·Mahakama Sports yahujumiwa kila kona baada ya kuonekana tishio
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Tanga
Katika hali isiyokuwa ya
kawaida, mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali
(SHIMIWI) yanayofanyika jijini hapa leo tarehe10 Octoba, 2022 yameingia doa
kutokana na dosari lukuki, ikiwemo viongozi kuruhusu baadhi ya timu kuchezesha
mamluki.
Dosari zilianza
kujionyesha mapema asubuhi wakati wa mchezo wa kamba kwa lengo la kuihujumu Timu
ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume iliyokuwa inashiriki mchezo
huo. Katika mchezo huo, Mahakama Sports ilikuwa imenyane na Uchukuzi kwa kufuata
kanuni za mashindano, lakini ilichezeshwa kibabe huku viongozi wa SHIMIWI
wakiruhusu Uchukuzi kuchezesha wachezaji ambao siyo watumishi.
Kwa kwa mujibu wa kanuni
za mashindano, kila timu inatakiwa kuleta wachezaji wenye vitambulisho ambavyo
vinaonyesha picha ya mshiriki, namba yake ya cheki, tarehe ya ajira, kituo
chake cha kazi na kitambulisho hicho kisainiwe na afisa wa michezo wa Idara au Wizara
yake.
Wakati ulipowadia wa
kuchezwa mchezo huo katika Viwanja vya Shule ya Ufundi Tanga, mmoja wa
wachezaji wa Uchukuzi hakuwa na kitambukisho na baadhi ya vitambulisho vya
wachezaji wengine havikuwa na kumbukumbu muhimu, ikiwemo namba za cheki za
watumishi hao.
Lakini cha kushangaza,
mwamuzi wa mchezo huo ambaye inasadikiwa ni mtumishi wa Uchukuzi pamoja na
baadhi ya viongozi wa SHIMIWI wakaamuru mchezo huo ufanyike, kitendo kilichoifanya
Timu ya Mahakama kucheza chini ya mgomo na kupoteza mpambano huo.
Viongozi wa Mahakama
wameamua kuchukua hatua, ikiwemo kukata rufaa ambayo kuna figisufigisu
zinaendelea za kutosikiliza rufaa hiyo kwa wakati ili kuibeba timu ya Uchukuzi.
Baada ya mchezo huo, figisufigisu
zilihamia katika Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Popatlal majira ya jioni
ambapo Timu ya Mahakama Sports Mpira wa Miguu ilikuwa icheze na timu ya RAS
Simiyu, lakini cha kushangaza Timu ya Uchukuzi ilivamia uwanja huo na kusababisha
mchezo huo uahirishwa katika mazingira ya kutatanisha bila ya viongozi wa
SHIMIWI kuchukua hatua.
Figisu zingine zenye nia
ya kuihujumu Timu ya Mahakama zilijitokeza wakati wa mchezo wa riadha ambapo Mahakama
ilishiriki katika mbio za kupokezana vijiti. Lakini cha kushangaza Timu hiyo ya
Mahakama iliondolewa kwenye mashindano hayo katika mazingira ya kutatanisha.
Mahakama Sports iliingia katika mchezo wa robo fainali ya mchezo huo baada ya
kushika nafasi ya tatu kwenye makundi.
Janja janja nyingine
ilijitokeza wakati mchezaji wa Mahakama mbio za wazee alishika nafasi ya tatu,
lakini waamuzi wakachomeka jina na mtu mwingine na mtumishi huyo kupewa nafasi
ya nne, hivyo kukosa medali aliyokuwa amestahili kuipata.
Mahakama Sports ipo Tanga
kushiriki katika michezo mbalimbali inayoendeshwa na SHIMIWI, ikiwemo Kamba
Wanaume, Kamba Wanawake, Riadha, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, bao, pamoja
na michezo mingine mingi ya ndani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni