
katika hatua ya makundi walikipata cha moto, huku Kamba Wanawake wakikutana na
Uchukuzi.
Akizungumza baada ya
mchezo huo, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amesema bado hawajamaliza
kwani lengo lao walilojiwekea ni kuchukua ubingwa.
"Tunatambua
wapinzani wetu walijaribu kutuzuia kwa kuchezesha mamluki baada ya kuwawashia
moto mkali, lakini sisi hatuzuiliki. Yoyote atakayekuja mbele yetu atapokea
kichapo na siku ya fainali kichapo kitakuwa kikali zaidi. Ikulu tunawajua,
tuliwachapa kwenye makundi na kwenye fainali watapata haki yao," alisema.
Wachezaji wa Kamba
Wanawake ni Zahara Abdallah, Beatrice Dibogo, Judith Mwakyalagwe, Melina Mwinuka,
Dotto Mlandula, Rebecca Mwakabuba, Salma Mwamende, Sarafina Mkumbo, Mariam
Mayala, Zawadi Amir, Namweta Mcharo, Valeria Ntyangili, Anna Hebron, Lucy
Mbwaga, Rose Mwalongo na Tumaini Kizito.
Katika mchezo wa Kamba
Wanaume, Mahakama Sports inawakilishwa na Leonard Kazimzuri, Yuda Mgalla,
Patrick Mundwe, Denis Kipeta, Joseph Chokela, Mjuni Denis, Komba Mussa, Mochiwa
Marko, Abdul Mumini, Mushi Martin, Magesa Phabian, Emmanuel Datsan, Robert
Oguda, Rajab Mwaliko, Fidelis Choka na Exavery Kasembe.
Viongozi ambao wameambatana na Timu ni Mwenyekiti Wilson Dede, Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Katibu Mkuu Msaidizi Theodosia Mwangoka, Mweka Hazina Rajab Ally, Timu Meneja Antony Mfaume, Afisa Michezo Nkrumah Katagile na Mjumbe Mwakilishi wa SHIMIWI Taifa Shaibu Kanyochole.
Bendera ya Mahakama ya Tanzania ikipepea katika Mashindano ya SHIMIWI Tanga.
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanawake ikijiandaa kuwashughulikia Waziri Mkuu Sera.
Timu ya Waziri Mkuu Sera ikijiandaa kukamuliwa na Mahakama Sports.
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanawake (juu) ikiwashughulikia Timu ya Waziri Mkuu Sera (chini) ambao walilamba tamu chini na baadaye kusambaratika.
Wababe wa Kamba wakiondoka eneo la tukio baada ya kumshughulikia mtu.
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume ikijiandaa kwa mapambano na Mambo ya Ndani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni