Na Angel Meela, Mahakama-Arusha
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa
kushirikiana na Mahakama ya Tanzania pamoja na Taasisi isiyo ya kiserikali
inayojihusisha na uhifadhi wa Mazingira na usalama wa Wanyamapori ‘PAMS Foundation’ kinaendesha mafunzo ya uendeshaji wa mashauri ya makosa dhidi ya
wanyamapori ikiwepo ujangiri na makosa yanayohusiana na hayo kwa wadau wa haki
jinai ili kuwawezesha kuendesha ipasavyo mashauri hayo.
Akifungua mafunzo hayo ya siku tano (5) jana tarehe 10 Oktoba, 2022 yanayofanyika katika ukumbi wa ‘Palace Hotel’ jijini Arusha, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
(IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe.Dkt. Paul
Kihwelo alisema lengo la mafunzo
hayo ni kuwaleta pamoja wadau wa haki jinai na kubadilishana uzoefu kwenye maeneo
mbalimbali ikiwemo sheria za kimataifa na kitaifa za wanyamapori na ushahidi.
“Mafunzo haya yanatarajia kuwafikia Majaji 15,
mahakimu 75, waendesha mashitaka 25 na wapelelezi 25 katika mafunzo kama haya
yatakayofanyika sehemu mbalimbali,” alisema Mhe. Kihwelo.
Jaji Kihwelo alisema kuwa, katika
mafunzo hayo watajadiliana kuhusu vitu gani vya kuboresha kwenye upelelezi hadi hatua ya uendeshaji wa mashauri hayo ili waweze kutenda
haki na kuongeza kuwa, changamoto zinazojitokeza katika uendeshaji wa
mashauri hayo ni pamoja na upelelezi na suala la ukusanyaji wa vielelezo.
“Mafunzo haya yana lengo la kuwaleta pamoja wadau wote na
hivyo kubadilishana uzoefu kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo Sheria za kimataifa na kitaifa za wanyamapori na
ushahidi, uandishi bora wa hukumu, utoaji wa adhabu, utekelezaji wa amri za Mahakama katika mashauri ya wanyamapori, pamoja
na upelelezi na uendeshaji wa mashauri ya makosa dhidi ya wanyamapori na makosa
yanayohusiana na hayo,” alibainisha Jaji Kihwelo.
Mhe. Kihwelo alitumia nafasi hiyo pia kumshukuru Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.
Prof. Ibrahim Hamis Juma, uongozi
wa Mahakama
pamoja na ‘PAMS Foundation’ kwa ushirikiano ambao wameuonesha tangu kuanza kufanyika kwa mafunzo haya.
Aidha; Mkuu huyo wa Chuo aliongeza kwamba, baada ya mafunzo hayo, anatarajia washiriki watakua bora zaidi na pia watakua wametimiza lengo kwani hiyo ndio fursa pekee ya kujadiliana maeneo yote yenye changamoto.
Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamad Khamis alisema kuwa, "Rais Samia Suluhu Hassan alizindua filamu
ya 'Royal Tour' lengo likiwa ni kuvutia wawekezaji na watalii, hivyo kama
hatutawalinda ile kazi itakuwa ya bure (Royal Tour) na tutakuwa na athari kubwa kiuchumi hivyo jukwaa kama hili
litasaidia kulinda rasilimali ili wageni waje na kuingiza fedha za kigeni."
Naye; Wakili wa Serikali Mwandamizi
na Wakili Mwendesha Mashitaka Kiongozi Mkoa wa
Singida, Karen Mrango alisema eneo hilo la wanyamapori kuwa muhimu ni lazima juhudi za wadau
zifanyike ili kulinda na kutunza rasilimali zilizopo.
Mafunzo hayo ya siku tano ambayo yamefunguliwa
na Mhe. Dkt. Kihwelo ambaye amezindua rasmi mtiririko wa mafunzo ya namna hiyo ambayo yatafanyika
pia kwa makundi mengine ya washiriki pamoja na Maafisa
wengine, ufunguzi huo umehudhuriwa pia na Bw. Joseph Pande, Naibu Mkurugenzi wa
Mashtaka na Maafisa kutoka Mamlaka ya Ngorongoro na TANAPA.
Kundi la kwanza la washiriki litajumuisha Majaji wa Mahakama Kuu, Waendesha Mashtaka Waandamizi na Wapelelezi Waandamizi pekee ambao watashiriki mafunzo hayo jijini Arusha kwa siku tano kuanzia tarehe 10 hadi 14 Oktoba 2022, wakifuatiwa na kundi la pili la Mahakimu, Waendesha Mashtaka na Wapelelezi ambao watashiriki mafunzo hayo kuanzia tarehe 17 hadi 21 Oktoba 2022. Kundi la mwisho la Mahakimu, Waendesha Mashtaka na Wapelelezi litashiriki mafunzo hayo katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kuanzia tarehe 24 hadi 28 Oktoba 2022.
Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni Maafisa wa Mahakama
ya Tanzania wakiwemo Majaji na Mahakimu
na watumishi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya Mashtaka ya Taifa,
Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na kadhalika.
Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano kati
ya ‘IJA’ na ‘PAMS Foundation’ ambayo yalisainiwa tarehe 23 Juni, 2022 jijini Dar es Salaam kati ya Mkuu wa Chuo
pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa ‘PAMS Foundation.’
Mkurugenzi wa Mafunzo na Operesheni kutoka Taasisi ya PAMS Foundation, Bw. Samson Kassala akitoa neno kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Bi. Krissie Clarkson wakati wa ufunguzi wa Mafunzo hayo.
Mgeni rasmi ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wote wa Mafunzo hayo. Wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga, wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa Mafunzo na Operesheni kutioka Taasisi ya PAMS Foundation, Bw. Samson Kassala na Washiriki wengine wa mafunzo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni