Na Faustine Kapama-Mahakama, Tanga
Mbinu za Timu ya Uchukuzi
kuikwamisha Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume
kushiriki mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali
(SHIMIWI) zimegonga mwamba.
Hatua hiyo inatokana na
uamuzi wa Kamati ya Rufani ya SHIMIWI kuikubali rufaa iliyowasilishwa na
Mahakama Sports kupinga ushindi waliopata Uchukuzi kwenye mchezo huo kwa
kuchezesha mamluki, yaani watu wasio na sifa ya kushiriki mashindano hayo.
Katika rufaa hiyo,
Mahakama Sports iliwasilisha sababu za rufaa tano, ikiwemo mmoja wa waamuzi
waliochezesha mchezo huo kuwa mwajiriwa wa Uchukuzi na baadhi ya wachezaji
hawana sifa za kushiriki mashindano ya SHIMIWI.
Sababu zingine ilikuwa
baadhi ya kadi za wachezaji wa Uchukuzi ziligushiwa, kutozingatiwa kwa kanuni
za mchezo wa kamba na mwamuzi kuruhusu mchezaji aliyekatiwa rufaa ya kutokuwa
mtumishi wa Wizara ya Uchukuzi kucheza wakati majibu ya rufaa bado hayajatolewa.
Wakati wa kusikiliza
rufaa hiyo, uongozi wa Majakama Sports chini ya Mwenyekiti wake Wilson Dede
uliunda timu ya wataaalamu ikiongozwa na Mushi Martin kushughulikia rufaa hiyo ambayo ilijumuisha wanasheria
nguli na maafisa utumishi waliobobea katika fani hizo.
Ilipofika wakati wa
kusikiliza, Kamati ya Rufaa ilielekeza Mahakama Sports kuanza kuthibitisha sababu
ya tatu, ambayo inahusu kugushi kwa kadi za wachezaji. Timu hiyo ya wataalamu iliwabana
Uchukuzi vilivyo na kushindwa kufurukuta.
Baada ya kubanwa mbavu
zote, kati ya wachezaji watatu waliolalamikiwa, mmoja alishindwa kabisa
kuthibitisha uhalali wa utumishi wake. Mchezaji huyo alijaribu kujitutumua
akaomba apewe muda wa kutosha kuwasilisha stakabathi ya mshahara.
Hata hivyo, timu ya Mahakama
ikaanza kumwaga utalaamu wa matumizi Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(TEHAMA) mbele ya Kamati na kuwaeleza kuwa stakabadhi hiyo inaweza kupatikana
hata kwa njia ya mtandao kwa mtumishi kuweka namba yake ya cheki hata kwenye
simu janja.
Baada ya kukabwa koo kila
kona, Uchukuzi wakasalimu amri. Kutokana na hatua hiyo, Mahakama ikawa
imethibitisha sababu hiyo ya kugushi kadi za wachezaji bila kuacha shaka yoyote
kwa mchezaji huyo mmoja mamluki.
Timu hiyo ya Mahakama
ilipoanza kuthibitisha sababu zingine kwa kuzingatia ushahidi mzito
uliokusanywa, Mwenyekiti wa Kamati ya Rufaa akawasihi waiachie meza kwa vile
sababu iliyothibitishwa ya kughushi inatosha kufikia uamuzi wa rufaa hiyo.
Kutokana na uamuzi huo,
Uchukuzi ikanyang'anywa ushindi na Mahakama kufanikiwa kuchumpa hadi nusu
fainali ambapo leo tarehe 12 Octoba, 2022 imepambana na Timu ya Wazara ya Mambo
ya Ndani na kuitoa kamasi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Latifa Mansour aliitembelea kambi ya Timu ya Mahakama na
kuwapa pole kufuatia misukosuko wanayopitia na kuwatia moyo. Aliwataka kuwa
wavumilivu na kuendelea kudumisha nidhamu kama ilivyo desturi ya watumishi wa
Mahakama.
Viongozi wa Mahakama
Sports wamemtaarifu Jaji Mfawidhi huyo kuwa wachezaji wote wapo salama na
wanazingatia taratibu zote za kambi na kuishi kwa nidhamu inayotakiwa.
Wamemuhakikishia kuwa watazingatia maelekezo yake yote aliyoyatoa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni