Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani amevitaka vyombo vya
habari nchini kujenga utamaduni wa kuandika habari zinazohusu mazuri yanayofanywa
na Mhimili wa Mahakama ili wananchi wajenge imani na Mhimili huo.
Akizungumza
na wadau wa utoaji haki nchini wakati wa Mkutano wa Tume ya Utumishi wa
Mahakama na wadau hao mjini Dodoma, Jaji Kiongozi amesema kuna umuhimu mkubwa
wa vyombo vya habari kushiriki shughuli za uboreshaji wa huduma za Mahakama kwa
kuufikishia Umma taarifa sahihi za mapinduzi ya kihuduma.
“Endeleeni
kufichua mapungufu yaliyothibitika dhidi ya Mahakama lakini msiishie hapo,
zungumzieni na mazuri pia kuhusu Mahakama ili wananchi wajenge imani na sisi”,
alisema Jaji Kiongozi.
Alisema
ndani ya Mahakama kuna mifumo imara ya kuwajibishana zikiwemo Kamati za maadili ya Maafisa wa Mahakama
ngazi za mikoa na wilaya ambazo ni muhimu wananchi wakazifahamu na kuzitumia
kuwasilisha malalamiko yao kuhusu utendaji kazi wa Maafisa wa Mahakama wakiwemo
Majaji na Mahakimu.
“Ni
watanzania wangapi wanafahamu kuwa Jaji au Hakimu anaweza kufikishwa mbele ya
kamati ya maadili na changamorto zake za kimaadili zikasikilizwa na kutolewa uamuzi,
na je ni wangapi wanajua uwepo wa kamati hizi za maadili?”, alihoji Jaji
Siyani.
Alisema
ni mara chache vyombo vya habari vikaripoti kuhusu matendo mazuri yanayofanywa
na watumishi wa Mahakama kama vile Mtumishi wa Mahakama kukataa rushwa japokuwa
wako watumishi wengi wanafanya hivyo.
Alisema
vyombo vya habari havina budi kujenga utamaduni wa kuandika mazuri ili jamii
ifahamu kuwa wako watumishi waadilifu, wanaoweza kuaminika na wenye kufanya
kazi kwa bidii.
Akizungumzia
kasi ya umalizwaji wa mashauri mahakamani, Jaji Kiongozi amewataka wajumbe wa
kamati za kusukuma mashauri ngazi za wilaya na mikoa kuhakikisha wanahudhuria
vikao vya kamati hizo ili vilete tija iliyotarajiwa. Alisema endapo italazimika
wajumbe hao kuwakilishwa basi wawakilishi wao wawe ni wale wenye kutoa maamuzi
ndani ya vikao hivyo.
Kuhusu
safari ya Mahakama kuelekea matumizi kamili ya TEHAMA, Jaji Kiongozi alisema
Mhimili huo umedhamiria kuachana na matumizi ya karatasi ifikapo mwaka 2025,
kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa kuhakikisha kwamba kasi ya utoaji haki inaimarika
kupitia matumizi hayo ya Teknolojia.
Aidha
Jaji Siyani aliwashauri wadau wa utoaji haki kujiandaa kuingia kwenye matumizi
ya TEHAMA kwa kuweka mipango sawasawa na Mahakama ili wasikwamishe juhudi za Mahakama
na pia kusaidia kuondokana na mlundikano wa mashauri mahakamani.
Kwa
upande wa Mawakili, Jaji Siyani amewataka kuacha kutumia mbinu za kiufundi
kuchelewesha upatikanaji wa haki mahakamani. Amewataka Mawakili hao pia
kuwasaidia wadaawa kwa kuwajengea mazingira ya kupatanisha kwa kuwa ni takwa la
kikatiba.
Tume
ya Utumishi wa Mahakama imemaliza ziara yake katika mkoa wa Dodoma na kuendelea
na ziara mkoani Singida. Mkoani Dodoma, wajumbe wa Tume hiyo walikutana na
wajumbe wa kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya Mkoa na wilaya Pamoja
na wadau wa utoaji haki.
Wadau wa Mahakama wakiwa katika kikao cha Tume jana mjini Dodoma.
Sehemu ya Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye kikao cha Tume na Wadau jana mjini Dodoma.
Sehemu ya Viongozi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye kikao cha Tume na Wadau jana mjini Dodoma. Katikati ni Naibu Katibu wa Tume (Ajira, Uteuzi na Upandishaji Vyeo) Bi. Enziel Mtei, kulia ni Naibu Katibu wa Tume (Nidhamu na Maadili) Bi. Alesia Mbuya na kushoto ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmilla Sarwatt.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni