·Kamba Wanawake watangulia nusu fainali
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Tanga
Timu ya Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanawake leo tarehe 10 Octoba, 2022
imeizamisha RAS Iringa na kufanikiwa kuingia hatua ya nusu fainali katika
mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI)
yanayofanyika jijini hapa.
Mchezo huo mzuri wa robo
fainali uliofanyika majira ya saa moja asubuhi katika Viwanja vya Tanga
Technical School ulianza kwa timu zote kutunishiana misuri, huku RAS Iringa
wakijaribu kuwakazia wapinzani wao.
Hata hivyo, Mahakama
Sports walisimama imara na kuwaondoa kwenye mchezo baada ya kuwakata pumzi na
kufanikiwa kupata ushindi katika mzunguko wa kwanza. Katika mzunguko wa pili,
Mahakama Sports hawakuwa na mzaha na mtu na haikuwachukua muda kumaliza mchezo huo
kwa kuwaminya kisawasawa RAS Iringa.
Kufuatia matokeo hayo,
Mahakama Sports Kamba Wanawake itakutana na Waziri Mkuu Sera kwenye nusu
fainali. Timu ya Waziri Mkuu Sera wamefika katika hatua hiyo baada ya kuwatoa
kwenye mashidano hayo timu ya Tamisemi.
Kabla ya kuingia kwenye
nusu fainali, Mahakama Sports ilishiriki katika 16 bora na kushinda mechi zake
zote. Ilicheza mechi yake ya kwanza ya
makundi na RAS Singida ambapo ilitoa kichapo kikali.
Mechi yake ya pili
ilikutana na Maji ambayo yalikamuliwa kisawasawa kwa mizunguko yote miwili na
katika mechi ya tatu ilipangiwa na RAS Manyara ambao waliingia mitini baada ya
kuogopa kupokea dozi iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili yao. Mahakama Sports
ilikutana na Viwanda na kuisambaratisha vikali katika mechi yake ya nne.
Wachezaji wa Kamba
Wanawake ni Zahara Abdallah, Beatrice Dibogo, Judith Mwakyalagwe, Melina
Mwinuka, Dotto Mlandula, Rebecca Mwakabuba, Salma Mwamende, Sarafina Mkumbo,
Mariam Mayala, Zawadi Amir, Namweta Mcharo, Valeria Ntyangili, Anna Hebron,
Lucy Mbwaga, Rose Mwalongo na Tumaini Kizito.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni